May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bajeti 2021/22: Mabadiliko makubwa Jeshi la Polisi

Simon Sirro, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP)

Spread the love

 

WAZIRI wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba amesema, kuanzia mwaka wa fedha 2021/22, askari wa Jeshi la Polisi wataingia mkataba wa kipindi cha miaka sita na kuingia katika ajira ya kudumu. Anaripoti Jemima Samwel, DMC…(endele)

Dk. Mwigulu amesema hayo, leo Alhamisi, tarehe 10 Juni 2021, wakati akiwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/22, bungeni jijini Dodoma.

Amesema, katika jeshi la polisi kwa askari wapiganaji, kuna utaratibu wa wapiganaji kufanya kazi kwa mikataba ya muda mfupi kwa miaka 12 kabla hawajapata ajira za kudumu.

Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango

Amesema, jambo hili huwasababishia wapatapo mkataba wa kudumu wawe wamechelewa kwa miaka 12 ikilinganishwa na mtumishi mwingine aliyeingia pamoja kazini katika idara nyingine.

“Jambo hili linamadhara hasi katika itifaki ya utumishi na mafao ya mpiganaji anapostaafu. Hiki kimekuwa kilio cha muda mrefu cha askari wa Jeshi la Polisi,” amesema

Waziri huyo amesema, kutokana na changamoto hiyo, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, “amesikia kilio cha askari hao na alituelekeza tukae na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kutafuta suluhisho la jambo hili.”

Dk. Mwigulu amesema, “napendekeza kuanzia mwaka 2021/22 askari wa Jeshi la Polisi wataingia mkataba wa kipindi cha miaka 6 na kuingia katika ajira ya kudumu.”

error: Content is protected !!