July 31, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Bajeti ya Rais Magufuli 2016/17 ‘kimeo’

Spread the love

BAJETI ya Seriali ya Awamu ya Tano kwa mwaka wa fedha 2016/17 chini ya Rais John Magufuli ni ngumu na haitekelezeki, anaandika Regina Mkonde.

Kauli hiyo ameitoa Prof. Ibrahimu Lipumba ambaye ni mtaalamu mbobezi katika masuala ya uchumi wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

“Pamoja na kauli mbiu ya bajeti ya mwaka 2016/2017 ya kuongeza uzalishaji wa viwandani ili kupanua fursa za ajira, hotuba ya bajeti haikueleza makadirio ya ajira mpya viwandani itakayotokana na utekelezaji wa bajeti hii,” amesema Prof. Lipumba.

Amefafanua kuwa, kuna baadhi ya mambo ambayo yatakwamisha ukuaji wa sekta ya viwanda ikiwemo ongezeko la riba katika mikopo ya kununulia malighafi, vipuli na mahitaji mengine ya viwanda.

“Riba ya mikopo iko juu karibia asilimia 20. Gharama hiyo ya mikopo ni kubwa mno na inapunguza faida ya wenye viwanda.

“Ni bora kuwa mchuuzi wa bidhaa toka nje ambazo zinaweza kuuzwa kwa haraka na kumuwezesha mfanyabiashara kulipa mkopo na kumudu gharama za riba,” amesema.

Kutokana na ukubwa wa riba amesema itakwamisha jitihada za serikali za kufufua sekta ya viwanda kwa lengo la kuleta ajira kwa wananchi na kuwaeezesha kuwa na uchumi wa pato la kati.

Kuhusu utekelezwaji wa bajeti hususani bajeti ya maendeleo amesema “nina wasiwasi bajeti ya maendeleo ya bilioni 11,820 haikutokana na uchambuzi wa hali halisi ya fedha na miradi inayoweza kutekelezwa.”

Amesema kuwa, hakuna mantiki ya watendaji serikalini kuchambua miradi na hali halisi ya matarajio ya mapato ya serikali na kujadiliwa katika Baraza la Mawaziri na kuwasilishwa bungeni halafu katika kipindi cha mwezi mmoja makadirio hayo yakaongezwa kwa asilimia 91

“Bila shaka bajeti ya amendeleo imeongezwa kwa shinikizo la rais. Mawaziri wanaohusika na bajeti wameogopa kutetea makadirio ya awali ya wataalamu wao, tofauti kubwa kati ya bajeti halisi na mwongozo wa bajeti utaathiri hadhi ya kitaalam ya waziri wa fedha katika duru za kimataiofa,” amesema.

Lipumba ameishauri serikali kuwa na mfumo wa kuandaa bajeti kulingana na ukubwa wa mapato badala ya kuandaa bajeti kabla ya kujua thamani ya mapato inayoweza mudu.

“Utaratibu mzuri wa bajeti ni kwanza kuelewa ukubwa wa keki uliyonayo, muhimu ilikuwa kuelewa na kujadili mapato yote ya serikali na vyanzo vyake na baada ya hapo ndiyo unaanza kuigawa keki hiyo kwenye kila sekta,” amesema na kuongeza.

“Utaratibu wa sasa ni wa kujadili mgawo wa keki kabla ya kukubaliana ukubwa wa keki yenyewe, huu siyo utaratibnu mzuri wa kupanga bajeti.”

“Changamoto kubwa ya bajeti ni ongezeko kubwa la makadirio ya ukusanyaji wa mapato.

“Mamlaka ya kodi imeongeza juhudi kubwa ya kukusanya kodi na kuziba mianya ya ukwepaji kodi.Pamoja na juhudi hizo mamlaka imefanikiwa kufidia malengo ya ukusanyaji kodi kama ilivyokadiriwa katika bajeti ya mwaka 2015/2016 na siyo kuvuka malengo hayo,”

Prof. Lipumba ameongeza kuwa “Ikumbukwe kuwa katika bajeti ya 2015/2016 makadirio ya mapato ya awali yalikuwa makubwa na kwamba kamati ya bunge ikafanmikiwa kuyapunguza kwa kuzingatia hali halisi ya ukusanyaji wa mapato.

Amesema juhudi kubwa iliyofanywa na mamlaka ya mapato katika awamu ya rais Magufuli imefanikisha kufikia lengo la makadirio yalioyopitishwa na bunge na siyo kuvuka lengo, na kwamba baadhi ya mapato yaliyokusanywa ni malimbikizo ya nyuma.

Anasema katika kikao cha bunge cha mwezi Februari mwaka huu waziri wa fedha na mipango aliwasilisha mwongozo wa mpango wa bajeti na ukajadiliwa pamoja na kupitishwa na bunge ambao ni tofauti na bajeti iliyotolewa ya mwaka 2016/2017.

Prof. Lipumba amesema sura ya bajeti ya 2016/2017 ni kubwa ukilinganisha na mwongozo uliotolewa februari 2016. Na kwamba imeongezeka kwa shilingi trilioni 6.55 sawa na asilimia 28.5.

Akinukuu maelezo ya waziri wa fedha Lipumba amesema “Waziri alieleza bunge kuwa sura ya bajeti ya mwaka 2016/2017 inaonesha kuwa jumla ya shilingi bilioni 22,991.5 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho

“Bajeti iliyowasilishwa bungeni ni tofauti kabisa na mwongozo wa mpango wa bajeti uliowasilishwa na kujadiliwa bungeni na kuungwa mkono na IMF matumizi yote ya serikali yatakuwa shilingi bilioni 29,539.6 badala ya shilingi bilkioni 22,991.5 hii ni ongezeko la shilingi bilioni 17,719.1 badala ya shilingi 6,182.2 na kufikia shilingi bilioni 11,820.5.

 

error: Content is protected !!