January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Baraza la Magufuli hili hapa

Spread the love

RAIS John Magufuli leo ametangaza Baraza la Mawaziri lenye jumla ya wizara 18 huku wizara nne zikiwa bado kutangazwa mawaziri wake. Anaandika Yusuph Katimba … (endelea).

Mbele ya waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alitaja majina ya mawaziri wake na wizara watakazotumikia katika kipindi chake cha uongozi.

Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Utumishi na Utawala Bora ina mawaziri wawili ambao ni George Simbachawene na Angela Kairuki, naibu ni Jafo Suleiman Said.

January Makamba ametajwa kuongoza Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira naibu wake akiwa Lugaha Mpina. Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira Vijana na Walemavu itaongozwa na Jenista Mhagama huku akisaidiwa na manaibu wawili ambao ni Dk. Abdallah Posi na Antony Mavunde.

Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi itaongozwa na Mwiguli Nchemba huku William Tate Ole Nasha akiwa naibu waziri. Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano haijatangazwa waziri wake ambapo naibu waziri ni Injinia Edwin Mgonyani.

Rais Magufuli hajatangaza waziri kwenye Wizara ya Fedha na Mipango lakini naibu waziri amemtaja kuwa Dk. Ashantu Kuaji. Wizara ya Nishati na Madini amekabidhiwa Prof. Mwijarubi Muhongo ambapo naibu waziri wake ni Dk. Mudadi Kaleman.

Wizara ya Katiba na Sheria imeelekezwa kwa Dk. Harrison Mwakyembe huku naibu waziri akiwa bado hajatangazwa. Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa ikienda kwa Dk. Augustine Mahiga ambapo naibu waziri akiwa Dk. Susan Kolimba.

Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa itaongozwa na Dk. Hussein Mwinyi ambapo naibu wake hajatangazwa. Wizara ya Mambo ya Ndani imekwenda kwa Dk. Charles Kitwanga ambapo naibu waziri hajatangazwa.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameendelea kuwa William Lukuvi ambapo Angelina Mabula ametajwa kuwa naibu wake. Wizara ya Maliasili na Utalii haijatangazwa waziri wake ambapo naibu waziri ametajwa kuwa ni Injinia Ramo Makani.

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji itaongozwa na Dk. Charles Mwijage lakini naibu waziri bado hajatangazwa. Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi bado hajatangazwa lakini nafasi ya naibu waziri imekwenda kwa Injinia Stella Manyanya.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto itaongozwa na Ummy Mwalimu ambapo naibu waziri wake ni Dk. Hamis Kigwangala.

Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo itaongozwa na Nape Nnauye ambapo Anastanzia Wambura akiwa naibu wake huku Wizara ya Maji na Umwagiliaji ikiwa chini ya Prof. Makame Mbarawa huku naibu wake akiwa Isack Kamwela.

error: Content is protected !!