WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso ametangazia vita kwa wakandarasi na wahandisi ambao watakwamisha miradi ya maji inayotekelezwa serikali. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea)
Aweso ametoa onyo hilo jana tarehe 9 Septemba 2021, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa miradi 28 ya maji nchini.
Amesema katika kutekeleza lengo la kumtua mwanamke ndoo kichwani, serikali imeamua kuongeza kiasi cha Sh. bilioni 207 tofauti na kiasi cha Sh. bilioni 680 zilizotolewa na Bunge.
“Serikali imeazimia kuwa ifikapo mwaka 2025 asilimia 85 ya wananchi waishio vijijini wawe wanapata huduma ya maji huku asilimia 95 ya watu waishio mjini wakiwa wanapata maji safi na salama.
“Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 Bunge lilitenga kiasi cha Sh. bilioni 680 kwa ajili ya umuhimu Rais Samia Suluhu Hassan ameiongezea Wizara ya Maji kiasi cha Sh. bilioni 207,” amesema Awesso.
Aweso amesema Rais Samia ameidhinisha kiasi cha Sh bilioni 207 kurahisisha upatikanaji wa maji vijijini ikiwa ni dhamira yake ya kumtua Mama ndoo kichwani.
“Ili kuhakikisha wizara inafanikiwa kufikia asilimia 85 ya upatikanaji wa maji vijijini, kwa mwaka huu tumepanga kuingia mikataba 1176, hivyo tutawapa zabuni wakandarasi wenye uwezo kutekeleza miradi hii.
“Wakandarasi wazuri wanafahamika na wakwamishaji wanafahamika… moja ya changamoto ya ukwamishaji wa miradi ya maji ni wakandarasi wababaishaji wasio na uwezo, hatuwezi kuwapa nafasi kwenye wizara yetu,” ameeleza.
Pia Aweso amewataka Wakandarasi watakaoingia mkataba na wizara hiyo kulichukulia suala la maji kama vita mahususi ya kuhakikisha watanzania waishio vijijini wanaondokana na kero ya maji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph amewatoa hofu wakazi wa Jiji la Dodoma kuwa Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na wizara ya maji itahakikisha inatatua kero zote za maji kwa kuhakikisha miradi yote ya maji inatekelezwa kikamilifu.
Leave a comment