WADAU wa haki za kijamii nchini wameiomba serikali kurekebisha baadhi ya mapendekezo ya marekebisho ya sheria mbalimbali, ikiwemo Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Sheria ya Takwimu. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Akisoma tamko la Asasi za Kiraia (AZAKI) leo tarehe 22 Juni 2019 Jijini Dodoma, Wakili Anna Henga, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC), amesema baadhi ya marekebisho hayo yemelenga kudhibiti utendaji wa asasi hizo.
Wakili Henga amesema kama marekebisho hayo yatapitishwa na Bunge na kuwa sheria, asasi nyingi na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’S) yatashindwa kufanya kazi nchini, kutokana na kuwekewa masharti magumu na yasiyotekelezeka.
“Kwa ujumla mabadiliko yanayopendekezwa katika sheria hizo yanalenga kudhibiti utendaji kazi wa asasi za kiraia, hivyo kuathiri namna wananchi wanavyoweza kufurahia haki yao ya kujumuika na kueleza maoni yao kwa uhuru , haki ya kushiriki katika maamuzi yanayowathiri na kuwawajibisha viongozi wao,” amesema Wakili Henga na kuongeza.
“Zitatokea athari za kiuchumi na kijamii zinazotokana na vikwazo kwa asasi za kiraia, endapo marekebisho haya yatapitishwa kama yalivyo. Mashirika mengi ya kiraia yatafutiwa usajili na kushindwa kuanza tena, madhara kadhaa yatatokea ikiwemo wananchi kukosa huduma za taasisi hizo.”
Akifafanua baadhi ya mapendekezo hayo, Wakili Henga amesema kifungu namba 25 cha mapendekezo ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, tafsiri ya asasi za kiraia haitoshelezi kutokana na kutojumuisha kazi ya utetezi wa haki za binadamu na makundi chechemuzi ya masuala ya utawala bora.
Pia, Wakili Henga amesema kama mapendekezo hayo yatapitishwa kuwa sheria, asasi za kiraia zitatakiwa kusajiliwa upya ndani ya miezi miwili, na kwamba kipindi hicho kikipita hazitaruhusiwa kufanya kazi hata kama zina usajili.
“Mapendekezo yanatishia ustawi wa asasi za kiraia , yatabatilisha kazi za msingi zinazofanywa na asasi. Kwa mujibu wa marekekebisho ya sheria ya makampuni na vyama vya kijamii, shirika lolote linalofanya kazi za maendeleo haliwezi kusajiliwa kama kampunmi isiyotengeneza faida,” amesema Wakili Henga na kuongeza.
“Asasi yoyote ambayo itakuwa haijasajiliwa chini ya sheria sahihi kwa mujibu wa tafsiri mpya, zitapaswa kuomba usajili bila kujali zimesajiliwa tayari. Namba 28 na 36 kinyume chake asasi zimepewa muda wa miezi 2 kuhakikisha zinatekeleza masharti ya sheria mpya. Itatikisa asasi zinazofanya kazi, maana yake baada ya miezi miwili zitakuwa zimeondoka katika usajili.”
Wakili Henga amesema Azaki zimetoa wito kwa serikali kuratibu mashirika yasiyo ya kiserikali ili kujua idadi yake, pamoja na kufanya mabadiliko kwa uangalifu ili kufanya uamuzi sahihi.
“Tunapaswa kufanya mabadiliko kwa uangalifu na kufikiri kwa kina sana, hasa wakati huu ambao tuna muda wa kutafakari na kufanya uamuzi sahihi, vinginevyo tunaweza kuwa na nia njema lakini tukajitkuta tunafanya makosa na kupelekea madhara yasiyorekebishika, “ amesema Wakili Henga.
Pia, Azaki zimeiomba serikali kutoa muda wa kutosha kwa wadau na wananchi ili waweze kujadili mapendekezo ya sheria hizo, kwa minajili ya kuepusha madhara yanayoweza sababishwa na mapendekezo yasiyo sahihi.
Kuhusu mapendekezo ya Sheria ya Takwimu, Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la TWAWEZA amesema mapendekezo hayo yanaweka vikwazo kwa Azaki kutoa ama kuchapisha takwimu, kwa kutakiwa kuiomba ruhusa Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
“Taasisi nyingi ambazo hapo awali zilifungiwa kutoa takwimu bila kuomba ruhusa, sasa wameruhusiwa kutangaza takwimu zao isipokuwa asasi za kiraia, ruksa kuchapa kutangaza takwimu zao.
Lakini ukiwa asasi za kiraia bado tunaambiwa tuombe ruhusa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali. Sisi ombi letu hiko kikwazo kiondoelwe, tuweze kuchapisha takwimu zetu bila kuomba ruhusa,” amesema Eyakuze.
Aidha, Eyakuze ameipongeza serikali kwa kufanya marekebisho katika baadhi ya vifungu vya Sheria ya Takwimu, ambavyo vilikuwa vinazuia Watanzania kuhoji takwimu za serikali.
“Tumeanza kuona mwanga, mtakumbuka Septemba 2019 ilipitishwa Sheria ya Takwimu iliyobana Watanzania kupata takwimu na kuhoji takwimu za serikali. Tulikuwa tunapaswa kama takwimu za serikali tulibidi twende kwenye Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuhoji takwimu zao.
tulibanwa kutangaza takwimu huru zisizo za serikali, Lakini wenye marekebisho haya kidogo kamwanya kamefunguka, ukitaka kuhoji takwimu za serikali unayo nafasi lakini kwanza ukashauriane na ofisi ya takwimu,” amesema Eyakuze.
Leave a comment