January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bandari, mabehewa vyamtoa jasho Sitta

Bandari ya Dar es Salaam

Spread the love

UJENZI wa gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam na ununuzi wa mabehewa chakavu ya treni ni mambo yaliyotawala mjadala wa Bunge wakati wa kujadili bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2015/16, inayoongozwa na Samuel Sitta. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Msemaji mkuu wa kambi rasimu ya upinzani bungeni kwa wizara hiyo, Moses Machali ndiye alichokonoa mjadala huo wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo, akisema ujenzi wa gati Na 13 na 14 umekuwa na utata kwa muda wa miaka mitano sasa.

Machali amesema kusuasua kwa ujenzi wa magati hizo kunaashiria uwepo wa rushwa na ufisadi kwa mamlaka zote zinazosimamia na kuratibu suala hilo.

Amesema kuwa kwa kipindi cha mwaka 2011/2012, kuliibuka utata wa suala la ujenzi huo wa magati hayo katika Bandari ya Dar es Salaam ambapo ilionekana mamlaka hiyo ilikuwa na kampuni yake iliyoiona inafaa kupewa ukandarasi wa ujenzi.

Machali amesema pamoja na hali hiyo kulizuka mvutano mkubwa kwani wizara ya Uchukuzi nayo ilionekana kuwa na mkandarasi ambaye alionekana naye anafaa kupewa kati ya utekelezaji wa ujenzi wa magati hayo.

Kwamba wakati yakifanyika hayo nchi ilikuwa haijawahi kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi huo kwa lengo la kupata gharama halisi ya utekelezaji mradi huo.

“Mamlaka ya Bandari (TPA), ilikuwa ikiimpigia chapuo kampuni ya China Communication Construction Company (CCCC) ambayo ilikusudia kujenga gati hizo kwa Sh.trilioni 1.

“Wakati huo huo palikuwepo na kampuni nyingine iliyokuwa ikipigiwa upatu na aliyekuwa waziri wa uchukuzi, Omary Nundu ipatiwe kazi ya kujenga na kumiliki bandari hiyo kwa miaka 45 chini ya mfumo unaojulikana kama BUILD OWN, OPERATE AND TRANSFER (BOOT) ambapo gharama za ujenzi ili gati 13 na 14 ziwe zimekamilika kwa mujibu wa kampuni hiyo ilikuwa ni Sh. 600 bilioni,”amesema.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuliepusha taifa kutoingia hasara ya kutumia gharama kubwa katika kutekeleza mradi huo muhimu.

“Kutokana na ukweli kwamba Tanzania kama taifa chini ya TPA na wizara hawakuwa wamefanya upembuzi yakinifu na badala yake viongozi na watendaji wa wizara pamoja na bandari walitaka kutumia upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi uliofanywa na makampuni ya kigeni tena ambayo yalikuwa na maslahi ya kutaka yapatiwe ujenzi wa magati hayo,”amesema.

Kwa mujibu wa Machali, hali hiyo yenye kuashiria utata mtupu iliyowafanya waziri na aliyekuwa naibu wake, Dk. Athuman Mfutakamba watofautiane katika kutekeleza majukumu yao kwa kuwa kila mmoja alikuwa ana kampuni aliyoonekana kuitetea ili ipatiwe ukandarasi.

“Kambi rasmi ya upinzani bungeni inaitaka serikali kulieleza Bunge na Watanzania wote, je ujenzi wa gati namba 13 na 14 utaanza lini ili kuongeza ufanisi wa bandari yetu ya Dar es Salaam. Pia serikali itoe ufafanuzi kuhusu utata wa gharama za ujenzi huo.

Kuhusu mabehewa chakavu, Machali amesema kuwa, tangu mwaka jana serikali ilisikika na kuonekana kupitia vyombo vya habari kwamba mabehewa ya treni yaliyonunuliwa kutoka nchini India ni chakavu ambayo hayana ubora unaotakiwa.

“Kwa jumla ni kwamba mabehewa hayo ya kubebea kokoto ni uozo mtupu na taifa limepata hasara kubwa kwa kuwa hayataweza kudumu huku ikielezwa kwamba zaidi ya Sh. 200 bilioni zilitumika kwa ajili ya manununzi ya mabehewa hayo.

Pia, Machali amezungumzia ufisadi katika uuzwaji wa nyumba za Tazara, akisema kuwa, imebainika kuna ufisadi unahusisha nyumba za shirika zilizopo mkoa wa Dar es Salaam na Mbeya.

Amesema mwaka 2002, uongozi wa Tanzania Zambia Railway Authority (Tazara) ulipata ruhusa toka kwa bodi ya wakurugenzi kuuza baadhi ya mali za shirika ambazo kwa maelezo yao hazikuwa muhimu kwa uendeshaji wa shirika (None core assets of the authority).

Machali ameongeza kuwa, kuuzwa kwa mali husika kulilenga kupunguza gharama za uendeshaji za shirika na kupata fedha.

Machali aliwataja baadhi ya viongozi wa Tazara, akisema wanadaiwa kujihusisha na ufisadi; hao ni Damas Ndamburo, Peter Mapunda, Evarist Laiderson, Hassan Hayeshi, Alexander Nkwamah, Godfrey Swalle, Michael Mwachiko, Anania Simbeye na Said Chamba.

Katika mjadala wa jumla, mbunge wa Kisarawe, Suleiman Jaffo (CCM), amesema watendaji wamekuwa wakihujumu nchi ili kuiharibia serikali ya CCM.

“Lazima hawa tuwashughulikie, watangazwe kwenye vyombo vya habari wahujumiwe nao. Wanaiba wanakwenda wanajenga kila mitaa nyumba,”alisema.

Mbunge wa Nkenge, Assumpta Mshama (CCM), ameitaka serikali kuinyang’anya  Kampuni ya Simon Group, uendeshaji wa mradi  wa mabasi yaendayo kwa kasi na Shirika la Usafirishaji  la Jiji la Dar es Salaam, (UDA) kwa kuwa ni matapeli.  

“Anyang’anywe hana uwezo wa kuendesha miradi hiyo, anakopa mafuta, anaandika hundi feki hata makanisa pia anawaandikia hundi ya Sh.5 milioni lakini hakuna fedha,”alisema .

Mbunge wa Tanga Mjini, Omary Nundu (CCM), ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Uchukuzi, amesema Kamati ya Bunge ilihongwa na watendaji ili wamuondoe yeye katika uwaziri.

“Mlipewa fedha na bandari ili mniondoe, mbona hanizuii. Bahati yenu nyie ningekuwepo hapa nyote mngekoma ,”amesema.

error: Content is protected !!