MWILI wa Katibu Mkuu Kiongozi nchini Tanzania, Balozi John Kijazi, umeagwa leo Alhamis tarehe 18 Februari 2021, katika Hospitali ya Benjami Mkapa, jijini Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Balozi Kijazi, aliyekuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, alifariki dunia jana Jumatano saa 3:10 usiku kwenye hospitali hiyo alipokuwa akitibiwa.
Baada ya shughuli ya kuaga iliyoongozwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, mwili wa Balozi Kijazi utasafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam, ambapo utaagwa kesho Alhamisi tarehe 19 Februari 2021 katika viwanja vya Karemjee ambapo Rais John Magufuli ataongoza waombolezaji.
Akizungumza katika shughuli hiyo, Katibu Mkuu-Ikulu, Moses Kisiluka amesema “tukimaliza hapa, tutaelekea Dar es Salaam ambapo mwili wake utaagwa katika viwanja vya Karemjee na Rais Magufuli ataongoza shughuli hiyo.
“Baada ya kumaliza, tutaelekea nyumbani kwao Korogwe jijini Tanga kwa maziko yatakayofanyika Jumamosi,” amesema Kisiluka.

Awali, Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Faustine Bee alisema, wamepokea msiba huo kwa masikitiko makubwa kwa kuwa Balozi Kijazi, aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mkuu wa chuo hicho, tarehe 21 Agosti 2020 na alisimikwa 17 Desemba 2020.
Balozi Kijazi aliteuliwa kushika wadhifa huo baada ya aliyekuwa mkuu wa chuo hicho, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kufariki dunia tarehe 23 Julai 2020, jijini Dar es Salaam.
Profesa Bee amesema, Balozi Kijazi alishiriki mahafali yake ya kwanza na ya 11 ya chuo hicho yaliyofanyika tarehe 17 Desemba 2020, ambapo kulifanyika shughuli mbalimbali ikiwemo kusimikwa kwake, Kijazi na kumtunuku Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa ya Siasa “mkuu wa chuo chetu, Hayati Benjamin Mkapa.”
“Katika muda mfupi tuliokaa na kiongezi wetu, tumejifunza mengi, alikuwa mshauri anayesikiliza na anayeelekeza. Tulitamani kuendelea kuwa naye ili kutupeleka mbele zaidi.
“Balozi Kijazi alitamani kuona Chuo Kikuu cha Dodoma kinakuwa kipya, haki na wajibu bila ubaghuzi wowote unatawala. Alipenda kuona Watanzania wanakimbilia chuo hiki kusoma na kufanya kazi,” amesema.

Balozi Kijazi amekuwa Katibu Mkuu Kiongozi kuanzia tarehe 7 Machi 2016, baada ya kuteuliwa na kuapishwa na Rais Magufuli akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Ombeni Sefue.
Balozi Kijazi amewahi kuwa mwakilishi wa Tanzania nchini India, Singapore, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal mwenye makazi yake jijini New Delhi, India kuanzia mwaka 2007 – 2016 na hivyo kumfanya kuwa Mkuu wa Mabalozi wote wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi.
Kabla ya kuwa balozi, Balozi Kijazi alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na baadaye Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu kuanzia mwaka 2002 hadi 2006, baada ya kuteuliwa kuwa Balozi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na hatimaye kupangiwa kituo cha New Delhi, India.
Kati ya mwaka 1996 hadi 2002, Balozi Kijazi alikuwa Mhandisi Mwandamiziwa Ujenzi wa Barabara ndani ya Wizara ya Ujenzi kabla ya kupandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Barabara za Mikoa ndani ya wizara hiyo hiyo.
Alipata Shahada ya Sayansi ya Uhandisi wa Umma mwaka 1982 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, na baadaye Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Barabara Kuu kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingerezamwaka 1992.
Balozi ameacha mjane mmoja, Fransisca Kijazi ambaye walijaaliwa kupata wato9to watatu wote wa kiume ambao ni David, Emmanuel, Richard
Leave a comment