August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bageni ahukumiwa kunyongwa, Zombe ‘roho ya paka’

Spread the love

MAHAKAMA ya Rufaa imemuhukumu ASP Christopher Bageni, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, kunyongwa hadi kufa baada ya kutiwa hatiani kwa kuhusika na mauaji ya kukusudia ya wafanyabiashara watatu wa madini,anaandika Faki Sosi.

Wakati ASP Bageni akihukumiwa kunyongwa hadi kufa Kamishina Msaidizi wa Polisi, Abdallah Zombe, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO) na wenzake wawili wameachiwa huru.

Hukumu ya mahakama hiyo, ilikuwa ikisikilizwa na jopo la majaji watatu. Benard Luanda, Sauda Mjasiri na Semistocles Kaijage, kufuatia rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuwaachia huru maofisa hao.

Akisoma hukumu hiyo leo, John Kahyoza, Msajili wa mahakama ya Rufaa, amesema mahakama ilichambua ushahidi wa mashahidi 37 uliotolewa na Mahakama Kuu wakati kesi hiyo ilipokuwa ikisikiliziwa na kisha wajibu rufani hao kuachiwa huru.

“Baada ya kupitia hoja zote zilizotolewa na pande zote pamoja na maamuzi ya Mahakama Kuu, ndipo Mahakama ya Rufaa imetengua  kuachiwa huru kwa mjibu rufani ASP Bageni na kumtia hatiani kwa makosa manne ya mauaji,” amesema Kahyoza.

Amefafanua kuwa, ushahidi uliotolewa umeonyesha kwamba Bageni ambaye alikuwa Mkuu wa Upelelezi Kinondoni (RCO), alikuwepo eneo la Pande ambapo wafanyabishara hao waliuawa.

Msajili Kahyoza amesema Mahakama ya Rufaa ilijiuliza  nani aliyetoa amri kwamba marehemu wapelekwe msitu wa Pande, nini ilikuwa nia ya watu hao kupelekwa huko ambapo hakukuwa na  nyumba.

Ameeleza kuwa kulingana na ushahidi uliotolewa na Koplo Rajabu Bakari, mpinga rufaa wa nne, ASP Bageni alikuwepo eneo la tukio na kulingana na cheo alichokuwa nacho alikuwa na uwezo wa kutoa amri kwamba tukio hilo lisifanyike.

“Mahakama imejiridhisha kuwa ASP Bageni alikuwepo eneo la tukio ingawa haijathibitika kwamba aliamuru mauaji lakini alisaidia mauaji kwa kiasi kikubwa kwani alikuwa na mamlaka ya kuzuia mauaji hayo,” amesema.

Kunusurika kwa ACP Zombe

Msajili Kahyoza amesema kuwa, mahakama imemuachia huru ACP Abdallah Zombe kutokana na ukweli kwamba, ushahidi uliotolewa haujamtia hatiani.

“ACP Zombe, ASP Ahmed Makele na Koplo Rajabu Bakari wanaachiwa huru kutokana na ushadidi kutojitosheleza kuwatia hatiani,” amesema Kahyoza.

Wajibu rufani hao, walidaiwa kutenda makosa hayo tarehe 14 Januari, 2006, katika Msitu wa Pande uliopo Mbezi Luis, jijini Dar es Salaam kwa kuwapeleka na kuwaua wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na dereva teksi wa Manzese Juma Ndugu.

17 Septemba, 2009 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliwaachia huru washtakiwa wote, ikisema “Baada ya kusikiliza ushahidi na hoja za mawakili wa pande zote imeridhika kuwa washtakiwa wote hawakuwa na hatia ya mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.

Jaji Salum Massati aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo alisema, Mahakama imebaini kuwa walioshtakiwa siyo waliohusika na mauaji hayo na kwamba wauaji hawakuwepo mahakamani na kuagiza Jamhuri iwasake wauaji na kuwafikisha mahakamani.

error: Content is protected !!