May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bakwata yazungumzia tahadhari ya corona

Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislam, Sheikh Khamisi Mataka

Spread the love

 

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), linaendelea kufanya tathimini za athari ya maambukizi ya corona (COVID-19), kisha itatoka na msimamo ya nini cha kufanya kwa waamini wake. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamesemwa Ijumaa tarehe 29 Januari 2021 na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka, alipozungumza na MwanaHALISI TV, iliyotaka kujua mikakati ya Baraza hilo kukabiliana na corona.

“Baraza msimamo wake ni kuwataka waumini wafuate maelekezo yote yanayotolewa na mamlaka husika kama wizara ya afya juu ya majanga yote yanayotukabili ikiwemo tishio la corona,” amesema Sheikh Mataka.

Amesema, wameipa jukumu tume ya huduma za jamii na kurugenzi ya huduma za afya za baraza hilo kwani “hawa ni wataalamu na tumewaachia wazifanyie kazi na tunasubiri taarifa za hao wataalamu ili watushauri nini cha kufanya.”

Wakati Bakwata wakieleza hayo, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limetoa waraka wa tahadhari juu ya maambukizi ya corona.

Barua hiyo, ulitolewa na Rais wa TEC, Askofu Gervas Nyaisonga kwenda kwa Mwadhama, Mpelekwa wa Baba Mtakatifu, Maaskofu Wakuu, Maaskofu na Maaskofu Wastaafu akiwataka kuchukua tahadhari ya maambukizi mapya ya corona.

Barua ya rais huyo wa TEC kwenda kwa viongozi hao, ilitumwa tarehe 26 Januari 2021 na kupewa kichwa cha maneno kisemacho, “tahadhari juu ya maambukizi mapya ya virusi vya Korona na ugonjwa wa Uviko 19 (COVID 19.”

Nyaisonga ni Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya.

Alisema, kuna wimbi jipya la maambukizo ya Korona kufuatia nchi kadhaa kuthibitisha kupita kwenye kipindi kigumu cha kuenea kwa virusi vya ugonjwa huo.

Alisema, “nchi yetu siyo kisiwa. Hatuna budi kuzingatia hekima ya wahenga wanasema, mwenzio akinyolewa wewe wewe tia maji. Ni muhimu tukaendelea kuzingatia kanuni za afya katika kukohoa au kupiga chafya na kuepuka kusogeleana, kugusana na kusongamana.”

Alisema, “hatuna budi kujihami, kuchukua tahadhari na kumlilia Mungu kwa nguvu zaidi, ili janga hili lisitukumbe.”

error: Content is protected !!