Spread the love

 

ASKOFU wa Kanisa la Kiingili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe Mkoa wa Kagera, Dk. Benson Bagonza ametoa uchambuzi wa namna ya kumwondolea uaskofu mtu ambaye amewekwa wakfu kuwa askofu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kagera … (endelea).

Uchambuzi huo ameutoa siku chache kupita tangu KKKT Dayosisi ya Konde kutangaza kumwondolea wakfu wa Uaskofu, Dk. Edward Mwaikali aliyekuwa askofu wa Dayosisi hiyo.

Aidha, uliviondolea wakfu vifaa vya Kiaskofu alivyokuwa anatumia pete, msalaba na fimbo ambavyo alikabidhiwa tarehe 18 Januari 2018 alipowekwa wakfu kuiongoza Dayosisi ya Konde.

Hayo yalifanyika Jumapili ya tarehe 5 Juni 2022 siku ambayo ilitumika pia kumweka wakfu mrithi wake, Dk. Geofrey Mwakihaba.

Wamefikia hatua hiyo baada ya Dk. Mwaikali kugoma kuvirejesha ili vitumike kwa mrithi wake kwa mujibu wa taratibu za kanisa hilo. Mwaikali amekuwa anapinga kwa madai utaratibu uliotumika kumwondoa kwenye nafasi hiyo ni batili.

Dk. Mwaikali aliondolewa madarakani tarehe 22 Machi 2022 na Mkutano Mkuu Maalum wa KKKT Dayosisi hiyo kwa kile kilichoelezwa kushindwa kuiongoza vyema.

Usiku wa jana Jumatatu tarehe 6 Juni 2022, Askofu Bagonza alitumia ukurasa wake wa Facebook kuweka andika alilolipa kichwa cha habari ‘Baraka zizizofutika (Irrevocable Blessings).

Andika hilo liliibua mjadala kwa wachangiaji wa andiko lake. Soma kwanza andiko lenyewe hapa chini;

Uaskofu wa Mnyororo (Apostolic Sucession) ni baraka isiyofutika bila mchakato.

Hata kwa mchakato mrefu, utaishia kuchukua ofisi lakini si uaskofu.

Hata kwa hila kama za Rebeka alizofanya na mwanae mdogo Yakobo ili abarikiwe na baba yake badala ya mtoto mkubwa Essau, bado Mzee Isaka baba yao, alishindwa kufuta baraka alizompa Yakobo kwa kudanganywa (Mwanzo 27:2-29).

Essau alimlilia baba yake Isaka akiuliza Baba una mbaraka mmoja tu? Alilenga kumwomba ambariki yeye mlengwa baada ya baraka kuwa zimeenda kwa Yakobo kwa hila.

Isaka angeweza kutamka kuwa baraka zile naziondolea Wakfu lakini hakufanya. Kilichobarikiwa, kimebarikiwa milele.

Uaskofu wa mnyororo waweza kuondolewa kwa mchakato endapo mambo mawili yametokea. Kwanza, ikiwa Askofu amekengeuka imani.

Hili hupimwa na jopo la wataalamu kwa muda mrefu na hasa kama Askofu hakufundisha huo uzushi wake. Jopo hilo hupeleka ripoti kwa baraza la waweka wakfu ambao nao humhoji mhusika.

Kama wamejiridhisha kuwa amekengeuka imani, aghalabu, wanaweza “kujaribu” kutengua wakfu. Nimesema wanaweza kujaribu!

Pili, ni ikiwa Askofu amekiuka maadili yanayoambatana au kufikia kiwango cha ibada ya sanamu (idolatry). Hii ni hali ya mtu kuamini kuwa bila kutenda tendo fulani(ovu) hawezi kufanya kazi zake za kitume.

Nje ya haya ni hakuna uwezekano wa kuondoa wakfu kwa Askofu. Ndiyo maana mchakato wa kumpata Askofu unahitaji kuwa wa umakini.

Siyo suala la kukusanya watu tu na kuwaamuru wanyoshe mikono wamchague Askofu. Wanaweza kuishia kumchagua aliyetokea amevaa vizuri siku hiyo!

Bila mchakato, kumvua mtu uaskofu ni kuikanyaga huduma ya uchungaji kwa kuilisha sumu jamii unayoitangazia. Hata inapobidi kumvua, si suala la kutangaza hadharani.

Ni wahusika ndo hujulishwa kwa utulivu na moyo mzito sana. Kutangaza kuvua uaskofu kwa bashasha kana kwamba unafurahia tendo hilo ni kujivua uaskofu wewe mwenyewe.

Makosa ya kutangaza hadharani ni sawa na kosa ninalofanya sasa kuwakosoa waliokosea wakati nami nakosea. Anyway, Mtoto akinyea mbeleko, mzazi hulazimika kumbeba humo humo.

Hila za Rebeka kutaka mtoto wake kipenzi Yakobo ndiye abarikiwe, zilimgharimu. Alimkosa Yakobo na Essau. Akamkosa mmewe. Watoto wakawa maadui na kutafuta kuuana. Hila hazijawahi kuacha mtu salama.

Baada ya andiko hili, kukaibuka mjadala na maswali mbalimbali ambapo Askofu Bagonza baadhi aliyajibu.

Gabriel Kamayugi alichangia hoja hiyo akiuliza; mbona nyie maaskofu mnafanya hayo kwa wachungaji wenu hadi kuwavua kola na kuwafungia wasifanye utumishi kwenye dayosisi yoyote ila hilo likifanyika kwa askofu mwenzenu inakua nongwa???

Askofu Bagonza alimjibu akisema, nijuacho kwenye uchungaji kuna anayejivua mwenyewe. Na kuna wanaoweza kuvuliwa kulingana na nadhiri waliyoiweka. Hili lina mchakato. La kwanza halina.

Kamayugi akamuuliza tena, kama la kwanza halina mchakato nini kazi ya halmashauri kuu ya dayosisi ilihali mchungaji akija kubarikiwa lazima halmashauri ikae na kukubali??? Kama la kumpata na kumuweka wakfu askofu lina mchakato kwanini mchakato uliotumika kumuweka usitumike kumtoa?

Askofu Bagonza akamjibu, kwa anayejivua halmashauri kuu haina nafasi isipokuwa kupewa taarifa tu. Wito huu ni hiari kwa hiyo akiamua kuuacha hawezi kulazimishwa.

Naye Jackson Ngeresa akauliza, vipi kuhusu Askofu kwenda mahakamani ilikuwa ni halali kwa kanisa?

Askofu Bagonza akamjibu, kuna mambo ni dhambi lakini si makosa. Kuna mambo ni makosa lakini si dhambi. Askofu kwenda mahakamani laweza kuwa kosa lakini si dhambi. Nimetaja mambo mawili ya kumvua mtu uaskofu. Kwenda mahakamani halimo. Kuna wakati kutokwenda mahakamani ni dhambi na kosa. Hilo lisubiri siku nyingine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *