AMMY Lukule ambaye ni mhasibu katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya amefanya mauji kwa familia yake kutokana na wivu wa mapenzi, Anaripoti Hamis Mguta.. (endelea).
Lukule amefanya tukio hilo usiku wa kuamkia jana na kisha kutimkia pasipojulikana.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Benedict Kitalika amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na
kusema kuwa muuaji alifanya tukio hilo usiku wa kuamkia jana nyumbani kwake eneo la Kimara jijini Dar es Salaam na kisha kutokomea kusikojulikana.
“Ni kweli mwanaume mmoja ambaye anafanya kazi ya uhasibu katika hospitali ya rufaa ya Mbeya, aliyejulikana kwa jina la Ammy Lucas Lukule, ameua mke, mtoto na shemeji yake, inasemekana kulikuwa na ugomvi ambapo mwanaume alikuwa akimtuhumu mkewe kuwa mtoto mdogo siyo wake na anajihusisha na mapenzi na wanaume wengine, hivyo aliamua kuwaua kwa jembe na kukimbia”, amesema Kamanda Kitalika.
Kamanda Kitalika amesema kuwa baada ya kufanya tukio hilo mtuhumiwa huyo aliacha ujumbe kuwa polisi wasihangaike kwani yeye ndiye kafanya mauaji hayo.
Jeshi la Polisi limesema taarifa za tukio hilo walizipata kutoka kwa majirani baada ya kugundua hakuna dalili ya kuwepo watu kwenye hiyo nyumba na kuanza kuchunguza, ndipo walipogundua hayo na kuita polisi kuvuja mlango.
Kamanda Kitalika amesema jeshi la polisi linaendelea kufanya uchunguzi wake kubaini alipo mhusika na kumchukulia hatua za kisheria.
Waliouawa wametajwa kuwa ni Upendo Lukule ambaye ndiye mke, Magreth Samuel ambaye ni shemeji yake na mtoto mdogo mwenye chini ya mwaka mmoja.
Leave a comment