Tuesday , 16 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Bajeti kilimo 2021/22 yaongezeka, yaja na vipaumbele 7
Habari za Siasa

Bajeti kilimo 2021/22 yaongezeka, yaja na vipaumbele 7

Prof Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu
Spread the love

 

BAJETI ya Wizara ya Kilimo, kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022, imeongezeka kwa Sh. 64.3 bilioni (22%), kutoka Sh. 229.83 bilioni (2020/2021), hadi Sh. 294.16 bilioni. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa ya ongezeko hilo, imetolewa bungeni jijini Dodoma na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, kwenye mjadala wa bajeti ya wizara hiyo , uliofanyika siku mbili, tarehe 24 hadi 25 Mei, 2021.

“Uchambuzi wa Kamati umebaini kwamba, bajeti inayoombwa kuidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022, imeongezeka kwa Sh. 64,322,263,000, sawa na asilimia 22. Ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021, ambayo ilikuwa Sh. 229,839,808,000,” imesema taarifa ya kamati hiyo.

Kamati hiyo imesema, Wizara ya Kilimo imepanga kutumia Sh. 82.914 bilioni (28.2%), kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh. 211.24 bilioni (71.8%), kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

“Kwa upande wa matumizi ya kawaida katika mwaka wa fedha 2021/2022, kuna ongezeko la Sh. 6,148,587,000, sawa na asilimia 7.4. Ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2020/2021, ambapo matumizi ya kawaida yalikuwa Sh. 76,765,484,000,” imesema taarifa hiyo.

Bunge la Tanzania

Taarifa hiyo imesema “kamati imeendelea kubaini kwamba, kiasi cha fedha za maendeleo kinachoombwa kimeongezeka kwa Sh. 61,173,676,000, sawa na asilimia 29 ikilinganishwa na kiasi kilichoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2020/2021, ambacho kilikuwa Sh. 150,074,324,000.”

Kamati hiyo imesema ongezeko hilo linatarajiwa kwenda kuboresha, kukarabati na kujenga skimu za umwagiliaji, ili kuongeza tija kwenye kilimo kwa kupunguza utegemezi wa kilimo cha kutegemea mvua.

Sambamba na ongezeko hilo, wizara hiyo imeanisha vipaumbele saba ambavyo vitakwenda kutekelezwa, kwa ajili ya kuimarisha sekta hiyo.

Kipaumbele cha kwanza kilichoanishwa kwenye hotuba ya wizara hiyo, iliyowasilishwa bungeni jana tarehe 24 Mei 2021 na Waziri wa Kilimo, Prof. Adolph Mkenda, ni mkakati wa kuongeza tija katika mazao sambamba na kuweka mkazo kwenye tafiti.

Mahindi yakiwa shambani

Katika kufanikisha kipaumbele hicho, wizara hiyo imeongeza bajeti ya fedha katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), kutoka Sh. 7.35 bilioni (2020/2021), hadi Sh. 11.63 bilioini (2021/2022).

Kipaumbele cha pili ni kuongeza kiwango cha uzalishaji mbegu bora nchini, ikiwemo kuendeleza mashamba 13 ya mbegu, kwa kuweka miundombinu ya umwagiliaji kwa kutumia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji.

“Tumepanga kuongeza bajeti ya uzalishaji wa mbegu bora kutoka Sh. 5.42 bilioni, mwaka 2020/2021 hadi Sh. 10.58 bilioni mwaka 2021/2022 na kuendelea kushirikiana na sekta binafsi, katika kuzalisha mbegu bora nchini,” imesema taarifa ya wizara hiyo.

Kipaumbele cha tatu ni uimarishaji huduma za ugani, kwa kuongeza bajeti ya eneo hilo kutoka Sh. 603 milioni, mwaka 2020/2021 hadi Sh. 11.5 bilioni mwaka 2021/2022.

“Fedha hizo zitatumika katika kuimarisha huduma za ugani nchini, ikiwa pamoja na kununua pikipiki 1,500, vifaa vya kupima afya ya udongo, visanduku vya ufundi, simu janja na kuwezesha uanzishwaji wa mashamba ya mfano, kwa kila Afisa Ugani na kutoa mafunzo rejea,” imesema taarifa hiyo.

Shamba la mpunga
Shamba la mpunga

Uimarishwaji kilimo cha umwagiliaji, ni kipaumbele cha nne cha wizara hiyo, na kwamba imepanga kuongeza eneo la umwagiliaji kwa kuhamasisha wadau kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu, uvunaji wa maji na uchimbaji visima.

Kipaumbele cha tano ni, uimarishaji upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo, kwa kutekeleza kilimo cha mkataba kwenye mazao ya biashara.

Taarifa ya wizara hiyo imesema kipaumbele cha sita ni, uimarishwaji kilimo anga, ambapo imeongeza bajeti yake kutoka Sh. 150 milioni mwaka 2020/2021, hadi Sh. 3 bilioni mwaka 2021/2022, ikiwemo kununua ndege moja mpya kwa ajili ya kudhibiti wadudu wasumbufu.

Kipaumbele cha mwisho ni, uimarishaji mifumo ya upatikanaji mitaji, kwa kutanua wigo wa wakulima kupata mikopo yenye masharti nafuu.

“Katika mwaka 2021/2022, wizara itafanya tathmini ya mifumo ya upatikanaji wa mitaji, kwa wakulima wadogo na wawekezaji wengine kwenye sekta ya kilimo. Ili kuibua vizuizi na kuvitafutia majawabu kwa ajili ya kuimarisha ugharamiaji wa mazao katika mnyororo wa thamani,” imesema taarifa hiyo.

3 Comments

 • Sasa kila wakati mnasema mtaboresha lakn hakuna kitu mnafanya, ajiri maafisa kilimo kila kata na muape masharti na malengo ya kufika kila mwaka, sio siasa za uongo

 • Kweli bajeti iko poa lakini sijaona sehemu ya ajira za maafisa kilimo au hakuna mwaka huu?

 • Asanteni,

  Kwa kweli bajeti imeboreshwa zaidi ukilinganisha na bajeti ya mwaka wa fedha uliopita.

  Asanteni sana kwa maboresho hayo. Muhimu mambo hayo kwenye makaratasi tuyaone kwenye jamii zetu.

  Rafiki yako,

  Aliko Musa.

  Mwekezaji na mbobezi kwenye majengo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Samia arejesha mikopo ya 10%, bilioni 227.96 zatengwa

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amerejesha utaratibu wa utoaji mikopo...

Habari za Siasa

Rais Samia amfariji mjane wa Musa Abdulrahman

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan leo Jumanne amempa pole Mwanakheri Mussa...

Habari za Siasa

Nape: Wanasiasa, wanahabari, wafanyabiashara mteteeni Samia

Spread the loveWaziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,...

Habari za Siasa

CAG: TAWA imegawa vibali vya uwindaji bila idhini ya waziri

Spread the loveRIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali...

error: Content is protected !!