January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Awamu ya Pili ‘Wazazi Nipendeni’ yazinduliwa

Nembo ya Wazazi nipendeni

Spread the love

WIZARA ya Afya imezindua kampeni ya awamu ya pili ya Wazazi Nipendeni inayolenga kutoa elimu kwa jamii kuhusu uzazi salama ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto. Anaandika Faki Sosi, DSJ … (endelea).

Kampeni hiyo imezinduliwa leo jijini Dar es salaam na Kaimu Mkuregenzi wa Taasisi ya Wazazi Nipendeni, Dk. Ally Mohammedi Ally ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Donan Mmbando.

Akizungumza na waandishi wa habari Dk. Ally amesema, Julai 23 na 24 mwaka huu wataanza kutoa kutoa elimu ya uzazi salama katika viwanja vya Mwembeyanga jijini Dar es Salaam na kisha kuenea nchi nzima.

Amesema kuwa, kampeni hiyo itawalenga wanawake wajawazito pamoja na waume zao na pia jamii yote kwa ujumla ambapo watalenga usalama wa mtoto kabla ya kuzaliwa, anapozaliwa na hadi kufika umri wa mwaka mmoja.

Dk. Ally amesema kuwa, kampeni hii inalenga kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pia watoto chini ya miaka mitano.

“Tumepiga hatua katika kupunguza vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano kutoka 157 mwaka 1990 mpaka 54 mwaka 2013 kwa watoto 1,000 wanaozaliwa na kufikia malengo ya millennia.

“Hata hivyo hali sio nzuri kwa upande wa vifo vitokanavyo na uzazi kwani vimepungua kutoka 770 kwa mwaka 1990 hadi 410 mwaka 2014 kwa kila vizazi hai 100,00 tofauti na malengo tuliojiwekea,” amesema Dk. Ally.

Aidha amesema, wadau ambao wanaipa nguvu kampeni hiyo ni pamoja na USAID, CDC na Wizara ya Afya.

Kaimu Katibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto, Georgina Msema ameongeza kuwa, elimu hiyo imekuwa ikitolewa katika vyombo mbalimbali vya habari na kwa njia ya ujumbe mfupi ambapo elimu hutolewa bure kwa kutuma neno (mtoto kwenda 15001).

Aidha amesema kuwa, kampeni hiyo yenye kauli mbiu “Wazazi Nipendeni, Onyesha Upendo Wako” itahakikisha inatoa elimu kwa wazazi, wenza na watoa huduma na kwa zile sehemu ambazo hazifikiwi na radio, runinga au chombo chochote cha habari, kuna watu maalum ambao wanatoa elimu ya uzazi salama katika vijiji mbalimbali nchini.

error: Content is protected !!