November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Bajeti 2022/23 ya Tanzania, watendaji wapewa maagizo 6

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa maagizo sita muhimu ambayo yanatakiwa kuzingatiwa kikamilifu na viongozi na watendaji wote wa Serikali wakati wa maandalizi na utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/2023. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Waziri Mkuu amewaagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama ashirikiane na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba kuhakikisha wanatatua changamoto ya upatikanaji wa mafao ya wastaafu kwa wakati.

Kuhusu udhibiti wa ongezeko la madeni ya Serikali, Majaliwa amewaagiza maafisa masuuli wote wahakikishe madai yote ya watoa huduma yanahakikiwa na kuingizwa kwenye hesabu za fungu husika.

Pia, mewaonya wasiingie mikataba ya miradi mipya bila kuwa na uhakika wa upatikanaji fedha; na kuwataka wazingatie matumizi ya hati za ununuzi zinazotolewa kwenye mfumo wa malipo ili kudhibiti ulimbikizaji wa madeni.

“…kudhibiti matumizi na kupunguza gharama. Maafisa masuuli endeleeni kuchukua hatua za kupunguza matumizi ya Serikali yasiyokuwa ya lazima na kuhakikisha kuwa taasisi za Serikali zinazojiendesha kibiashara, zinapata faida na kuacha kutegemea ruzuku kutoka Serikali Kuu,” amesema

Akizungumzia kuhusu ukusanyaji wa mapato ya ndani, Majaliwa amesema hilo ni miongoni mwa maeneo yaliyoibua hoja kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge.

“Hivyo, nisisitize kuwa Wizara ya Fedha ishirikiane na Ofisi ya Rais – Tamisemi kuimarisha matumizi ya vifaa vya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Serikali.”

Majaliwa amesema mbali na uwasilishwaji wa Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2022/2023 pia Bunge lilipokea, kujadili, kushauri na kupitisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.

Amesema Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2022/2023 ni wa kwanza kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambao utaendelea kutekelezwa katika maeneo mahsusi ya kipaumbele.

Majaliwa ameyataja maeneo hayo kuwa ni ya kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; kukuza biashara na uwekezaji; kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu.

error: Content is protected !!