Sunday , 2 April 2023
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Balozi Amina hamaanishi akisemacho au hasemi akimaanishacho
Makala & Uchambuzi

Balozi Amina hamaanishi akisemacho au hasemi akimaanishacho

Balozi Amina Salum Ali. Picha ndogo mmea wa karafuu
Spread the love

MWANZONI mwa wiki hii, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko kwenye serikali ya Dk. Ali Mohamed Shein, Balozi Amina Salum Ali, aliliambia Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kuwa sababu kubwa ya wanawake wengi kubakwa wakiwa wanaokota karafuu ni kujipamba wakati wakienda mashambani, anaandika Mohammed Ghassani.

Maelezo haya yalitokana na swali aliloulizwa na mwakilishi aliyetaka kujuwa ni kwa nini serikali ilipiga marufuku uokotaji wa ‘mpeta’. Panapohusika zao la karafuu, mpeta hubeba maana mbili:

Moja ni karafuu zinazopukutika kutokana na ama upepo au maradhi au zinazoanguka – katika njia ya kumponyoka mchumaji – wakati wa uchumaji.

Maana ya pili, ni karafuu kavu ambazo katika kukauka kwake zilipatwa na matatizo ya kuingiwa na maji au kukosa mwangaza wa kutosha wa jua na hivyo zikawa na daraja ya chini ya thamani zinapofikishwa sokoni.

Huu mpeta wa pili, kwa hakika, hata huwa hauokotwi mashambani, bali kwenye maeneo ya kuuzia na kuanikia karafuu, au hata njia za maji ikitokezea karafuu zilisombwa na maji wakati zilipokuwa zimeanikwa.

Kwa wale waliozaliwa na kukulia kwenye mashamba ya karafuu, mimi nikiwa miongoni mwao, wanafahamu kuwa mpeta ni chanzo kimoja cha mapato kwa wale wananchi wasioweza kupanda mikarafuu mikubwa kwa ajili ya kuchuma. Ndani ya kundi hili, wamo akinamama, watoto na hata wazee.

Hii haimaanishi kuwa wanawake si wachumaji wa karafuu kwa ujumla wake. Hapana. Nimekulia kijijini ambako binafsi nikiwa barobaro wa miaka 14 mpaka 18, nilikuwa nikichuana na dada zangu kwenye uchumaji karafuu. Mara nyingi wakinishinda kwa kupata pishi nyingi. Walikuwa wa mwanzo kujaza pakacha au mapolo yao kila siku.

Ni kwa wale wenye dharura ya kutojiweza tu na ambao huwa wanataka kujipatia pato wakati wa msimu wa karafuu, ndio ambao huokota mpeta.

Turudi kwenye uokotaji wa mpeta na ubakwaji wa wanawake mikarafuuni. Tena hasa kwa kutumia sababu ya kuwa wanawake hao huwa wanakwenda mashambani mwa mikarafuu wakiwa wamejipamba na hivyo kuwapa wanaume vishawishi, ambao nao (hao wanaume) huamua kuwabaka.

Kutokana na malalamiko mengi ambayo Balozi Amina anasema ameyapokea kutoka kwa wananchi, serikali ikaonelea bora kupiga marufuku njia hii ya kujipatia riziki akinamama, watoto na watu wazima wasiojiweza. Yapasa kukiri kwa kila mwenye huruma kuwa njia hii ni ya halali wala haiipunji serikali kwa vyovyote vile.

Hakuishia hapo, kwa kuwa hilo la kupiga marufuku ni la serikali, basi akaonya kuwa adhabu kali itawashukia wale watakaolikaidi agizo lenyewe – la kutookota mpeta.

Ndani ya majibu haya ya Balozi Amina, muna upotoshwaji mkubwa ambao kamwe haukupaswa kufanywa na mtu anayetambuliwa na hadhi yake; tena ndani ya chombo kikubwa kama Baraza la Wawakilishi. Nitafafanua.

Kwanza, kufika mahala mwanamke anakwenda kuokota mpeta ni kwa kuwa ana dhiki kubwa ya maisha na hana uwezo wa kupanda mikarafuu akachuma. Uokotaji mpeta ni fursa adhimu ya watu wa namna hii. Imezoeleka hivyo maisha yote ya uchumaji wa karafuu.

Sasa mwananchi wa aina hii, alipaswa kulindwa na kushajiishwa na serikali iliyochukuwa dhamana ya kulinda maisha ya watu wake, na sio kuzuiwa kujipatia riziki yake ati kwa kuwa huko kuna mijanadume ina uchu.

Pili, licha ya kwamba sheria za nchi hazimzuwii mwanamke wala mwanamme kujipamba wakati aendapo kwenye shughuli ya kutafuta riziki, wanawake wetu wa mashamba si watu wa kujipodoapodoa kama walivyo wanawake wa mijini. Na hili Balozi Amina hakika hakuliona.

Wanawake wa mijini huenda maofisini wakiwa wamejikwatua kupita kiasi, pengine hata kuliko wakiwa majumbani mwao na waume zao. Je, kila wakati wanabakwa?

Kwa kauli hii, ni kwamba Balozi Amina anathibitisha kuwa maofisini, yakiwemo maofisi ya serikali aliyomo yeye, kuna ubakwaji wa hali ya juu, maana nako pia mijanadume iko tele.

Na, kwa hivyo, marufuku ya kutafuta riziki halali maofisini ingetolewa pia kwa wanawake wa Kizanzibari, maana kulivyo na taarifa za wanawake wanaobakwa mikarafuuni, kuna taarifa za wake wanaochukuliwa na waume za watu ni nyingi.

Tatu, ubakaji visiwani Zanzibar ni tatizo kubwa kuliko linavyoonekana kwa juu. Kuna visa vingi vya watoto wadogo wa kike na kiume kudhalilishwa kijinsia majumbani, mitaani na kwenye maeneo ya kupatia taaluma kama skuli na madrasa.

Vitoto hivi havijui hata kuushika wanja wa kujipaka machoni mwao, na bado mijanadume huvitamani na kumalizia uchu wao. Na nyingi ya kesi hizi humalizika kimyakimya ndani ya majalada ya ofisi za serikali hiihii inayopiga marufuku mpeta. Kwa hivyo, ubakaji hauchochewi na kujipamba wala si kwa wanawake watu wazima pekee.

Naona Balozi Amina hasemi anachokimaanisha au hamaanishi anachokisema. Chochote kati ya mawili hayo kinaiweka kauli yake kuwa alama kuu ya upotoshaji katika suala tete linaloila sasa jamii ya Zanzibar – yaani ubakaji na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto.

Kuna ukweli mmoja, ninavyouona, ambao serikali ya Dk. Shein haitaki kuusema. Imebanwa sana na haina nguvu za kiuchumi za kujiendesha. Inapambana kila njia kujikusanyia mapato. Inatumia njia yoyote iwayo. Hapa pana suala la soko la karafuu.

Kabla ya kupiga marufuku mpeta, serikali ya Dk. Shein ilijiingiza katika biashara ya mchanga wa kujengea nyumba. Imedhibiti kazi ya uchimbaji wa mchanga, iliyokuwa ikifanywa na wananchi kupitia maeneo yanayomilikiwa na wenyewe wananchi. Lawama zilitoka kila upande kuhusu hilo.

Kwa wasiojuwa ni kuwa kwa babati mbaya, tafauti na ilivyo kwa mazao mengine ya biashara ndani na nje ya Zanzibar, soko pekee la karafuu ni serikali. Hata nazi, ambalo ni zao la pili kwa ukubwa kibiashara visiwani Zanzibar, huuzwa na kununuliwa na wananchi wa kawaida.

Hata viungo vyote – hiliki, mdalasini, tangawizi na kila ukijuwacho – ni biashara ya watu binafsi. Hata utalii – njia nyengine inayoingiza fedha nyingi za kigeni Zanzibar – imebinafsishwa. Karafuu peke yake, ndiyo imehodhiwa na serikali.

Ingawa hili la ukiritimba wa soko la karafuu, nitakuja kulizungumzia tena siku nyengine, itoshe kutaja hapa kwamba ndio sababu ya marufuku hii ya mpeta, na wala sio kumlinda mwanamke anayekwenda mikarafuuni.

Mpeta huwa ni daraja ya mwisho kabisa ya karafuu na thamani yake ni ya chini. Kwa kuwa serikali ndiyo pekee mnunuzi na msafirishaji wa karafuu nje, kitisho cha mpeta kuingia kwa wingi kwenye mikono yake ni kikubwa. Unajuwa kwa sababu gani?

Karafuu ni zao kubwa la biashara Zanzibar, na linalimwa kwa wingi zaidi kisiwani Pemba, ambako zaidi ya asilimia 90 ya karafuu yote ya Zanzibar, hutoka. Pemba si eneo salama kisiasa kwa serikali ya Zanzibar kwa kuwa watu wake, kwa wingi wao, hawajawahi kuiunga mkono serikali hiyo wanayoamini si chaguo lao la halali. Wanaiona haipo madarakani kihalali.

Hivi karibuni, serikali hiyo ilipitisha uamuzi wa kuyachukuwa mashamba ya mikarafuu kutoka kwa wenyewe na kuyakodisha katika maeneo kadhaa. Licha ya serikali kusema imechukuwa hatua hiyo kisheria, inahofia uwezekano wa hujuma kutoka kwa wakulima wa karafuu kutoka kisiwa hicho.

Wapemba, wanaofahamika kwa utekelezaji visa wa kimyakimya dhidi ya serikali – kama ule uchaguzi wa Maruhani wa mwaka 2003 – wanahofiwa kuwa wanaweza kuzifanya karafuu zote zinazoingia mikononi mwa serikali kuwa mpeta. Kuifanya karafuu kuwa mpeta ni jambo rahisi sana. Ni kuinyima jua tu au kuiwacha ikapigwa na mvua.

Akiwa waziri wa biashara na masoko, Balozi Amina anajuwa hiyo inamaanisha nini kwenye biashara na soko la karafuu ya Zanzibar, hasa katika wakati huu ambapo mirija ya serikali kujikusanyia fedha za kigeni imenywea sana kutokana na mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na kufutwa uchaguzi halali wa Oktoba 2015 na kuitishwa mwengine kinyume cha sheria hapo Machi 2016.

Hiki ndicho nilichotangulia kusema hakisemwi kwenye marufuku hii ya mpeta. Vyenginevyo, akiwa mwanasiasa msomi aliyepanda daraja kadhaa hadi kufikia kuwa balozi wa Umoja wa Afrika katika Umoja wa Mataifa na, juu ya yote, mwanamke, hiki kingelikuwa kitu cha mwisho kabisa kustahiki kusemwa na kiongozi wa serikali inayojuwa dhamana iliyojibebesha kwa umma inaoutawala.
Ends.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Makala & Uchambuzi

Kondomu zinavyotumika kufukuza Tembo

Spread the loveMIKUMI ni miongoni mwa hifadhi za Taifa, inashika nafasi ya...

Makala & Uchambuzi

Ujio wa Kamala Harris: Fahamu uhusiano uliopo baina ya Tanzania na Marekani

Spread the love  TANZANIA ni miongoni mwa nchi tatu ambazo zimebahatika kutembelewa...

Makala & Uchambuzi

ZITTO: Hii ndio sababu Malaysia kuushinda umasikini kupitia kilimo, Tanzania ikikwama

Spread the love  MNAMO Februari 2017, miaka sita sasa imepita, niliandika, kupitia...

Makala & Uchambuzi

Ruth Zaipuna: Sekta ya kibenki imeimarika maradufu miaka miwili ya Dk. Samia

Spread the loveTarehe 19 ya mwezi Machi, ni siku muhimu sana kwa...

error: Content is protected !!