August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bajaji, daladala mikononi mwa RC Rugimbana

Jordan Rugimbana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma

Spread the love

JORDAN Rugimbana, mkuu wa Mkoa wa Dodoma ameombwa kuingilia kati mgogoro kati ya madereva wa daladala na bajaji ambao wamekuwa na mvutano mkubwa katika kituo cha Mashujaa, Manispaa ya Dodoma, anaandika Dany Tibason.

Madereva bajaji wamekuwa wakilalamikia vitendo vya madereva wa daladala kuendesha bila uangalifu – ‘kuwachomekea’ na kuwasababishia ajali mara kwa mara kiasi cha kuhatarisha usalama wa vyombo hivyo na uhai wa binadamu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na MwanaHALISI Online, wamesema wanakumbana na changamoto kubwa kuitoka kwa madereva wa daladala

Hasani Mohamedi dereva wa bajaji mjini Dodoma amesema umefika wakati kwa serikali ya mkoa kuwawekea miundombinu mizuri ya kazi na kuepusha ajali za mara kwa mara.

“Inabidi Mkuu wa Mkoa aingilie katika ili kunusuru hali hii, tumekuwa na mvutano wa mara kwa mara kati yetu na watu wa daladala na kila mtu anajiona ana haki kuliko mwenzake. Jambo hili linachochewa pia na ushindani wa kibiashara kwani wao wanaona tunachukua abiria wao,” amesema.

Jafari Salum, katibu wa umoja wa madereva wa daladala ziendayo, Kisasa, Area D amesema madereva wa Bajaji ni kero kwani wanapita na kuweka vituo katika njia ambazo zimesajiliwa kwa ajili ya biashara ya daladala.

“Imekuwa kawaida kwa madereva wa bajaji kupita katika njia za daladala na kuanza kupakia abiria jambo ambalo linakuwa kero kwa kwa daladala kwani madereva daladala wanalipia ushuru mkubwa ilihali madereva bajaji wanapakia abiria kwenye vituo hivyo,” amesema.

Jordan Rugimbana, Mkuu wa Mkoa wa Dadoma, amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema kuwa tayari ofisi yake inafanyia kazi changamoto hiyo ili kuipatia ufumbuzi wa kudumu na kwamba kwa sasa ni kipindi cha mpito tu.

error: Content is protected !!