September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Bakwata yaunda tume kubaini ‘majipu’

Spread the love

BARAZA Kuu la Waislaimu nchini (BAKWATA),  limeunda tume  ya kuchunguza na kubainisha mali zilizopotea na mikataba isiyofaa ya baraza hilo, anaandika Faki Sosi.

Sheikh Abubakari Zuberi, Mufti Mkuu wa Bakwata, ameiunda tume hiyo, itakayokuwa na jumla ya watu nane.

Sheikh Issa Othman, Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, amewambia wanahabari kuwa, tume hiyo itaanza kazi ya kufuatilia mali zote za Bakwata zilizouzwa ili kubaini uhalali na mchalato wa kuuzwa kwake.

“Tume pia itapitia vyema mikataba yote iliyoingiwa baina ya Bakwata na taasisi zingine na kama kutakuwa na urasimu au ukiukwaji wa taratibu basi hatua stahiki zitachukuliwa ili kuzirejesha mali hizo au kuvunja mikataba husika,” amesema Sheikh Othman huku akiongeza;

“Tume itafanya kazi ndani ya siku 90 (miezi mitatu). Mikataba yote ya uuzwaji wa viwanja na nyumba za Bakwata itapitiwa, tunawataka waislamu nchini pamoja na wananchi wote kuipa ushirikiano tume kwa kutoa taarifa zitakazowezesha kubaini mali zote ambazo zimeuzwa ama kubadilishwa umiliki kinyemela.”

Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu juu ya matumizi mabaya ya mali za Bakwata na inategemewa kuwa tume hiyo itabaini mengi zaidi kuhusiana na mali hizo huku ikiwa tayari imetangaza kuchukua hatua kali za kisheria kwa wote watakaobainika kuhusika na ubadhirifu huo.

 

error: Content is protected !!