BAO la dakika ya 90 +4 la Steven Sey lilitosha kuipatia Namungo sare kwenye mchezo dhidi ya Azam FC, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 na kuifanya Azam FC kucheza mchezo wa sita bila kupata ushindi. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).
Mchezo huo ulichezwa kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi mbele ya kicha wake mpya, George Lwandamina akiiongoza timu hiyo kwa mara ya kwanza tangu alipopewa kibarua cha kuinoa mara baada ya kutimuliwa kwa Aristica Cioaba.
Azam ilikuwa ya kwanza kutangulia kwenye mchezo huo baada ya kupachika bao la kwanza lililofungwa na Iddi Nado dakika ya 19 na dakika tano baadae beki wa kushoto wa Namungo Edward Manyama alichomoa bao hilo kwenye dakika ya 24 kwa mpira wa adhabu ndogo na kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa zimetoshana nguvu.
Dakika ya 74 kipindi cha pili, Nado aliiandikia Azam bao la pili huku timu hiyo ikiwa na matumaini ya kuondoka na pointi tatu ndipo Steve Sey mshambuliaji raia wa Uganda aliipachikia Namungo bao la kusawazisha baada ya kuunganisha kona iliyopigwa na Lucas Kikoti kwenye dakika ya 90+4.

Kwa matokeo hayo Azam itasalia kwenye nafasi ya tatu ikiwa na pointi 28 baada ya kucheza michezo 15, ikiwa nyuma kwa pointi moja dhidi ya Simba ambayo imecheza michezo 13, huku Yanga akiendelea kusalia kileleni akiwa na pointi 37 na michezo 15.
Namungo imepanda mpaka nafasi ya 13 ikiwa na pointi 17 baada ya kucheza michezo 13 na mechi mbili mkononi.
Mchezo ujao wa Ligi Azam itashuka dimbani dhidi ya Ruvu Shooting ambayo inashika nafasi ya nne kwenye msimamo ambayo ilicheza michezo saba bila kupoteza kabla ya kufungwa na Yanga kwa mabao 2-1.
Leave a comment