Friday , 19 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Balozi Seif akerwa talaka za ovyo, unyanyasaji Z’bar
Habari Mchanganyiko

Balozi Seif akerwa talaka za ovyo, unyanyasaji Z’bar

Balozi Seif Ali Iddi.
Spread the love

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ameitaka Tume ya Haki za Binadamu Tanzania kufanya wajibu wake wa kuwaelimisha wananchi kuhusu haki ili kuelewa haki zao pindi wanapokuwa na matatizo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar…(endelea)

Akizungumza ofisini kwake Vuga Mjini  Zanzibar alipotembelewa na ujumbe wa Tume hiyo wakiongozwa na Mwanyekiti wake, Jaji mataafu Mathew  Pauwa Mhina, Balozi Seif amesema, Zanzibar imekuwa na matukio mengi ya unyanyasaji wa kijinsia jambo ambalo Tume ya Haki za Binadamu inapaswa kuwaelimisha wananchi kuhusu upatikanaji wa haki.

Pia, kuwaeleza madhara ya unyanyasaji wa kijinsia, kwani kufanya hivyo kutaisaidia Serikali kuu kupata nguvu na uwezo wa ziada wa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi hususan wanawake, watoto na hata wananchi wenye mahitaji maalum.

Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, akipokea kitabu kinachohusu masuala ya haki za binadamu na utawala bora kutoka kwa Mwenyekiti na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Mathew Mhina, Walipomtembelea Ofisini kwake leo Juni 3, 2020 Vuga Mjini Zanzibar.

“Tume ya Haki za Binadamu ina kazi kubwa katika kutekeleza majukumu yake  kwa upande wa Zanzibar kutokana na migogoro na changamoto nyingi zinazowakabili wananchi hali inayosababisha mitafaruki na mifarakano miongoni mwa jamii  yenyewe.”

“Kwa hiyo, nyie kama tume, waelimisheni wananchi wa Zanzibar kufahamu sehemu ya kupata haki zao, lakini pia nyie mna jukumu kubwa la kusaidia kutatua migogoro na mifarakano inayotokea ya wananchi  kusumbuliwa  katika maeneo tofauti nchini,” amesema Balozi Seif .

Aidha , Balozi Seif ameueleza uongozi wa Tume hiyo yapo matatizo mengi yanayowakabili wananchi hasa wanawake ya kupewa ovyo talaka na matokeo yake kutelekezwa na waume zao sambamba na kuachiwa  watoto bila ya huduma hali ambayo inakuwa ni kazi kwao kutimiza majuku ya kulea watoto.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi (katikakati), akiwa kwenye picha ya pamoja na Ugeni wa Wajumbe wa Tume ya Haki za Bianadamu na utawala Bora wakati wa ziara ya tume hiyo katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar leo Juni 3, 2020.

Ametahadharisha tabia hiyo iliyoanza kuota mizizi kwa baadhi ya wanaume wasiojali utu wa binadamu ni ya hatari kwa mtoto kwa vile inawakosesha haki zao za msingi kama vile kupata elimu na huduma za afya kwa sababu ya kutokuwa na ushirikiano wa kimalezi baina ya pande mbili.

Pia, alieleza  suala  la  udhalilishaji wa wanawake na watoto  linaloikumba Dunia, hivyo watendaji na viongozi wa Tume wa lazima wajikite zaidi kushirikiana na taasisi za utoaji haki pamoja na wananchi katika vita ya kukabiliana na tatizo hilo linalochangia kupotoshwa kwa maadili ya jamii.

“Kwa sasa, masuala ya wanawake na watoto kudhalilishwa limekuwa ni jambo ambalo duniani kote ni mtihani, kwa hiyo Tume ya Haki za Binadamu jikiteni zaidi katika kufanya upembuzi wa suala hili.”

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu, Mathew Mhina na Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mohamedi Khamis Hamadi wakiwasili katika Ofisi za Makamu wa Pili wa Rais zilizopo Vuga Mjini Zanzabar.

“Ili taasisi  za utoaji haki na Serikali ipate kuwasaidia wananchi kupitia nyinyi, lakini pia msisahau kutoa elimu kuhusu haki zao kwani hiyo itawasaidia kupambana na waharifu na wavunjaji wa haki za binadamu,” alisema Balozi Seif.

Akijibu ombi la  Tume ya Haki za Binaadamu la kupewa jengo la Ofisi kwa upande wa Zanzibar,  Makamu huyo wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameshauri ujumbe wa Tume kuwa na mpango wa kujenga majengo ya kudumu ya ofisi zake Visiwani Zanzibar kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa maeneo ya ujenzi huo wakati wowote pale itapohitajika kutekelezwa mpango huo.

Kwa upande wake,  Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu Mhina, alisema Taasisi hiyo ni chombo cha umma kilichoundwa kusimamia upatikanaji wa haki za binadamu ili kusimamia utawala bora hapa nchini na kuwawezesha wananchi kupata haki zao za msingi pale inapohitajika

“Tume  ya haki za binadamu imeundwa na viongozi wake waliteuliwa na Rais John Pombe Magufuli ili kutetea haki za Watanzania bila kujali imani zao.”

“Kwa hiyo, utekelezaji wa majukumu yake upo kwa ajili ya wananchi wanaopokonywa haki zao, lakini pale ambapo watendaji  wa Tume wakienda tofauti ni masuala ya kibinadamu ya kuteleza  katika utekelezaji wa majukumu yao,” amesema Jaji Mhina

Aidha, Tume ya Haki za Binadamu Tanzania kupitia Mwenyekiti wake iliipongeza Serikali ya Jamahuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa  inayoifanya ya kuhudumia wananchi jambo ambalo uongozi wa Tume hiyo unaliunga mkono.

Makamishina wa Tume ya Haki za Binadamu Tanzania waliteuliwa na Rais Magufuli mnamo tarehe 19 Septemba Mwaka 2019, ili kuhakikisha kunakuwepo na upatikanaji wa haki kwa watanzania katika maeneno yote ya Kijamii.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

Habari Mchanganyiko

Carbon First, Ruangwa wasaini makubaliano ya biashara ya hewa ukaa

Spread the love  KAMPUNI ya Carbon First Tanzania Limited na Halmashauri ya...

Habari Mchanganyiko

CBE yawakumbuka wenye mahitaji maalum Jangwani

Spread the loveCHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimetoa msaada mbalimbali na...

error: Content is protected !!