July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Balozi Amina Salum atia mguu, Makongoro achukua fomu

Balozi Amina Salum Ally

Spread the love

MWANASIASA mashuhuri Visiwani Zanzibar, Balozi Amina Salum Ally, ameandika historia ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuchukua fomu ya kuomba uteuzi wa kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, huku akiainisha vipaumbele vyake 11. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Wakati Balozi Amina akifungua milango ya uthubutu kwa wanawake, mtoto wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere aitwaye Makongoro Nyerere naye ametinga mkoani Dodoma alasiri ya leo na kukabidhiwa fomu katika Makao Makuu ya CCM.

Ikumbukwe kwamba, Balozi Amina ambaye amewahi kushika nyadhifa kadhaa za uwaziri visiwani ikiwemo wizara nyeti ya fedha, pia amewahi kujitokeza kuchukua fomu ya kuomba uteuzi wa CCM kuwania urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kuleta mchuano mkali.

Akizungumza na waandishi baada ya kukabidhiwa fomu yake, Balozi Amina amesema kipaumbele chake cha kwanza ni kuwa na chombo maalum cha kusimamia masuala ya uchumi na maendeleo ambacho kitakuwa na jukumu la kutoa ushauri wa haraka kuhusu maeneo na aina ya uwekezaji unaohitajika.

Amesema chombo hicho kitasaidia kuondosha ucheleweshwaji wa maamuzi ya uwekezaji, kuondoa mikataba mibovu na ya hasara isiyo na tija kwa taifa.

“Kipaumbele kitawekwa kwa sekta zitakazochangia haraka moja kwa moja kupunguza umasikini, kwa mfano, kilimo na viwanda, serikali itabuni njia bora za kukuza uhusiano kati ya uwekezaji na ukuaji wa viwanda na kilimo kuanzia wakulima na wajasiriamali wadogo wadogo hadi wakulima na viwanda vikubwa,”amesema.

Amezitaja njia kuu za usafirishaji kuwa itakuwa ni njia pekee ya kukuza uchumi ambazo ni pamoja na reli, barabara, na usafiri wa baharini sambamba na maziwa huku akiahidi kufufuliwa au kujengwa upya ili ziweze kuchangia haraka kukua kwa uchumi.

Amefafanua kuwa Tanzania ina idadi kubwa ya wanawake ambapo takwimu zinaonesha idadi ya wanawake wote  ni takriban milioni 25 zaidi ya nusu ya watanzania wote ambao wanahitaji kutambuliwa na kupewa fursa sawa kwa kushirikishwa kikamilifu katika upangaji wa matumizi ya rasilimali za kitaifa.

Kwa imani ya Balozi Amina, hilo linawezekana ikiwa wanawake watashirikishwa au kuwezeshwa kushiriki katika mipango yote ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa hasa katika maeneo ya kutoa maamuzi yaayogusa jamii.

Amesema serikali yake itapigania kuondoa kasoro za mfumo dume ambao bado unachangia kudumaza huduma za msingi kwa wanawake huku akitolea mfano pamoja na elimu ili kuweze kupatikana maendeleo ya haraka.

“Mimi ninaamini, kwa wingi wao, mkakati wa kumuendeleza na kuwainua kimaendeleo wanawake wa kitanzania utakuwa ni njia nzuri pia ya kuwainua watanzania kutoka katika ufukara wa kipato na kielimu pia,”amesema.

Kipaumbele chake cha pili ni utoaji wa huduma za jamii kwa usawa kwa wote ikiwa takribani miaka 50 nchi imegubikwa na tatizo la huduma duni kwa jamii huku akitolea mfano wa afya na kinga za mama na mwana ili kupunguza vifo.

Pato la Taifa

Kuhusu mgawo bora wa pato la taifa, amesema kwa takribani miaka kumi iliyopita pato la nchi limekuwa likikua kwa kiwango kinachoridhisha huku ukuaji wake haujaambatana na kuwaletea maisha bora watanzania walio wengi. 

“Kwangu tofauti hiyo kubwa ya kipato katika jamii ni hatari kwa mustakbali wa umoja wa kitaifa na amani na utulivu wa kuletea nchi yetu maendeleo. KUa kuna kila sababu ya kimsingi inayohitaji utekelezaji wa haraka wa kuwepo mgawo bora wa pato la taifa,” amesema.

Elimu

Balozi Amina amesema kuporomoka kwa ubora wa elimu katika ngazi zote ni changamoto kubwa katika nchi ikiwa ni pamoja na wahitimu kukosa uwezo au elimu ya kutosha kupata au kujiajiri wenyewe ili waweze kujikimu kimaisha.

Ameahidi kuhakikisha elimu wanayopata vijana inawawezesha katika kukabili kikamilifu ushindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Utawala wa Sheria

Balozi Amina ameahidi kuweka mazingira bora ya kisheria katika kuwezesha uwekezaji katika uzalishaji mali na kuendesha biashara na miradi mikubwa nchini.

Amesema ili kukuza haraka ukuaji uchumi na kushinda vita dhidi ya umaskini ni vyema kukubali kuwa mchango wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi wa nchi  unahitaji kusimamiwa vyema kwa wawekezaji wa nje kuwekewa mazingira mazuri. 

Ukusanyaji kodi

Ameainisha kuwa takwimu za kitaifa zinaonyesha bayana kushuka kwa ukusanyaji wa kodi nchini mwaka hadi mwaka tangu mwishoni mwa miaka ya 1990s.

Kwa mujibu wa Balozi Amina, mapungufu ambayo yamekuwa yakijitokeza katika ukusanyaji huo yamekuwa yakileta adha nyingi kwa serikali na hata kwa watanzania huku akitolea mfano kushuku au kukosekana kwa huduma muhimu za kijamii. 

Rushwa

Amesema rushwa, ufisadi, uwajibikaji usioridhisha na ukosefu wa maadili ni mambo ya msingi ya kushughulikia kwa taifa linalofuata sera ya uwazi na utawala bora na maadili mema.

Kwamba, Tanzania imeingia doa kutokana na kugubikwa na vitendo vya ufisadi, rushwa na mapungufu makubwa ya ukosefu wa uadilifu na uwajibikaji serikalini takriban katika ngazi zote.

“Mimi naamini, serikali ni lazima iwe inawahudumia wananchi wake wote kwa kusimamia upatikanaji wa huduma bila ya ufisadi na vitendo vya rushwa kwa kufanya hivyo, wananchi watakuwa na imani na serikali yao,”amesema.

Muungano 

Balozi Amina ametamba kuwa, akipewa ridhaa ataendeleza mchakato wa kupata Katiba mpya ambao ulisimamiwa na serikali ya awamu ya nne na kwamba yeye ni muumini wa uhakika wa utawala.

Amesema kuwa Katiba bora itavusha taifa kwenda katika hali ya juu ya maendeleo na amani na utulivu.

Lugha

Pia amegusia lugha ya Taifa akisema Kiswahili kwa ajili ya mawasiliano ya aina mbalimbali ni moja ya tunu na nguzo zinazoliweka taifa kuwa kwenye umoja upendo na mshikamano ambao ndio ulioupatia amani na usalama.

Ameseme kutokana na hali hiyo, Kiswahili kinatakiwa kiendelezwe kudumishwa kama lugha ya Taifa na kwamba kutokana na kuongezeka kwa mashirikiano ya kibiashara, kisiasa na kitamaduni kati ya Tanzania na nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, inabidi kitumike na kisimamiwe katika ufundishaji nyenzo ya kuwapatia vijana ajira.

Makongoro Nyerere achukua fomu 

Mwanasiasa huyo, ambaye ameingia kwenye kinyang’anyiro kwa tambo za kutaka kuwabana aliowaita “vibaka” ndani ya CCM, ametinga kuchukua fomu akiongozana na Mzee Chifupa na kisha kuelezea ratiba ya kukusanya wadhamini akianzia Singida na Tabora. 

Amesema kuwa, atazunguka na usafiri wa gari ambalo alikopa kwenye ubunge wa Afrika Mashariki na kwamba yeye hana uwezo wa kifedha kama wengine huku akitamba kuwa hata waliofika Butiama kumsikiliza walijigharamia.

Kwa mujibu wa Makongoro, serikali ya CCM ina watu maarufu sana ambao pia ni maarufu kwa kutoa na kupokea rushwa na kusababisha kushusha heshima ya chama pamoja na kukigawa katika makundi ya ukabila na udini. 

Kuhusu ilani ya chama, amesema kuna wengi waliosema akiingia madarakani ataweka uchumi wa kati, wakulima wataacha jembe la mkono, jambo alidai huo ni uongo kwa vile wagombea sio wanaotengeneza ilani ya chama.

Ratiba ya kesho

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CCM Makao Makuu, kesho saa 4:00 hadi 5:30 asubuhi, atakayekuwa wa kwanza kuchukua fomu ni Amos Siyatemi. Kati ya saa 5:30 hadi 7:00, atachukua Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye.

Baadaye kuanzia saa 7:00 hadi 8:30 mchana, itakuwa zamu ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk.Mohamed Gharib Bilali, akifuatiwa na Balozi Ally Karume kati ya 8:30 hadi 10:00 alasiri.

Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa zamu yake itakuwa kuanzia saa 10:30 hadi 11:30 alasiri huku Dk. John Magufuli akifunga dimba kwa siku hiyo kati ya 11:30 hadi 12:30 jioni.

error: Content is protected !!