Friday , 3 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Babu Duni, Othman waanika vipaumbele 10
Habari za Siasa

Babu Duni, Othman waanika vipaumbele 10

Juma Duni Haji
Spread the love

 

MWENYEKITI mpya wa Chama cha ACT-Wazalendo, Babu Juma Haji Duni na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Othman Masoud Othman wametaja vipaumbele 10 ambavyo watavisimamia katika kipindi cha uongozi wao. Anaripoti Selemani Msuya, Dar es Salaam … (endelea).

Aidha, viongozi hao wamesema pamoja na vipaumbele hivyo katika kipindi cha uongozi wao watahakikisha Tanzania Bara inakuwa ya zambarau kama ilivyo Zanzibar.

Viongozi hao wapya wamesema hayo leo tarehe 1 Februari, 2022 wakati wakizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni siku tatu zimepita baada ya kuchaguliwa kwa kishindo na wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho uliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Ubungo jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo maalumu ulifunguliwa na Rais wa Chama cha Citizens Coalition for Change (C.C.C), Nelson Chamisa ambapo aliwataka viongozi watakaochaguliwa kuhakikisha wanafanikisha mabadiliko ya kisiasa, kijamii na maendeleo nchini na Afrika.

Duni ametaja vipaumbele vyake vitano ambavyo mosi ni kusimamia mageuzi ya uendeshaji wa chama kisasa ambapo aliweka bayana kuwa Halmashauri Kuu ya Chama Taifa, kwenye kikao chake cha Januari 28, 2022 imeidhinisha program ya ACT Kiganjani ambayo inakusudia kuendesha chama kisasa.

“Program hii, pamoja na mambo mengine, itawawezesha wanachama kusajiliwa na kulipia ada za uwanachama kwa simu. Pia, programu itawezesha mawasiliano ndani ya chama na upashanaji wa habari za chama kufanyika kwa mtandao.

“Nitatumia muda wangu mwingi kuisimamia Sekretarieti na ngome ya vijana ambayo ndio iliyopewa dhamana ya kusimamia usajili wa wanachama kwa kushirikiana na viongozi wa ngazi husika kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao,” amesema.

Mwenyekiti huyo amesema anahimiza wanachama wote nchini ambao bado hawajajisajili kwenye mfumo wa ACT Kiganjani wafanye hivyo.

Ametaja kipaumbe cha pili ni Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya na kwamba tangu kuanzishwa vyama vingi kumekuwa ni kilio cha vyama vya upinzani na wadau wa demokrasia kuwa nchi inahitaji tume huru na Katiba Mpya.

Amesema ACT imejipanga vizuri kuhakikisha mwaka 2022 unakuwa mwaka wa kudai tume huru ya uchaguzi na Katiba mpya ili kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025 unakuwa huru, wa haki na wa kuaminika.

“Kipaumbnele change cha tatu ni kuendeleza siasa za hoja, kwa kushirikiana na ofisi ya Kiongozi wa Chama ambaye ndiye msimamizi mkuu wa sera, nitahakikisha kuwa chama kinaendelea kujipambanua kwa siasa za hoja muhimu za kitaifa kama kisiasa, kiuchumi na kijamii,” alisema.

Aidha alisema ACT kitaendelea kuwa sauti ya wananchi wa chini ambapo alibainisha kuwa utafiti wao wa hivi karibuni unaonesha kuwa hali ya maisha nchini ni ngumu kutokana na kupanda kwa bidhaa muhimu.

“Mathalani, katika msimu huu wa kilimo, mbolea aina ya Urea imepanda kutoka shilingi 50,000 hadi shilingi 105,000 kwenye maeneo mengi. Hali ni hiyo hiyo kwenye bidhaa nyingi nchini ikiwemo mahitaji muhimu kama vile vyakula, mafuta na vifaa vya ujenzi. ACT Wazalendo itaendelea kupaza sauti juu ya masuala haya na mengine kuhakikisha kila Mtanzania anaishi kwa raha, furaha na ustawi,’ amesema.

Babu Duni amesema kipaumbele cha nne katika uongozi wake kitakuwa ujenzi wa taasisi imara ambapo amejipanga kuimarisha mshikamano wa ndani ya chama hasa mwaka 2022.

Mwenyekiti huyo amesema kipaumbele cha tano ni kupigania na kutetea haki, umoja na maridhiano. “Nitaendeleza pale alipoishia Maalim Seif Sharif Hamad kwa kupigania haki, umoja na maridhiano yatakayowezesha nchi yetu kupiga hatua kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Pia, nitashirikiana na Makamu Mwenyekiti Zanzibar kuhakikisha kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unakuwa wa haki na usawa. Hili litawezekana kupitia kuandikwa kwa Katiba Mpya ambayo itaipa Zanzibar mamlaka yake kamili na kuweka usawa baina ya washirika wawili wa Muungano; Tanganyika na Zanzibar.,” amesema.

Aidha, Babu Duni amesema pamoja na vipaumbele hivyo, pia kuna maswali kutoka kwa waandishi na wanachama wa ACT kuwa ataweza kuvaa viatu vya Maalim Seif, ambapo aliweka wazi kuwa Maalim Seif hakuwa kiongozi wa kawaida na kwamba viongozi wa aina yake hutokea mara chache duniani. Hivyo hataweza kulinganishwa naye.

“Lakini, nawahakikishieni kuwa nami nina uzoefu wa muda mrefu wa kutosha wa muda mrefu na maarifa ya kutosha ambayo nitayatumia katika kukiongoza chama cha ACT Wazalendo katika kufikia mafanikio yake ya kushika dola na kuwakomboa Watanzania kiuchumi, kisiasa na kijamii,” amesema.

Mwenyekiti huyo amesema katika kuthibitisha hilo anajipanga kuja kuzindua ACT upande wa Tanzania Bara ili iwe kama upande wa Zanzibar.

“Bara inahitajika kuzinduliwa ili iwe zambarau, hili naliweza na muda mchache ujao nitaanza kazi hiyo ya kuizindua ACT Watanzania wanipokee,” amesema.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Othman ametaja vipaumbele vyake vitano kuwa ni kuwaunganisha wanachama wote kuwa pamoja na kushirikiana katika shughuli za kijamii na kusiasa na kukataa kugawika kwa namna yoyote ile ili kuimarisha nguvu ya kisiasa ya chama chetu Unguja na Pemba.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) aemtaja kipaumbele cha pili ni kusimamia uwajibikaji wa kitaasisi ambapo kila kiongozi wa chama wa ngazi yoyote kutoka tawi hadi taifa wanatimiza wajibu wao kwa mujibu wa Katiba, kanuni na maelekezo mbalimbali ya chama.

“Pia kuhuisha utamuduni wa kukifanya chama kuwa chemuchemu ya fikra mbadala kwa kuibua hoja katika mijadala ya kitaifa inayopelekea kuimarishwa kwa sera na sheria mbalimbali za kitaifa zinazogusa maslahi ya moja kwa moja ya wananchi.

Nne ni kuendelea kusimamia maridhiano ya kisiasa yaliyoasisiwa na mtangulizi wangu, Maalim Seif na kwamba chini ya uongozi wangu ACT Wazalendo kitabaki kuwa ni chama kinachopigania haki za kijamii, kisaiasa na ustawi wa kiuchumi kwa wananchi wote, kwa lugha ya Kizanzibari, “Safari ya kuelekea Singapore ipo pale pale chini ya ACT Wazalendo,” alisisitiza Othman.

Amesema wakiyafikia hayo kama watasimamia kwa dhati maridhiano ya kisiasa. “Katika hili la maridhiano ya kisiasa; nitatumia nafasi yangu ya makamu mwenyekiti na makamu wa kwanza wa rais kusimamia mambo ya msingi yaliyokubaliwa baina yetu kabla hatujaingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema.

Makamu Mwenyekiti ameyataja mambo hayo ni kuufanyia mabadiliko mfumo wa uchaguzi ili kuwa na mfumo wa unaohakikisha kuwepo kwa uchaguzi huru, haki na unaoaminika na wadau wote wa uchaguzi.

Amesema watafanya hivyo kwa kuhimiza na kupigania mabadiliko ya sheria mbalimbali zinazokwanza chaguzi huru na za haki.

Othman ametaja jambo lingine ni kufanyika kwa uchunguzi huru wa matukio ya uvunjaji wa haki za binadamu wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na kwamba waliohusika na matukio hayo kuchukuliwa hatua stahiki na wahanga nao kufidiwa.

Amesema lingine ni kutumia maarifa na uzoefu wake kwa kushirikiana na wenzake, watasimama na kujipanga kimkakati ili kuhakikisha chama chao kinajipanga vyema kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na tunavuka vikwanzo vyote vilivyowazuia huko nyuma kuunda Serikali.

Halikadhalika Othman ametoa wito kwa viongozi na wanachama wenzake kuungana pamoja, kuacha tofauti zao ndogondogo na kusimamia dhamira inayowaunganisha ndani ya ACT Wazalendo.

“Tukishikamana kwa pamoja naiona Zanzibar ya zambarau ikiwa nuru mpya ya matumanini kwa Wazanzibari wote, lakini pia hata Tanzania Bara ya zambarau inawezekana,” amesema.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Vijana ACT-Wazalendo Dar wampa tano Rais Samia

Spread the love  NGOME ya Vijana ya Chama cha ACT-Wazalendo, kimempongeza Rais...

Habari za Siasa

ACT-Wazalendo yaiangukia Serikali kunusuru wananchi Liwale, Nachingwea

Spread the love  CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimeitaka Serikali kuchukua hatua za haraka...

Habari za SiasaTangulizi

Vigogo wanaokwamisha mradi Liganga na Mchuchuma kitanzani

Spread the love  NAIBU Spika wa Bunge, Mussa Zungu, watu wanaokwamisha utekelezaji...

Habari za Siasa

Gridi ya Taifa kufumuliwa kukabiliana na katizo la mgao wa umeme

Spread the love  WAZIRI wa Nishati, Januari Makamba, amesema Serikali ina mpango...

error: Content is protected !!