December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Baraza la Mawaziri latoa maelekezo ajali ya Precision

Spread the love

BARAZA la Mawaziri nchini Tanzania limeelekeza vitengo vyote vinavyohusika na kukabiliana na majanga viimarishwe ili kuongeza uwezo wa kukabiliana na majanga. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Baraza hilo lililoketi kwa dharura leo tarehe 14 Novemba, 2022, jijini Dodoma, kujadili ajali ya ndege ya Precision iliyotokea Novemba 6 mwaka huu, limeelekeza pia wataalamu wa ndani washirikiane na wataalamu wa nje katika uchunguzi na baadae kutoa taarifa juu ya chanzo cha ajali na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

Hayo yamebainishwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msingwa, mbele ya waandishi wa habari muda mchache baada ya kumalizika kwa kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri, Rais Samia Suluhu Hassan.

Msingwa amesema wakati uchunguzi ukiendelea lazima watanzania watambue kuwa zipo hatua tatu muhimu zinazofanyika katika uchunguzi na kuwataka kuendelea kuwa wavumilivu hadi pale ripoti itakapokamilika.

“Kwanza timu ya uchunguzi wa ajali ya ndege ambayo inafanya uchunguzi wake na inatoa maelezo ya awali ndani ya siku 14 na baada ya timu hiyo inafuatiwa na ripoti ya awali yaani ‘preliminary report’ ambayo inatolewa ndani ya siku 30 na hatimaye tutamaliza na ripoti kamili ambayo inatolewa ndani ya miezi 12 baada ya ajali kutokea kwahiyo hatua hizi zote tayari zimeanza…ripoti hii itakapokamilika tutatoa taarifa kwa wananchi,” amesema Msingwa.

Aidha amesema Bazara la Mawaziri limetoa shukrani kwa wote waliohusika katika ukoaji wa manusura ikiwemo wananchi, wavuvi, timu ya uokoaji na maofisa wa afya.

Ajali ya ndege ya Precision ilitokea baada ya ndege hiyo Na. 5H-PWF aina ya ATR 42-500 kuanguka Ziwa Victoria mita chache kutoka uwanja wa ndege wa Bukoba kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutokana na hali mbaya ya hewa. Ilisababisha vifo vya watu 19 akiwemo rubani na msaidizi wake kati ya watu 43 waliokuwamo katika ndege hiyo iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam.

error: Content is protected !!