August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Balozi Idd ni mpotoshaji – Awadh

Spread the love

SIKU moja baada ya Balozi Seif Ali Idd, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, kusema kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iko palepale, Awadh Ali Said, Wakili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, amesema kiongozi huyo ni mpotoshaji,anaandika Regina Mkonde.

Balozi Idd juzi amenukuliwa gazeti moja la kila siku akisema, “naamini kuwa Rais (Ali Mohamed) Shein atatumia hekima na busara kuchagua viongozi wa vyama vingine vya upinzani kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) baada ya chama cha CUF kususia uchaguzi.”

Akizungumza na MwanahalisiOnline, Awadh amesema kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 na kuingizwa kipengele cha muundo wa SUK, hakuna hoja itakayohalalisha muundo wa SUK.

“Kwa mujibu wa Katiba na kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi hakuna utata kwa nafasi ya urais na nafasi ya makamu wa pili. Mtihani upo katika kumpata huyu makamo wa kwanza. Kwa vipi?” anahoji Awadh.

Anasema serikali ya Rais Shein haitafanikiwa kuenzi SUK kwa sababu hata kama atatumia nafasi 10 za kuteua wawakilishi kutoka upinzani, bado katiba inambana kwa kuwa inasema kabla ya kuteua wajumbe wawili kati ya hao 10, lazima rais ashauriane na kiongozi wa upinzani. Kwa sasa hakuna kiongozi wa upinzani katika Baraza la Wawakilishi.

Anasema: “Rais akiteua wapinzani, hawatakuwa na ridhaa kutoka viongozi wa upinzani. Katiba inasema wapinzani watakaoteuliwa  lazima wawe wamepata baraka ya wapinzani jambo litakalo shindikana sababu hakuna kambi ya upinzani.

“Katika hali hiyo Katiba imeelekeza kuwa nafasi hiyo iende kwa chama kilichoshika nafasi ya pili kwa wingi wa viti vya uwakilishi majimboni. Hadi sasa hakipo, maana viti vyote 54 vimechukuliwa na CCM.

“Vilevile hakutakuwa na mgawo wa wizara maana, mbali na CCM, hakuna vyama vilivyopata viti vya uwakilishi majimboni.”

Kwa mujibu wa wakili huyo, wizara za SUK hupatikana kwa mfumo maalumu ambao hutokana na idadi ya majimbo yanayowakilishwa na chama tawala na vyama vya upinzani. Kwa sasa hakuna chama cha upinzani kwenye Baraza la Wawakilishi.

“Wizara za SUK hupatikana kulingana na wingi wa viti vya majimbo. Mfano kama upinzani wana majimbo 20 ambayo yana asilimia 35, nafasi katika wizara watapata asilimia 35. Huo ndio muundo wa wizara za SUK,” amesema.

Awadh amedai kuwa wizara hupatikana kwa mujibu wa matakwa ya wananchi ambao wanachagua wawakili wa majimbo, na kwamba matakwa ya wananchi ya kuchagua wizara wanazotaka yalipuuzwa baada ya Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, kufuta kwa hila uchaguzi wa Oktoba 25, 2015.

Katiba inaelekeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa ni ya muundo wa Umoja wa Kitaifa. Ibara ya 9 (3) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 inaweka wazi hili:

“Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakuwa wa Umoja wa Kitaifa, na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja nchini na lengo la kufikia demokrasia” anasema.

Changamoto kubwa iliyopo sasa ni kwamba Katiba haikutoa jibu la nini kifanyike inapotokezea hali kama iliyopo wakati huu.

Waandishi wa katiba waliongozwa na uzoefu wao wa kawaida wa mwenendo wa siasa za Zanzibar. Hawakutarajia haya yaliyojitokeza, na ndiyo maana hawakuweka vifungu vya akiba.

error: Content is protected !!