Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari Bakwata wamkangaa Sheikh wa Dar es Salaam
HabariTangulizi

Bakwata wamkangaa Sheikh wa Dar es Salaam

Spread the love

 

BARAZA la Ulamaa, limefutilia mbali uamuzi wa “kuvunja ndoa,” uliyofanywa na sheikh wa BAKWATA mkoani Dar es Salaam, Alhadj Mussa Salum. Anaripoti Kelvin Mwaipungu…(endelea).

Taarifa ya baraza hilo, iliyotolewa leo Ijumaa, tarehe 27 Januari 2023, imeeleza kuwa hatua ya viongozi wa Bakwata jijini Dar es Salaam, kuingilia shauri la ndoa ya Juma Mwaka na mkewe Queenie Oscar, ni kinyume na misingi na maadili ya uislamu.

“Ndoa ya Bwana Juma Mwaka (Dk. Mwaka) na mkewe Bi. Queenie Oscar Masanja, haijavunjika na kwa kuwa kuna malalamiko yaliyopelekwa kwenye ofisi ya Qadhi, baraza linaelekeza kuwa shauri hilo ni sharti likasikilizwa,” imeeleza taarifa hiyo, iliyosainiwa na katibu wa baraza hilo, Sheikh Hassan Said Chizenga.

Ameongeza, “Baraza la Ulamaa, linapenda kuwafahamisha Waislamu popote waliko, pale wanapoona kuna upindishwaji wa mambo wasisite kufanya mawasiliano na baraza hili.”

Hatua ya Baraza la Ulamaa – chombo muhimu cha Waislamu katika kushughulikia masuala ya ndoa, talaka na mirathi – kujitosa katika sakata la ndoa ya Dk. Mwaka, imekuja siku mbili tangu “mganga huyo,” kulalamika kuvunjwa kwa ndoa yake, kinyume na taratibu za kiislamu.

Kwa mujibu wa Dk. Mwaka, ndoa kati yake na mkewe, imevunjwa kupitia mkutano na waandishi wa habari, uliyoitishwa na Sheikh Mussa, kinyume cha taratibu.

Akizungumza kwa hisia kali, Dk. Mwaka alisema, hata kama Sheikh Mussa alikuwa na mamlaka ya kuvunja ndoa yake, bado hakustahili kufanya hivyo.

“Kwanza, huyu mtu nimekuwa na mgogoro naye kwa muda mrefu, hivyo hana mamlaka ya kimaadili ya kusikiliza shauri langu. Lakini pia, hawezi kuvunja ndoa ya mtu, bila mhusika au wahusika kupewa haki ya kusikilizwa,” alieleza.

Aliongeza: “Kwa msingi huo, ndoa yangu haijavunjika. Ni kwa sababu, waliotangaza kuwa ndoa yangu imevunjika, ni wasela tu. Hawana mamlaka yoyote ya kisheria na kimaadili ya kufanya hivyo.

“Baraza la Ulamaa ni chombo huru. Hakipaswi kuingilia na kinachoitwa, ‘Baraza la Masheikh wa mkoa wa Dar es Salaam.’ Hii ni kwa kuwa mamlaka ya Qadhi, yako juu ya Sheikh wa mkoa na genge lake.”

Dk. Mwaka alifika mbali zaidi kwa kutuhumu wanaompigia chapuo ndoa yake kuvunjika, yawezekana kuwa na maslahi binafsi, ikiwamo kutaka kumchukua mwanamke huyo.

Maneno ya Dk. Mwaka yanaungwa mkono na kauli ya Baraza la Ulamaa, pale linaposema, “muhimili wa Mahakama ya Qadhi, ni mhimili muhimu na unaojitegemea. Si sahihi maamuzi yake, kuingiliwa na mamlaka za Bakwata wilaya au mkoa.

“Na pale suala litakaposhindikana katika Mahakama ya chini, suala hilo litapanda katika ngazi ya juu ndani ya mhimili huo na siyo vinginevyo.”

Aidha, Baraza la Ulamaa linasema, “utaratibu uliowekwa wa mgawanyo wa madaraka kuanzia ngazi zote, ni muhimu ukafuatwa na kudumishwa kwa ajili ya kuchunga dhana nzuri ya utawala bora ndani ya Baraza.”

MwanaHALISI Online, limeshindwa kumpata Sheikh Mussa, kutoa maoni yake kuhusiana na maekekezo ya Baraza la Ulamaa na hata kujibu madai ya Dk. Mwaka kuhusiana na jambo hilo.

Lakini alipotakiwa maoni yake Dk. Mwaka, haraka alisema, “nimepokea kwa moyo mkunjufu na nimefurahi sana.”

1 Comment

  • Je, huyo mke ni muislamu?
    Kama siyo muislamu, Mahakama ya Kadhi haipaswi kuisikiliza. Ipelekwe mahakama ya kawaida kitengo cha ndoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

Habari za SiasaTangulizi

CAG aibua madudu halmashauri 10, TANESCO na MSD

Spread the loveRIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali...

error: Content is protected !!