January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

AZAKI wazindua Ilani ya Uchaguzi

Spread the love

ASASI za Kiraia (AZAKI) za nchini Tanzania zimebuni Ilani ya Uchaguzi na kuizundua rasmi mbele ya hadhara, katika hafla iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na viongozi wa asasi, wanasiasa na waandishi wa habari. Anaandika Pendo Omary … (endelea)

Ilani hiyo imekusudiwa kuwa dira na mwongozo wa kuzingatiwa na kila mshiriki katika hatua za uchaguzi mkuu wa mwaka huu ambapo Watanzania wanatarajiwa kupiga kura tarehe 25 Oktoba.

Wananchi, wagombea, vyama vya siasa, serikali na taasisi zake zenye jukumu katika kusimamia taratibu zikiwemo za ulinzi na usalama kufanikisha uchaguzi mkuu kwa lengo la kusaidia tume za uchaguzi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Pia ilani hiyo ni mwongozo kwa waomba ridhaa ya kuongoza ambao wanawajibu wa kuzingatia masuala ya msingi ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni yenye tija na maslahi mapana kwa umma kwa maendeleo ya taifa.

Ilani hiyo imebeba vipaumbele vikuu vya kuzingatiwa na vyama katika kutambua wajibu wao kulingana na mahitaji ya wananchi wanaoingia katika kutafuta uongozi wa nchi.

Vipaumbele hivyo ni Katiba Mpya, sera ya uchumi wa kitaifa (Sera inayolenga kulikwamua taifa kiuchumi kwa kujenga mazingira sawa ya kiuchumi kwa Watanzania wote bila ya kuweka matabanaka ya walionacho na wasionacho); usimamizi wa rasilimali za umma na ulinzi wa haki za binadamu, utawala wa sheria na mgawanyo wa madaraka.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ilani hiyo, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania, Bahame Nyanduga amesema ilani inalenga kuelekeza wananchi, wagombea, tume za uchaguzi, vyombo vya ulinzi na usalama na vyama vya siasa katika kutoa mchango wao kwenye usimamizi wa taratibu za kufanikisha uchaguzi mkuu.

Usimamizi huo unapaswa kuwa imara usioruhusu mwanya wa hatua hizo kutekelezwa kwa nguvu ya rushwa, hongo, matumizi ya nguvu upande wa vyombo vya ulinzi na usalama na rasilimali ya umma.

Onesmo Olengurumwa, Mkurugezi Mtendaji wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania – Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDs) – amesema wazo la kuweka wazi matakwa ya AZAKI juu ya Tanzania wanayoitaka katika mfumo wa ilani ya uchaguzi ilitokana na mkutano wa watetezi wa haki za binadamu uliofanyika 24 Julai, mwaka huu.

Lengo likiwa ni kutathmini nafasi ya AZAKI katika michakato ya upanuzi wa demokrasia ukiwemo uchaguzi mkuu.

“Mkutano huo uliazimia pamoja na mambo mengine, kuundwa kwa kikosi kazi kitakachoandaa rasimu ya ilani hii kwa niaba ya AZAKI. Inaleta faraja kwamba, ndoto hii imeweza kutimia na kuwezesha kukamilika kwa ilani hii,” amesema Olengurumwa.

Miongoni mwa asasi zilizochangia kubuniwa kwa ilani hiyo ya AZAKI, ni Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHCR), Mwamvuli wa asasi zisizo za kiserikali Zanzibar (ANGOZA), Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA).

Uzinduzi wa ilani hiyo umefanyika wakati vyama vya siasa vimo katika kipindi cha kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani. Kura itapigwa Oktoba 25 mwaka huu.

Siku hiyohiyo, Wazanzibari mbali na kuchagua viongozi hao, watakuwa na kura nyingine ya kumchagua Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani.

error: Content is protected !!