July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bakwata Dodoma watangaza nafasi zinazogombaniwa

Spread the love

BARAZA Kuu la Waislamu (BAKWATA), Mkoa wa Dodoma limewataka waislamu kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika Baraza hilo. Anandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Ofisini kwake, Mjini hapa jana, Katibu wa Baraza hilo Mashaka Kitundu, amesema Baraza hilo limetoa fomu za kugombea nafasi mbalimbali.

Kitundu, alizitaja nafasi zinazogombaniwa kuwa ni Baraza la Masheikh Mkoa watu 5, Halmashauri Kuu Bakwata Mkoa nafasi 10 na Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa nafasi moja.

“Katika hii nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa tumetoa fomu kwa sababu nafasi imebaki wazi kutokana na aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo kufariki dunia,’’ amesema Kitundu.

Kitundu, amesema baada ya kupatikana wagombea hao, majina yao yatapelekwa kwenye Baraza Kuu la Ulamaa kwa ajili ya kufanyiwa usaili na baada ya usaili huo yatarejeshwa mkoani hapa kwa hatua nyingine.

Aidha, Kitundu amewataka waislamu kujitokeza kwa wingi katika kugombea nafasi hizo, kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia katika kujenga umoja ambao ni muhimu kwa Waislam.

Amesema hivyo kwa sababu Baraza hilo ni la Waislamu wote kinyume na baadhi ya waumini kufikiri kuwa ni la matabaka jambo ambalo siyo la kweli.

‘’Baraza ni la wote niwaombe waislamu tuwe na umoja, tupendane, tuheshimiane na kusaidiana kama  Quran inavyoagiza,’’ amesema.

Pia Kitundu amesema pamoja na changamoto iliyopo ya Sreikali kutangaza kuwa elimu ni bure wao wamejipanga kuhakikisha wanatoa elimu ya kuchangia yenye ubora.

Pia alitoa wito kwa wazazi kuwapeleka Wanafunzi katika shule zenye maadili ya kidini kwani kwa kufanya hivyo watazalisha viongozi wenye hofu ya mungu, ambao wataweza kusimamia haki.

Alisema katika shule yao ya Hijra wanataka kurudisha masomo ya ufundi ambayo hapo awali yalitolewa.

error: Content is protected !!