SERIKALI imezitaka Asasi za Kiraia (AZAKI) kusimamia vyema matumizi ya fedha za miradi, ili ziwanufaishe walengwa. Anaripoti Danson Kaijage…(endelea).
Wito huo umetolewa na Mwita Waitara, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wakati akizungumza na wakurugenzi wa AZAKI katika zoezi la kusaini mikataba ya ruzuku, lililofanyika jijini Dodoma.
Waitara amezitaka AZAKI hizo kuunda mifumo mizuri ya usimamizi wa fedha, ili kudhibiti mianya ya ubadhirifu wa fedha za miradi.
Aidha, Waitara amezitaka AZAKI zote nchini kufanya kazi kwa kushirikiana na Maafisa wa Serikali za Mitaa pamoja na Halmashauri , kwenye maeneo yanayotekelezwa miradi .
“Niwaombe sana, hakikisheni mnafanya matumizi sahihi ya fedha za miradi na kuhakikisha walengwa halisi wanafikiwa na kufaidika na miradi hiyo, pia mhakikishe mnawahusisha maafisa wa serikali za mitaa kwenye maeneo ya utekelezaji” amesema Waitara.
Pamoja na hayo, Waitara amesema serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Asasi za Kiraia nchini katika kusukuma mbele maendeleo vijijini, kuleta teknolojia mpya na rahisi kwa wananchi, sambamba na kupinga mila potofu na kandamizi miongoni mwa jamii hasa maeneo ya pembezoni.
Pia , Waitara ameziomba AZAKI kuwajengea uwezo wananchi pamoja na viongozi wa serikali za mitaa ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kupitia mafunzo mbalimbali katika miradi, ili washirikiane kutatua changamoto zilizopo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uwezeshaji wa AZAKI, Francis Kiwanga, amesema mwaka huu watatoa ruzuku kiasi cha Shilingi 11.7 Billioni kwa asasi za kiraia 154, ambazo zimekidhi vigezo vya kupewa ruzuku ili wakatekeleze miradi yao.
Kiwanga amesema dhumuni la taasisi hiyo ni kuwekeza katika utoaji wa ruzuku kwa AZAKI, na kuleta mabadiliko chanya yanayogusa maisha ya watanzania kupitia AZAKI zao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Tusonge kutoka Moshi, Aginata Rutazaa amesema watahakikisha wanaweka uwazi katika matumizi ya fedha ili ziweze kuleta tija kwa wahusika.
Leave a comment