PAMOJA na kutolewa kwa elimu juu ya kujikinga na virusi vinavyosababisha ugonjwa hatari duniani wa corona bado jamii imekuwa na fikra hasi kwa madai kuwa watu weusi hawawezi kukumbwa na ugonjwa huo. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Hali hiyo imebainishwa na Mariam Masenga, mmoja wa wasimamizi wa zoezi la kunawa mikono kwa wafanyabiashara na wateja katika soko la Bonanza, jijini Dodoma linalouza samaki, mbogamboga na matunda.
Mariam alisema kuwa anakumbana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukutana na baadhi ya watu ambao wanakuwa wabishi kunawa mikono kwa madai kuwa watu weusi hawapatwi na corona.
“Kunatakiwa elimu kubwa sana kwa jamii, changamoto iliyopi, kuna watu wanakataa kunawa, wakidai kuwa eti wananawa kwani kuna chakula? wengine wanasema eti corona haiwapati watu weusi, inatulazimu kuwalazimisha na wakigoma hawaruhusiwi kuingia sokoni.
“Sijui nani katoa elimu kuwa watu weusi hawawezi kupatwa na ugonjwa huu wa corona, serikali na wataalamu wa afya wanatakiwa kutoa elimu ya kutosha ili kuondosha upotoshaji huu,” alisema Mariam.
Naye Katibu mkuu wa soko hilo, Dickson Mwesigwa alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa ugonjwa huo ambao ni tishio kwa dunia uongozi wa soko umelazimika kuweka vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na vitakatisha mikono katika milango miwili ya soko na kuwaweka wasimamizi ambao watahakikisha kila anayeingia sokoni hapo ananawa mikono.
Alisema kuwa vifaa hivyo ambavyo vimewekwa katika milango maalumu ya kuingilia katika soko hilo na kuwaweka wasimamizi ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha ananawa mikono pindi anapotaka kuingia ndani ya soko na bila kujali anayeingia sokoni ni mfanya biashara au ni mteja.
“Sokoni tunapokea watu wengi, huwezi kujua nani mwathirika na ni nani ambaye yupo salama kutokana na hali hiyo uongozi wa soko la bonanza ambalo ni maarufu kwa kuuza samaki, matunda na mbogamboga ,tumeamua kutekeleza kwa vitendo maagizo ya serikali na wataalamu wa afya kwa kuweka vifaa mbalimbali vya kujikinga na ugonjwa huo,” alisema Katibu Mwesigwa.
Leave a comment