July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bajeti 2015/16 yauma, kupuliza

Wizara wa Fedha, Saada Mkuya akiwa na begi lenye bajeti ya Serikali ya mwaka 2015/16

Spread the love

BAJETI ya Serikali kwa mwaka 2015/16 ya Sh. 22.4 trilioni, imewasilishwa huku upande moja ikiuma na upande mwingine ikipuliza kwa mwananchi wa kawaida.Wanaandika waandishi wetu … (endelea).

Katika bajeti hiyo yenye ongezeko la Sh. 2.6 trilioni zaidi ya ile ya 2014/15 ya Sh. 19.8 trilioni, serikali imebuni vyanzo vipya vya mapato na kuachana na utegemezi wa kodi za vinywaji na vileo ambavyo vinawaumiza wananchi, lakini imeongeza ushuru katika mafuta ya taa, petrol na dizeli.

Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya ametumia saa mbili kuwasilisha bajeti hiyo na kusema “ni ya kipekee kwa sababu kadhaa. Kwanza ni Bajeti ya mwaka wa Uchaguzi Mkuu ambapo Serikali ya Awamu ya Nne inamaliza muda wake na Serikali mpya ya Awamu ya Tano inatarajiwa kuingia madarakani.”

“Kwa mantiki hiyo, hii ni Bajeti ya mwisho katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010. Pili, utekelezaji wa MKUKUTA II ulipangwa kufikia tamati Juni, 2015.”

Hata hivyo, serikali imeamua kuongeza muda wa kutekeleza MKUKUTA II hadi Juni 2016 ili utekelezaji wake ukamilike sawia na kumalizika kwa utekelezaji wa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Hata hivyo, katika hali ya kuonesha kuwa joto la uchaguzi bado linawavuruga wabunge na mawaziri, wakati wa uwasilishaji huo, idadi yao kubwa hawakuwemo ukumbini na hivyo viti vingi kuonekana wazi.

Vipaumbele

Mkuya amesema, bajeti hii ina vipaumbele vichache vifuatavyo. Kwanza, kugharamia shughuli za Uchaguzi Mkuu ikiwa ni pamoja na gharama zote za shughuli za Bunge lijalo, Mabaraza ya Madiwani na shughuli za Serikali awamu ya nne na kuanza kazi kwa Bunge líjalo.

Pili, kuweka msukumo katika kukamilisha miradi inayoendelea; na tatu, kuweka msukumo maalum kwenye miradi ya umeme na maji vijijini na kuimarisha rasilimali watu. Ili kutekeleza hayo, msisitizo mkubwa utawekwa kwenye kukusanya mapato ya ndani.

Malengo

Amesema kuwa, bajeti inalenga katika kukamilisha miradi iliyoanza kutekelezwa na Serikali na kulinda mafanikio yaliyokwishapatikana katika sekta ya Elimu, Afya, Maji na Maendeleo ya Jamii.

“Hivyo, hakutakuwa na miradi mipya isipokuwa ile tu ambayo majadiliano yake yamefikia katika hatua za mwisho. Miradi inayotegemewa kukamilishwa na imetengewa fedha ni pamoja na upanuzi wa uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Ujenzi wa mtambo wa kufua Umeme – Kinyerezi II na ujenzi wa Maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 Wilaya ya Mbozi na tani 10,000 Songea Mjini.

“Mingine ni ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi (Integrated Land Management Information System); kuimarisha na kuboresha vitendea kazi na huduma katika reli ya kati; ujenzi wa Bandari mpya ya Mbegani; Awamu ya tatu ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano; kuendelea na utekelezaji wa Mradi wa upanuaji wa mtambo wa maji wa Ruvu juu na Ruvu chini; kuandikisha wapiga kura na Vitambulisho vya Taifa,”ameema.

Mapato

Kuhusu mapato, Mkuya amesema mtazamo mpya wa mapato ya ndani, amegusia mageuzi kwenye suala la misamaha ya kodi akisema, jambo la kwanza linahusu mwelekeo wa mageuzi ya kodi.

“Kwa muda sasa Serikali imekuwa ikipunguza misamaha ya kodi inayotolewa kwa ridhaa ya Waziri wa Fedha kwa mujibu wa sheria. Badala ya kutoa misamaha kwa ridhaa, Serikali imechukua mwelekeo wa kupunguza au kuondoa kodi kwenye bidhaa zenye umuhimu wa kipekee, ili yeyote anayenunua bidhaa hizo awe na nafuu ya kodi moja kwa moja, bila kutegemea ridhaa ya waziri,”amesema.

Amesema kuwa, Sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ambayo itaanza kutumika tarehe mosi Julai, 2015 Serikali imeondoa kodi kwa bidhaa muhimu kama vile pembejeo, zana za kilimo, zana za uvuvi, vifaa tiba pamoja na bidhaa zote za mitaji.

Hivyo, mwananchi atakaponunua bidhaa hizo hatatozwa kodi. “Huu ndio mwelekeo wa mageuzi tunayoyafanya katika kupunguza  misamaha ya kodi inayotolewa kwa ridhaa (discretionary). Kauli mbiu ya mageuzi haya ni “punguza ridhaa ongeza bidhaa”, yaani kupunguza misamaha ya kodi inayotolewa kwa ridhaa na badala yake kupunguza kodi kwenye bidhaa zenye umuhimu maalum kwa wananchi.”

Ametaja hatua nyingine kuwa ni kupiga marufuku Serikali kutumia wazabuni ambao hawalipi kodi kikamilifu.

Mkuya amesema, Serikali, Wakala wa Serikali na Mamlaka za Serikali za Mitaa haitafanya biashara na mzabuni yeyote ambaye hatumii mashine za EFD.

“Ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi pia utaimarishwa kwa kuchukua hatua mbalimbali. Kwanza, ni lazima mfumo wa kieletroniki utumike katika utoaji wa risiti kwa tozo, faini, ada na malipo mengine yote ya Serikali kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Wakala wote wa Serikali,”amesema.

Katika kuongeza mapato hayo, Mkuya amesema Sheria ya Mafuta ya Petroli, SURA 392 89 kwa kupendekeza kuongeza Tozo ya Mafuta ya Petroli kwa viwango vifuatavyo;

“Mafuta ya dizeli kutoka Sh. 50 kwa lita hadi Sh.100 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh. 50 kwa lita, mafuta ya petroli kutoka Sh. 50 hadi Sh. 100 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh.50 kwa lita, mafuta ya taa kutoka Sh. 50 kwa lita hadi Sh.150 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh.100 kwa lita ili kuondoa uwezekano wa kuchakachua.

“Hatua ya kuongeza Tozo ya mafuta ya petroli inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh. milioni 139,786.8. Fedha hizi zote zitaelekezwa katika mfuko wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA)kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za usambazaji wa umeme vijijini,” amesema. 

Matumizi

Kwa mujibu wa Mkuya, katika kipindi cha 2015/16, Serikali imekadiria kutumia Sh. 22.4 trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo. Kiasi hiki kinajumuisha Sh. 16.5 trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh. 5.9 trilioni ni matumizi ya maendeleo.

Amesema mgawanyo wa fedha katika sekta ambao haujumuishi madeni ya kisekta yanayolipwa kupitia Mfuko Mkuu wa Serikali (CFS) ni kama ifuatavyo; Nishati na Madini Sh. 916.7 bilioni. Kati ya kiasi hicho, Sh. 447.1 bilioni zimetengwa kwa ajili ya mradi wa usambazaji wa umeme vijijini

Miundombinu imetengewa Sh. 2,428.8 bilioni, kati ya hizo Sh.322.4 bilioni zimetengwa kwa ajili ya miundombinu ya usafirishaji; Sh.1,608.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja;Sh. 9.5 bilioni kwa ajili ya kujenga na kuboresha bandari.

Mkuya amesema kilimo kimetengewa Sh. 1,001.4 bilioni kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji, ujenzi wa maghala na masoko katika maeneo mbalimbali nchini.

Elimu imetengewa Sh. 3,870.2 bilioni ili kugharamia ubora wa elimu na kuimarisha miundombinu ya elimu kati ya fedha hizo, Sh.348.3 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kutoa mikopo ya elimu ya juu.

“Maji yametengewa Sh.573.5 bilioni kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya maji mijini na vijijini huku sekta ya Afya ikipata Sh.1,821.1 bilioni kwa ajili ya kuboresha huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na ununuzi wa madawa, kuzuia magonjwa ya mlipuko, chanjo za watoto, ujenzi wa zahanati na kudhibiti Ukimwi na Malaria,” amesema.

Amefafanua kuwa katika mwaka 2015/16, mikoa na halmashauri zimetengewa Sh. 4,947.8 bilioni ikiwa ni nyongeza ya Sh. 448.8 bilioni ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2014/15. Aidha, halmashauri zinakadiriwa kukusanya mapato ya ndani ya Sh.521.8 bilioni.

Mkuya amesema “katika mwaka 2015/16, Sh. 36.5 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi pamoja na majengo ya makao makuu ya halmashauri mpya. Aidha, Sh. 27.2 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na nyumba za wakuu wa mikoa, wilaya pamoja na makatibu Tarafa katika maeneo hayo.”

Amesema serikali imepanga kukusanya Sh. 22.4 trilioni kutoka kwenye vyanzo vya ndani na nje. Mapato ya kodi na mapato yasiyo ya kodi yanatarajiwa kufikia Sh.13.4 trilioni sawa na asilimia 14.3 ya Pato la Taifa.

Aidha, mapato kutokana na vyanzo vya Mamlaka za Serikali za Mitaa yanatarajiwa kufikia Sh. 521.9 bilioni huku Washirika wa Maendeleo wameahidi kuchangia Sh. 2,322.5 bilioni kama misaada na mikopo nafuu.

“Kati ya fedha hizo, Sh. 660.3 bilioni ni mikopo nafuu ya kibajeti, Sh.1,463.2 bilioni ni misaada na mikopo nafuu kwa ajili ya miradi ya maendeleo na Sh.119  bilioni ni Mifuko ya Pamoja ya Kisekta.

“Ili kuziba nakisi ya bajeti, serikali inatarajia kukopa kutoka katika vyanzo vya ndani na nje Sh.6,175.5 bilioni. Kati ya fedha hizo, Sh. 2,600 bilioni ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za serikali zinazoiva; Sh. 1,433 bilioni ni mkopo wa ndani ambao unajumuisha Sh. 628.3 bilioni ni kwa ajili ya kulipia madeni yaliyohakikiwa,” amesema.

Ameongewa kuwa Sh. 804.7 bilioni ni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo; Sh.2,124.5 bilioni ni mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara ambayo itatumika kugharamia miradi ya maendeleo.

Serikali imekadiria kutumia Sh.22.4 trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, matumizi ya kawaida ni Sh. 16.5 trilioni ambayo yanajumuisha Sh. 6.4 trilioni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali, Wakala na Taasisi za Serikali; Sh. 6.3 trilioni ni kwa ajili ya Mfuko Mkuu wa Serikali.

Mkuya amesema matumizi mengineyo Sh.3.7 trilioni, matumizi ya maendeleo ni Sh.5.9 trilioni bila kujumuisha matumizi ya kawaida yenye sura ya kimaendeleo.

Aidha, matumizi ya maendeleo ni asilimia 37.4 ya Bajeti yote ambayo inajumuisha matumizi ya kawaida yenye sura ya kimaendeleo yanayolipwa kupitia Mfuko Mkuu wa Serikali.

Mkuya ametaja mambo sita ambayo serikali itayapa kipaumbe kuwa ni kujizatiti katika ukusanyaji wa mapato ili bajeti hii itekelezwe kama ilivyopangwa, ili kuhakikisha wabunge kupitia Bunge wanasimamia utendaji wa mashirika ya umma ipasavyo pamoja na kutekeleza mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, serikali italipa ankara za umeme na maji za serikali kwa pamoja (Centrally) na fedha hizo zitatoka katika mafungu husika.

Mengine ni suala la madeni ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii kushughulikiwa na kumalizika, kuongeza kima cha chini cha malipo ya pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu kutoka Sh.50,000 hadi Sh. 85,000 na kukamilisha taratibu za kuwalipa mafao ya wazee.

Kuhusu wafanyakazi wa umma, Mkuya amesema serikali imeendelea kuboresha maslahi ya watumishi ikiwa ni pamoja na kuongeza mshahara wa kima cha chini kutoka Sh.65,000 mwaka 2005 hadi kufikia 265,000 mwaka 2014/15.

Aidha, serikali imeendelea kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi ya mishahara (PAYE) kwa kupunguza kiwango cha kodi cha chini kutoka asilimia 18.5 mwaka 2006/07 hadi asilimia 11 mwaka 2015/16 ikiwa ni punguzo la asilimia 35.

Deni la Taifa

Mkuya amesema serikali imeendelea kusimamia Deni la Taifa kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134. Aidha, msisitizo umewekwa kukopa mikopo yenye masharti nafuu tofauti na ile ya kibiashara ambayo inakopwa kwa uangalifu na kutumika kwenye miradi yenye vichocheo vya ukuaji wa uchumi.

“Hadi Machi, 2015, Deni la Taifa likijumuisha deni la ndani na la nje la Serikali pamoja na deni la nje la sekta binafsi lilifikia dola ya Marekani bilioni 19.5 sawa na Sh. 35 trilioni ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 18.7 sawa na Sh. 30.6 trilioni Machi 2014, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 21.

“Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni Sh. 25.6 trilioni sawa na asilimia 73.2 ya Deni la Taifa na deni la ndani ni Sh. 9.4 trilioni ambazo ni sawa na asilimia 26.8 ya Deni la Taifa,” amesema.

error: Content is protected !!