July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bajeti 2021/22 yamuibua Zitto

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo

Spread the love

 

KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema hatua ya Serikali kufanya uhakiki wa madeni ya wastaafu katika mifuko ya hifadhi ya jamii, kwa ajili kulipa kupitia njia ya hati fungani, itaongeza ukwasi wa mifuko hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Zitto ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, tarehe 10 Juni 2021, saa chache baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, kuwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali katika mwaka wa fedha wa 2021/22, bungeni jijini Dodoma.

Mwanasiasa huyo amesema, hatua hiyo itamaliza malimbikizo ya madeni ya muda mrefu, yaliyotengenezwa katika Serikali ya Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Magufuli.

“Madeni ya Serikali kutoka mifuko ya hifadhi ya jamii, ambayo kwa Miaka 10 Serikali za Kikwete na Magufuli zilishindwa kuyatambua, sasa kutambuliwa na kulipwa kwa njia ya hati fungani. Huu ni ukombozi mkubwa kwa wastaafu kwani mifuko itakuwa na ukwasi mkubwa,” ameandika Zitto kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango

Awali, Dk. Mwigulu alisema changamoto ya mrundikano wa madeni, ilipunguza ufanisi wa mifuko hiyo na kwamba Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan, ameagiza wizara yake na Ofisi ya Waziri Mkuu, kukamilisha zoezi la kitalaamu la uhakiki, kujua hali halisi ya madeni, kwa ajili ya kubaini namna bora ya kuyalipa.

Ili kutatua changamoto hiyo, Dk. Mwigulu alisema kuanzia mwaka wa fedha ujao, Serikali itatenga fedha katika bajeti na kutumia utaratibu wa kutoa hati fungani maalum isiyo taslimu, zitakazoiva kwa nyakati tofauti kuanzia miaka miwili hadi 25.

“Utaratibu wa hatifungani una faida mbalimbali zikiwemo, kuipa Serikali nafasi ya kibajeti ya kuendelea kutekeleza miradi mingine ya maendeleo. Kuiwezesha Serikali kuyatambua madeni hayo kwenye kanzidata ya madeni na kuzuia madeni hayo kuendelea kuongezeka kulingana na tathmini ya thamani ya madai,” amesema Dk. Mwigulu na kuongeza.

“ Utaratibu huo utaboresha mizania ya hesabu na mtiririko wa mapato yanayotokana na riba ya hatifungani hizo kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Hatua hii inakwenda kumaliza kabisa tatizo hilo la wazee wetu kudai haki yao kwa damu na machozi yaliyodumu kwa muda mrefu.”

error: Content is protected !!