RAIS mteule Donald Trump wa Marekani amebakisha muda usiozidi siku mbili kabla ya kuapishwa rasmi kuwa rais wa taifa hilo lenye nguvu kubwa ya kiuchumi duniani, anaandika Wolfram Mwalongo.
Trump anatarajia kuapishwa Ijumaa ya wiki hii (tarehe 20 Januari), tayari kuiongoza Marekani ingawa takwimu za mtandao wa habari wa NBC zinaonesha kuwa ni asilimia 44 tu ya Wamarekani wanaoafiki ushindi wake.
Takwimu za NBC zinashabihiana na ushindi wa Trump wa asilimia 46 alioupata katika uchaguzi mkuu wa tarehe 8 Novemba mwaka jana.
Ijumaa ya wiki hii Trump anatarajia kuhamishia rasmi makazi yake katika Ikulu ya White House huku Barack Obama akitarajia kufungasha kila kilicho chake.
Wakati takwimu za NBC zikionesha kuwa Wamarekani wana imani na Trump kwa asilimia 44 tu, mtangulizi wake Barack Obama katika kipindi kama hiki mwaka 2009 aliingia Ikulu huku akiungwa mkono kwa asilimia 71.
George Bush Rais wa 43 aliingia Ikulu mwaka 2001akikubalika kwa silimia 57 huku Bill Clinton mwaka 1991akiwa na asilimia 77.
Wachambuzi wa masuala ya siasa za Magharibi wamesema huenda wapinzani wa Trump wakatumia mwanya huo kuzorotesha uongozi wake kama njia ya kumwangusha katika uchaguzi unaofuata.
Hata hivyo bilionea huyo anaonekana kutojali maneno yanayozungumzwa huku akisema yupo tayari kurejesha hadhi ya taifa hilo.
Mpaka sasa ameendelea kupiga vita jumuiya za kimataifa anazoamini taifa lake linachangia kiasi kikubwa cha fedha katika mambo yasiyo na maslahi kwa Marekani.
Leave a comment