August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bakwata yapinga wafanyakazi kunyanyaswa

Spread the love

SELEMANI Lolila, Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), amesema kuwa dhuluma na manyanyaso kwa wafanyakazi wa Shule ya Sekondari ya Hijra na Shule ya Sekondari ya Jamhuri ikiwemo kusitishiwa mikataba yao bila kulipwa stahiki zao, hayakubaliki, anaandika Dany Tibason.

Watumishi watatu kati ya 13 wa shule hizo walizungumza na MwanaHALISI Online  wakieleza kuidai BAKWATA Mkoa wa Dodoma zaidi ya milioni 84 baada ya  kusitishwa mikataba yao bila kulipwa stahili zao.

Watumishi hao wamedai kuwa, wamekuwa wakinyanyaswa na Mashaka Kitundu, Kaimu Katibu wa Bakwata Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni meneja wa shule hizo, akiwaeleza kuwa haki zao zitalipwa zote kufikia mwezi Agosti, 2018.

Mussa Kunga, mmoja kati ya waliokuwa watumishi wa shule hizo amesema, anadai zaidi ya Sh. 4 milioni, ikiwemo malimbikizo ya mshahara, kiinua mgongo na Sadaka ambayo walitakiwa walipwe.

“Tunashangaa kuona wanatupangia namna ya kutulipa. Mikataba yetu ya ajira ilikuwa inaisha tarehe 30 Januari mwaka 2017, lakini barua ya kusitisha mikataba yetu imeeleza kuwa ifikapo tarehe 30 Agosti mwaka huu ajira zitakuwa zimesitishwa rasmi,” ameeleza na kuongeza;

“Pamoja na kusitisha mikataba yetu, Kitundu anajipangia muda wa kutulipa fedha zetu ambayo ni madeni ya malimbikizo tuliyotakiwa kuwa tumeshapata. Anasema watatulipa kuanzia Januari 2017 hadi Agosti  2018.”

Rehema Yegela, mtumishi mwingine wa shule hizo amesema, inashanagza kuona haki zao zilizotokana na utumishi wa hali na mali zinawekwa rehani kana kwamba wanaomba msaada.

Mtandao huu umeona barua ya kusitisha mkataba wa Rehema yenye Kumb. Na HSS/HMF/INF/01/2016, ya 27 Julai, 2016 ikisema, “Nasikitika kukuarifu kwamba taasisi imeamua kusitisha mkataba wako ambao ulikuwa unaishia 30 Januari 2017. Kuanzia 1/08/2016 hadi 30/8 2016 ajira yako itakuwa imesitishwa rasmi.”

Barua ambayo imesainiwa na M.S .Kitundu, Meneja wa Shule hiyo na nakala kupelekwa kwa Katibu Mkuu wa Bakwata Taifa.

Sheikh Lolila akizungumzia sakata hilo amesema, Mashaka Kitundu, meneja wa shule hizo ndiye anayepaswa kutoa majibu juu ya madai ya watumishi hao na kusema dini ya kiislamu hairuhusu dhuluma na Bakwata haitaruhusu uporaji wa haki za watu

“Hayo mambo yanayotuvunjia heshima, mimi ni Katibu wa Bakwata nchi nzima, siwezi kubariki watu wanyimwe fedha zao kwani ni haki yao, mtafute Mashaka Kitundu, meneja wa shule hizo akupe majibu ya kuridhisha. Kila mwenye haki lazima apewe,” amesema.

MwanaHALISI online ilipomtafuta Kitundu amejibu kuwa, “Mimi sihiitaji kuongea na wewe. Andika unachoweza, wewe gazeti lako halitendi haki hilo ni gazeti la kisiasa.”

 

error: Content is protected !!