April 14, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Balozi Mahiga alivyozikwa, Samia Suluhu amwakilisha Rais Magufuli

Spread the love

SAFARI ya mwisho hapa duniani ya Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Augustine Mahiga imehitimishwa leo Jumamosi tarehe Mei 2, 2020 kwa mwili wake kuzikwa kijijini kwao katika makaburi ya Tosamaganga mkoani Iringa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Iringa … (endelea).

Balozi Mahiga alifariki dunia ghafla jana Ijumaa akiwa nyumbani kwake jijini Dodoma.

Shughuli ya mazishi ya mwanadiplomasia huyo mashuhuru imeanzisha Kanisa Katoliki la Tosamaganga kisha mwili wake kupelekwa makaburini kwa maziko.

Katika shughuli hiyo, Rais John Magufuli amewakilishwa na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan.

Wakati wote kanisani na makaburini, tahadhari mkubwa ya kujikinga Homa ya Mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona imezingatiwa kwa waombolezaji kuvaa barakoa na kukaa mbalimbali.

Akitoa salamu za Serikali, Samia amesema,”Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anapenda kuleta mbele yenu salamu za pole kwa Bunge la Jamhuri la Muungano na watumishi wote wa Wizara ya Katiba na Sheria.”

“Upande wa Serikali, tumepata pigo kubwa kwa kuondokewa na waziri mwenye uzoefu wa kimataifa. Rais Magufuli alimchagua kama waziri wa mambo ya nje na baadaye kumchagua kuwa waziri wa Katiba na Sheria,” amesema Samia

Amesema Balozi Mahiga ameiwakilisha vema nchi kimataifa kama mwanadiplomasia ambaye alikuwa mnyenyekevu na asiyejikweza.

Naye Naibu Spika, Dk Tulia Ackson akitoa salamu za Bunge kwa niaba ya Spika Job Ndugai amesema Balozi Mahiga alikuwa mnyenyekevu mtu mwenye akili na Bunge limepata msaada wake mkubwa.

“Bajeti yake imepita kirahisi sana kutokana na uweledi wake, ndugu yetu amepata fursa nyingi, salamu zimetoka sehemu nyingi duniani,” amesema Dk Tulia

“Nimepata habari mke wa marehemu yupo Nairobi anauguza mtoto, tunampa pole sana kwa wakti huu mgumu”, amesema Dk Tulia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ali Hapi amesema ukisoma wasifu wa Balozi Mahinga kuna mambo makubwa ya kujifunza.

“Kutokuwa mtu mwenye majivuno, usikivu wake na tukiwa kama vijana tumejifunza mengi,” amesema Hapi

Pia, kwenye shughuli hiyo ya maziko alikuwepo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Wasifu wake

Dk. Augustine Mahiga alizaliwa Agosti 28, 1945 huko Tosamanganga, Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa (Agosti mwaka huu angetimiza miaka 75).

Amesoma elimu ya msingi katika shule za Serikali enzi ya mkoloni na alihitimu darasa la VIII muda mfupi baada ya uhuru.

Safari ya elimu ya Dk Mahiga ilikuwa ya umaskini uliopitiliza, alishindwa kuendelea na elimu ya sekondari kwa kutokuwa na fedha za kulipia mashuka na mablanketi hadi aliposaidiwa na msamaria mwema kutoka Shirika la Kennedy wakati huo.

Aliendelea na masomo ya sekondari hapahapa nchini na mwaka 1968, alijiunga katika Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, Dar es Salaam na kuhitimu Shahada ya Sanaa akibobea kwenye elimu mwaka 1971.

Mwaka huohuo, Dk Mahiga alipata ufadhili na kuendelea na masomo ya juu nchini Canada katika Chuo Kikuu cha Toronto ambako alihitimu Shahada ya Uzamili. Aliendelea na masomo ya Shahada ya Uzamivu (PhD) katika chuo hichohicho akijikita katika Uhusiano wa Kimataifa na kuhitimu mwaka 1975.

Mwaka huohuo 1975 (akiwa na miaka 30), Dk Mahiga alirejea nchini akiwa daktari wa falsafa kitaaluma na alipangiwa kazi ya kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwa mhadhiri katika Idara ya Kimataifa na Ushirikiano wa Kikanda.

Alifanya kazi hiyo hadi mwaka 1977 alipohamishiwa katika Ofisi ya Rais kuwa Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo na alidumu hapo akifanya kazi pamoja na hayati Mwalimu Julius Kambarege Nyerere hadi mwaka 1980.

Kati ya mwaka 1980 hadi 1983, Dk Mahiga alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa. Nafasi hii aliitumikia kwa weledi mkubwa katika historia ya watu waliowahi kuitumikia, aliweza kuifahamu nchi vizuri na mifumo yake kwa mtizamo wa ndani na nje.

Mwaka 1989 hadi 1992, aliteuliwa kuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Kimataifa akifanyia kazi Geneva – Uswisi na mwaka 1992 hadi 1994, Balozi Mahiga aliteuliwa kuwa Kiongozi (Mwakilishi) wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) mjini Monrovia, Liberia na huu ndiyo wakati aliponusurika kuuawa na Majeshi ya Rais Charles Taylor, kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Kuna wakati akiwa katikati ya operesheni ya wakimbizi hapo Monrovia, Serikali ya Tanzania ilimteua kuwa Balozi na kumuongezea jukumu jingine zito.

Mwaka 1994–1998, Balozi Mahiga alihudumu akiwa Mratibu na Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni ya Dharura ya Ukanda wa Maziwa Makuu akifanyia kazi hiyo kutokea Geneva–Uswisi na kati ya mwaka 1998 – 2002 aliteuliwa kuwa Kiongozi Mkuu (Mwakilishi) wa Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR) huko mjini Delhi India kabla ya kuteuliwa tena kuwa mwakilishi wa shirika hilo katika nchi za Italia, Malta na Jamhuri ya San Marino kati ya mwaka 2002 – 2003.

Balozi Mahiga amepata pia kuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika kipindi cha mwaka 2003 hadi 2010 na alishiriki kikamilifu katika mipango ya kimataifa pamoja na kusimamia mazungumzo ya kuanzishwa kwa Kamisheni ya Ujenzi wa Amani (mwaka 2005).

Pia, kushiriki kwenye masuala ya maingiliano ya serikali mbalimbali na makundi yanayofanya kazi zisizo rasmi, maendeleo, amani, usalama na ujenzi wa ushirikiano wa uhakika kati ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Balozi Mahiga alirejesha heshima ya Tanzania hadi kuwa mojawapo ya nchi zilizounda Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi yetu ilipopata heshima hiyo, yeye aliteuliwa kuwa mkuu wa ujumbe wa Tanzania katika Baraza hilo, hii ilikuwa ni mwaka 2005.
Katika ulingo wa siasa, mwaka 2015 Balozi Mahiga alikuwa miongoni mwa wana CCM 42 waliojitokeza kuwania urais. Hata hivyo, hakupata fursa hiyo na aliyeibuka mshindi alikuwa Dk. John Magufuli.

Baada ya Dk. Magufuli kuibuka mshindi, alipounda baraza lake la mawaziri, alimteua Balozi Mahiga kuwa mbunge kisha akamteua kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.
Balozi Mahiga alihudumu nafasi hiyo hadi tarehe 3 Machi 2019 alipomhamishiwa wizara ya katiba na sheria na nafasi yake kuchukuliwa na Profesa Palamagamba Kabudi.
Awali, Parofesa Kabudi alikuwa waziri wa katiba na sheria.

error: Content is protected !!