UONGOZI wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) Kata ya Chamwino mkoani Dodoma umefanya matembezi ya amani ya kuunga mkono kauli ya Muft Mkuu Sheikh Abubakari Zuberi ya kupinga na kulaani ndoa za jinsia moja. Anaripoti Danson Kaijage,Dodoma …(endelea).
Akizungumza na waumini wa dini hiyo katika msikiti wa Masjid Hudaa muda mfupi baada ya matembezi Sheikh wa Kata ya Makole na Mjumbe wa Baraza la Masheikh Bakwata Wilaya ya Dodoma, kwa niaba ya Sheikh wa Wilaya, Hasan Ngao amesema mapenzi ya jinsia moja ni kitendo cha kishetani na kila afanyaye vitendo hivyo hafai kuishi hata katika ardhi aliyozikwa pindi atakapokufa.

Ameeleza kuwa mapenzi ya jinsia moja au ndoa za jinsia moja si tu chukizo mbele za wanadamu, bali hata kwa maelekezo ya Mwenyezi Mungu ni chukizo kubwa.
Kiongozi huyo wa kiroho ameenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa iwapo masuala ya ushoga na usagaji yataendelea kushika kasi ni wazi hakutakuwepo na uzazi kwani mwanaume hawezi kupata mtoto iwapo atakuwa ameonana na mwanaume mwenzake au mwanamke hawezi kupata mimba iwapo atakuwa ameoana na mwanamke mwenzake.
“Mungu alituweka duniani na kutuambia anendeni mkaijaze dunia kwa ndoa ya mke na mume, sasa iwapo mume na mume au mke na mke wataoana uzazi au watoto watatoka wapi,” amehoji Sheikh Ngao.
Aidha, amesema ni laana kubwa kwa mtu yoyote anayefanya mapenzi kinyume na maumbile au kumaliza hamu zake kwa kutumia mkono (kujichua) kwani hukumu yake kwa Mungu ni kuhesabiwa mauaji kutokana na kile alichosema “mtu huyo amekuwa ameua mbegu ambazo zingetengeneza watoto.”
Naye Katibu wa Bakwata kata Chamwino Jijini Dodoma, Twaha Selemani amesema licha ya serikali na viongozi wa dini kupinga vitendo vya ushoga pia wazazi wanatakiwa kuwa karibu na watoto wao kwa ukaribu zaidi.
Amesema kwa sasa wazazi wamekuwa na hulka ya kuwapeleka watoto wao katika shule za bweni ambako kumekuwepo na matukio mabaya ambayo yanachangia kukuza masuala ya ushoga na kulawitiana.
Sambamba na hilo ameiomba serikali kuangalia utaratibu wa kubadilisha vipindi vya masomo kwa wanafunzi wa shule ya msingi kutokana na wanafunzi wengi kwa sasa kukosa muda wa kusoma masomo ya dini.
“Hivi sasa watoto wa shule ya msingi anasoma kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni hana hata muda wa kujifunza masomo ya dini jambo ambalo linasababisha watoto wengi kutokuwa na hofu ya Mungu.
“Matukio mengi ya ajabu au ufisadi unatokea kutokana na watu kutokuwa na hofu ya Ki-Mungu na kukosekana kwa hofu ya Mungu unatokana na tabia ya watu kutosoma na kujifunza kwa kina neno la Mungu” amesisitiza Katibu Twaha.
Leave a comment