January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Balozi Mahiga atia nia urais, azua hofu

Balozi Augustine Mahiga akitangaza nia ya kugombea urais kupitia CCM. Kulia ni mke wake, Elizabeth Mahiga

Spread the love

UJIO wa Balozi Augustine Mahiga katika mbio za kuomba uteuzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), umetajwa na wachambuzi wa siasa kuwa utabadili upepo wa makada wanaoshinda naye, kutokana na uwezo na uzoefu wake. Anaandika Jimmy Mfuru … (endelea).

Hata hivyo, hofu kubwa ya Balozi Mahiga ni rushwa iliyokithiri katika mfumo wa siasa, ambapo anaona kuwa anaweza asipitishwe kwa sababu hatatoa fedha kuwanunua wajumbe.

Baadala yake, Balozi Mahiga ambaye pia ni mwakilishi mstaafu wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, amesema kuwa akipitishwa na kushinda urais atatangaza vita dhidi ya rushwa na ufisadi huku akiimarisha misingi ya maadili.

Akitangaza nia ya kuingia katika kinyang’anyiro hicho, amesema  atalifanya suala hilo kuwa la utashi wa kisiasa kwa kushirikiana na asasi za kijamii, kiraia na mashirika ya haki za binadamu kwa kuzifanya zipaze sauti na kuwafichukua wala rushwa huku akiahidi kuunda chombo maalum cha kushughulikia suala hilo.

Kwa mujibu wa Balozi Mahiga, rushwa ikiachwa bila kufanyiwa jitihada za dhati athari yake ni kubwa katika jamii na ina madhara yake  makubwa kwa afya ya uchumi kwa nchi na ustawi wa nchi kwa ujumla.

Amesema rushwa inafanya watanzania wakose haki, jambo ambalo linasababisha kuwepo na tabaka la wasiokuwa nacho na wenye nacho na hivyo kuibua chuki kubwa ndani ya jamii ambayo inaweza kupelekea uvunjivu wa amani.

Balozi Mahiga amesema usimamiaji misingi ya umoja wa taifa ndio njia pekee iliyofanya kuiletea Tanzania uhuru kwa kuwa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere alilisimamia, hivyo naye ataendelea kusimamia na kuimarisha ili kuondoa masuala ya udini, ukabila na ukanda.

Amesema “Taifa likiwa na maadili na yakisimamiwa ipasavyo, kutakuwepo na uzalendo, umoja, uwajibikaji, kwa ustawi wa nchi na jamii kwa ujumla.”

Balozi Mahiga pia amegusia suala la amani, akisema ni la msingi katika nchi yoyote huku akitolea mfano nchi ambazo amani imepotea kama Somalia na Liberia kuwa kuirudisha ni kazi ngumu, kutokana na uzoefu alioupata akiwa mmoja wa watu waliotatua migogoro katika mataifa hayo.

Tofauti na mbwembwe zilizooneshwa na baadhi ya watangaza nia, ikiwa ni pamoja na kugharamia matangazo ya moja kwa moja katika runinga na redio, Balozi Mahiga yeye ameitisha mkutano na waadishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), na kufikisha ujumbe wake.

Historia yake

Balozi Mahiga alizaliwa 28 Agosti, 1945, huko Tosamanganga, Jimbo la Kalenga,mkoani Iringa. Amesoma elimu ya msingi katika shule za Serikali enzi ya kikoloni na kuhitimu darasa la VIII muda mfupi baada ya uhuru.

Aliendelea na masomo ya sekondari hapa hapa nchini na mwaka 1968. Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuhitimu mwaka 1971.

Baadaye alipata ufadhili na kuendelea na masomo ya juu nchini Canada katika Chuo Kikuu cha Toronto ambako alihitimu Shahada ya Uzamili kisha aliendelea na Shahada ya Uzamivu katika chuo hicho hicho akijikita katika Uhusiano wa Kimataifa na kuhitimu mwaka 1975.

Balozi Mahiga alirejea nchini akiwa na udaktari wa falsafa (PhD) na kupangiwa kazi ya kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwa mhadhiri katika Idara ya Kimataifa na Ushirikiano wa Kikanda.

Alifanya kazi hiyo kazi hiyo hadi mwaka 1977, alipohamishiwa katika Ofisi ya Rais kuwa Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo na alidumu hapo akifanya kazi pamoja na Mwalimu Julius Nyerere hadi mwaka 1980.

Kati ya mwaka 1980 hadi 1983, Balozi Mahiga alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Mwaka 1989 hadi 1992, aliteuliwa kuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Kimataifa akifanyia kazi Geneva – Uswisi na mwaka 1992 hadi 1994, Balozi Mahiga aliteuliwa kuwa Kiongozi (Mwakilishi) wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi duniani (UNHCR) mjini Monrovia, Liberia.

Mwaka 1994–1998, Balozi Mahiga alihudumu akiwa Mratibu na Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni ya Dharura ya Ukanda wa Maziwa Makuu akifanyia kazi hiyo kutokea Geneva–Uswisi na kati ya mwaka 1998 – 2002.

Aliteuliwa kuwa Kiongozi Mkuu (Mwakilishi) wa Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR) huko mjini Delhi India kabla ya kuteuliwa tena kuwa mwakilishi wa shirika hilo katika nchi za Italia, Malta na Jamhuri ya San Marino kati ya mwaka 2002 – 2003.

Balozi Mahiga amepata pia kuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika kipindi cha mwaka 2003 hadi 2010 na alishiriki kikamilifu katika mipango ya kimataifa pamoja na kusimamia mazungumzo ya kuanzishwa kwa Kamisheni ya Ujenzi wa Amani (mwaka 2005).

error: Content is protected !!