August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Barza ya Mchukucha yavamiwa

Kundi la watu wenye kufunika uso Zanzibar (Mazombi)

Spread the love

SAA chache baada ya viongozi wa serikali mkoa wa Mjini Magharibi kuongoza kisomo cha dua ya kuiombea Zanzibar amani na salama, askari wa serikali wamevamia baraza inayokaliwa na wafuasi wa Suleiman Mchukucha, na kujeruhi watu kadhaa, anaandika Jabir Idrissa.

Mmoja wa watu waliojeruhiwa ni Maulid Abdalla Chawa, babu wa umri wa miaka 72, ambaye wakati wavamizi walipofika na kuanza kushambulia watu, yeye alikuwa amejinyoosha kwenye jamvi akisubiri muda wa kurudi kujipumzisha nyumbani kwake eneo la Taveta, mjini Zanzibar.

“Nilikuwa nimejinyoosha jamvini walipokuja. Ghafla nilisikia sauti za watu wanaotoa maneno ya matusi, nikainuka lakini kabla sijafanya lolote, nikajikuta narudishwa chini kwa kipigo. Vijana wawili walinipiga nikaumia kama unavyoona,” amesema mzee Chawa.

Mzee Chawa alifanya mazungumzo na MwanaHALISI Online kwa njia ya simu ya mwanabaraza mwenzake ambaye siku ya tukio hakuwepo barazani. Ameumizwa mguu sehemu ya muundi kwa kupigwa marungu. Alilazimika kupelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu.

Kabla ya kupelekwa hospitali, mzee Chawa na wenzake wanne walioumizwa katika mashambulizi yaliyofanywa na askari waliofika barazani wakiwa wamejifunika nyuso zao kwa vitambaa vyeusi, walipelekwa Kituo Kidogo cha Polisi cha Kijitoupele ambako walipatiwa fomu za kupatia matibabu. Malalamiko yao kituoni, yalisajiliwa kwa Kumb. Na. RB.2248.

Watu wengine waliojeruhiwa katika tukio hilo ni Aziz Mohamed Ali (42), Mbaraka Pandu Makame (40), Suleiman Vuai Lobilo (56) ambao nao walitibiwa hospitalini kutokana na majeraha waliyoyapata kwenye sehemu mbalimbali za miili.

Tukio hilo lilitokea kiasi cha saa 3 usiku siku ya 6 Desemba 2016, kwenye baraza iitwayo Super Power ambayo inafadhiliwa na Suleiman Mnoga Mchukucha, aliyegombea uwakilishi jimbo la Pangawe kupitia Chama cha Wananachi (CUF) katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa 25 Oktoba 2015, ambao ulihujumiwa kwa kufutwa 28 Oktoba 2015, na Jecha Salim Jecha, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Mchukucha ni mwanasiasa kijana aliyejipatia umaarufu mkubwa kutokana na harakati zake zilizomfikisha hadi kurekodiwa moja ya hotuba zake majukwaani na kuenezwa kwenye mitandao ya kijamii ambamo anaonekana akinengua burudani iliyokuwa inatolewa mkutanoni na vijana wa CUF.

Mchana wa siku hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohamed Mahmoud, akiwa mgeni rasmi, aliongoza wananachi kwenye hafla ya kusoma dua iliyoelezwa kuwa ililenga kuiombea nchi amani na salama.

Katika hafla hiyo walihudhuria viongozi mbalimbali wa serikali na CCM, pamoja na viongozi wa dini wakiongozwa na masheikh walioko Ofisi ya Mufti wa Zanzibar. Hata Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salim alihudhuria.

Hafla hiyo ilionekana kama imeandaliwa na mtandao wa CCM chama ambacho kinashikilia hatamu za serikali baada ya kusimamia kuhujumiwa kwa uchaguzi mkuu ambao waangalizi wa ndani na nje ya nchi zikiwemo asasi za kikanda na kimataifa, waliueleza kuwa ulikuwa huru, wa haki na uliofanyika katika mazingira ya amani.

CCM ilitangazwa mshindi wa uchaguzi ulioitishwa na Jecha na mgombea wake wa urais, Dk. Ali Mohamed Shein akaapishwa kuwa rais. Matokeo ya uchaguzi wa marudio yalitangazwa siku hiyohiyo ya 20 Machi 2016 ulipofanyika, kinyume na ilivyokuwa kwa uchaguzi mkuu ambako katika siku ya 28 Oktoba iliyotarajiwa tume itangaze matokeo ya urais, Jecha aliyekuwa mafichoni alitangaza kuufuta pamoja na matokeo yake yote.

CUF iliyomsimamisha Maalim Seif Shariff Hamad kuwania urais, imeongoza vyama vingine na wagombea wao kupinga kufutwa kwa uchaguzi kwa msimamo kuwa kulikuwa ni hujuma na ukiukaji wa sheria na katiba ya nchi. Wanasema si Jecha wala Tume ya Uchaguzi yenye mamlaka ya kufuta uchaguzi uliokwishafanyika.

Ufutaji wa uchaguzi na hadi ulipofanyika uchaguzi wa marudio, na mpaka wakati huu matukio ya askari wa vikosi vya serikali kuvamia maeneo ya makazi ya watu hasa kunakosadikika ngome za upinzani, yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara lakini hakuna mtu aliyekamatwa na kushitakiwa kwa uhalifu huo. Hata hivi juzi Jeshi la Polisi lilitangaza kama kawaida yake, kufanya uchunguzi wa tukio la Taveta.

 

error: Content is protected !!