February 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

ATCL watakiwa kubadilika

Spread the love

WATUMISHI wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) wamewashauriwa kuchukua hatua ya kubadilika kuendana na mabadiliko yaliyopo katika usafiri wa ndege kwa sasa ili kujenga msingi thabiti wa kuonesha ushindani kwa viwango vya kimataifa. Anaripoti Christina Haule … (endelea).

Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Mkoa wa Morogoro, Lucas Mwaisaka amesema hayo kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe wakati akifunga kikao cha pili cha baraza la wafanyakazi wa shirika hilo kilichofanyika mjini hapa.

Mwaisaka amesema kuwa ni ikiwa hawatabadilika mambo yote waliyojifunza yatakuwa ni kazi bure ambapo aliyataja mambo hayo kuwa ni mbinu za kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara na mbinu za kushindana kwa viwango vya kimataifa.

Aidha amesema kuwa kufuatia kauli mbiu ya ATCL kuwa ni “Tunaweza, Tubadilike” hivyo hawana budi kuchukua hatua ya kubadilika.

Hivyo ameuomba uongozi wa baraza na menejimenti ya shirika hilo kuchukua hatua za makusudi ya kuendelea kujenga uwezo wa wafanyakazi katika utekelezaji wa mambo muhimu yaliyotokana na mafunzo yaliyotolewa kwa ajili ya ustawi wa kampuni hiyo.

Hata hivyo amesema Serikali ya Awamu ya Tano imeonesha jinsi ilivyokusudia kuimarisha usafiri wa anga ili uchangie ukuaji wa utalii na uchumi wa nchi kwa kuongeza usafiri wa ndege na kufikisha ndege sita mpaka sasa ambapo aliwataka wajumbe hao kutumia fursa hiyo kuonesha kwamba wanaweza.

Naye Mkaguzi mkuu wa ndani wa ATCL Khamis Mambo amesema azma ya Rais John Magufuli imeweza kuwafanya kupiga hatua ya usafirishaji ambapo kabla ya ujio wa ndege mbili za mwanzo kampuni ilikuwa na asilimia 9.2 ya usafirishaji lakini baada ya kufikishwa wameweza kuwa na asilimia 24%.

Aidha Mambo amesema kuwa ATCL kwa sasa imeweza kubadilika na kuona namna ya kuhudumia wateja vizuri ili waweze kurudi huku ikihakikisha gharama za uendeshaji zinakuwa za chini ili wapate wateja.

Hata hivyo aliiasa jamii licha ya kutambua kuwa shirika hilo ni mali ya Umma inapaswa kutambua kuwa lazima liwe na mikakati ya kibiashara ili liweze kujiendesha.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Mawasiliano na Uchukuzi (COTWU) Taifa, Musa Mwakalinga aliiomba Serikali kuongeza mishahara kwa wafanyakazi wa shirika hilo ili kuendelea kuwajengea moyo wa kizalendo waliouonyesha tangu zamani.

Mwakalinga amesema kuwa wafanyakazi wa ATCL wamekuwa wakilalamikia kutopanda kwa mishahara yao licha ya ndege kuongezeka huku watumishi wakibaki wale wale.

“Haya ni malalamiko yao kwetu, nasi tunaelekeza kwa Serikali, nampongeza kwanza Mheshimiwa Rais kwa kuongeza na kuboresha usafiri wa ndege Tanzania lakini wafanyakazi wanaomba kuongezewa misharaha, ndege nyingi wafanyakazi wachache lakini waongezewe mishahara” alisema.

Naye Mfanyakazi wa kwenye ndege, Magreth Makwaia amesema, kufuatia mafunzo waliyopata wanaweza kuleta ufanisi mzuri katika kazi zao ikiwemo kutoa huduma nzuri kwa wateja wao na kuongeza wateja wengi zaidi ili wasiweze kwenda kwenye makampuni mengine kufuatia ushindani wa kibiashara uliopo wa sasa.

error: Content is protected !!