July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bajeti 2015/16 kugharamia uchaguzi, umeme, maji

Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya akiwa na begi la bajeti ya mwaka jana

Spread the love

SAADA Mkuya- Waziri wa Fedha na Uchumi, ametoa mwelekeo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2015/2016, akisema itaweka kipaumbele katika kugharamia uchaguzi mkuu na kukamilisha miradi inayoendelea na kuweka msukumo maalum kwenye miradi ya umeme vijijini, maji vijijini na kuimarisha rasilimali watu. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Akitoa mwelekeo huo leo jijini Dar es Salaam mbele ya wabunge, Mkuya amesema jumla ya matumizi ya bajeti hiyo itakuwa ni Sh. 22.4 trilioni, likiwa ni ongezeko la asilimi 16 ya bajeti ya mwaka 2014/2015 ya Sh. 19.6 trilioni.

 “Serikali itaendelea na juhudi za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuchukua hatua mbalimbali za kisera na kiutawala kwa lengo la kuongeza mapato kwa kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya mapato,” amesema Mkuya.

Amesema hatua hizo ni;- Kusisitiza matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji na kudhibiti upotevu wa mapato;

Kuhakikisha kuwa taasisi, wakala, mamlaka zinazojitegemea na mashirika ya umma yanakusanya ipasavyo mapato yasiyo ya kodi ili kupunguza utegemezi kutoka serikali kuu na kuwasilisha ziada kwenye mfumo mkuu wa serikali;

Kuendelea kuchukua hatua za kudhibiti misamaha ya kodi; Kuboresha mazingira ya kufanya biashara ili kuwezesha urasimishaji wa shughuli za biashara na kupanua wigo wa kodi;

Kupitia upya baadhi ya viwango vya kodi, ada na tozo mbalimbali ili viendane na hali halisi ya utoaji wa huduma husika;

Kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa kodi za majengo na kupitia upya viwango vya kodi ili zitozwe kwa kuzingatia thamani ya jengo badala ya utaratibu wa sasa wa viwango sawa;

Kuendelea kutafuta mikopo kutoka ndani na nje ya nchi kugharamia bajeti ya maendeleo kwa kuzingatia uhimilivu wa deni la taifa.

Mkuya amesema kwa kuzingatia sera za uchumi jumla pamoja na misingi na sera za bajeti kwa mwaka 2015/2016, sura ya bajeti inaonesha jumla ya Sh. 22,480.4 bilioni zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho.

“Jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh. 14,824.4 bilioni, sawa na asilimia 57.8 ya bajeti yote. Kati ya mapato hayo, serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh. 13,353.4 bilioni sawa na asilimia 90.1 ya mapato ya ndani,” Mkuya amesema.

Aidha, mapato yasiyo ya kodi na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri ni Sh. 949.2 bilioni na Sh. 521.9 bilioni. Serikali inategemea kukopa Sh. 5,767.8 bilioni kutoka vyanzo vyenye masharti ya kibiashara.

Pia, washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh. 1,888.2 bilioni sawa na asilimia 8.4 tu ya bajeti ikilinganishwa na asilimia 14.8 ya bajeti ya mwaka 2014/2015 ambazo sehemu kubwa ni mikopo ya masharti nafuu.

“Kwa upande wa matumizi, katika mwaka 2015/2016 serikali inapanga kutumia jumla ya Sh. 22,480.4 bilioni kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo, Sh. 16,711.2 bilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikijumuisha Sh. 6,612 bilioni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa serikali na taasisi,” amesema Mkuya

Katika bajeti hiyo, Sh. 2,600 bilioni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za serikali zinazoiva. Matumizi ya maendeleo yatakuwa Sh. 5,769.2 bilioni sawa na asilimia 25.9 ya bajeti yote ambapo kiasi cha Sh. 4,327.8 ni fedha za ndani sawa na asilimia 75 ya fedha za maendeleo.

 Mkuya amesema “shabaha na misingi ya bajeti kwa mwaka 2015/2016 inalenga: kuongeza kasi ya ukuaji wa pato halisi la taifa kufikia asilimia 7.2 mwaka 2015 kwa kutumia takwimu zilizorekebishwa za mwaka wa kizio wa 2007”.

Aidha, kuendelea kudhibiti kasi ya mfumko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja;

Kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri kufikia asilimia 15.7 ya pato la taifa; kuongeza mapato yatokanayo na kodi kufikia asilimia 14.2 ya pato la taifa;

“Matumizi ya serikali yanatarajiwa kuwa asilimia 20.7 ya pato la taifa; Kupunguza nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) hadi kufikia asilimia 3.6; Kasi ya ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi kuwa asilimia 16 mwezi Juni 2016,” amesema Mkuya.

Ameongeza kuwa mikopo kwa sekta binafsi itakuwa kwa asilimia 19.5 ya pato la taifa mwezi Juni 2016;

Kupunguza nakisi katika urari wa malipo ya nje ya kawaida unaojumuisha urari wa biashara ya bidhaa, huduma, mapato na vitega uchumi na uhamisho mali wa kawaida (current account balance including transfers) kufikia asilimia 10.7;

Pia, kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.

“Changamoto katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2014/2015 ni;- Kutokufikia malengo ya kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi kwa kiwango kinachotakiwa; Wafanyabiashara kugomea matumizi ya mashine za kielektroniki za ulipaji kodi (EFD’s),” ameongeza Mkuya.

Amezitaja changamoto zingine ni;- “Mapato ya ndani na nje kutokupatikana kama ilivyokadiriwa; Sera kulazimika kutoa fedha kwa mashirika ya umma ya biashara kama vile ATCL, TRL na TAZARA na hivyo kuongeza gharama ambazo zimepaswa kulipwa na mashirika yenyewe”.

Pia, mahitaji makubwa ya kuboresha miundombinu hususan ya maji, reli, bandari, viwanja vya ndege na barabara ili kukuza uchumi na kuongeza ajira na mchakato mrefu wa kupata mikopo ya kibiashara.

“Mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo, serikali itaboresha na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato; Kuendelea kusisitiza matumizi kulipa kodi na tozo mbalimbali kwa kutumia mitandao ya kielektroniki,” ameongeza Mkuya.

Mikakati mingine ni kuhakikisha kwamba hakuna kuingia mikataba mipya ya miradi na huduma bila kuwa na uthibitisho wa kuwepo kwa fedha; Kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa lengo la kuvutia uwekezaji wa ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma;

Kuimarisha mchakato wa kutathiminiwa kwa uwezo wa serikali wa kukopesheka na hivyo kuingia kwenye soko la fedha la kimataifa kukopa kwa masharti bora zaidi;

Kukamilisha uandaaji wa kanuni za utekelezaji wa Sheria ya Bajeti na kuendelea kuimarisha mfumo wa kieletroniki wa usimamizi wa malipo (IFMS).

Akizungumzia kuhusu bajeti hiyo, Esther Bulaya, Mbunge wa viti Maalum (CCM), amesema “zaidi ya asilimia 60 ya bajeti iliyopita haijatekelezwa. Mwaka jana Miradi ya maendeleo ilitengewa trilioni sita, zimetoka trilioni mbili. Deni la taifa linaongezeka kutoka trilioni 18 hadi 19. Bajeti ya mwaka huu ni ngumu na haina matumaini.”

error: Content is protected !!