March 3, 2021

Uhuru hauna Mipaka

ATC yaleta taharuki Dodoma

Spread the love

NDEGE ya shirika la ndege la taifa (ATC), iliyokuwa imetokea Dar es Salaam kuja Dodoma leo Jumatano, imeshindwa kutua kwenye uwanja wa ndege mjini hapa kutokana na kuchafuka kwa hali ya hewa. Anaripoti Mwandishi Wetu kutoka Dodoma … (endelea).

Taarifa zilizothibitishwa na meneja wa ATC mkoani Dodoma, Harrieth Rutihinda zinesema, ndege hiyo iliyokuwa imewasili majira ya saa moja na nusu asubuhi, ililazimika kurejea Dar es Salaam, baada ya rubani kushindwa kuona njia za kutua.

“Ndege ilifika hapa katika muda wake wa kawaida. Lakini rubani alishindwa kutua kutokana na anga kugubikwa na ukungu. Akalazimika kurejea Dar es Salaam, ambapo baada ya hali ya hewa kutulia, ndipo ilipoanza tena safari ya kuja Dodoma,” ameeleza.

Kwa mujibu wa meneja huyo, pamoja na kwamba suala la ndege hiyo kushindwa kutua kwenye uwanja wa Dodoma kama lilivyopangwa limeleta usumbufu kwa abiria, lakini uamuzi wa rubani wa kurudisha ndege Dar es Salaam, ni uamuzi sahihi na wa kupongezwa.

Amesema, “kulikuwa hakuna namna. Uamuzi wa rubani wa kurudisha ndege Dar es Salaam, ni sahihi kuliko kama angeamua kuirudisha chini wakati njia hazioni kutokana na giza lililotanda.”

Kwa mujibu wa mtoa taarifa wetu ambaye alikuwa abiria kwenye ndege hiyo anasema, rubani alitumia muda mwingi kuzunguuka eneo la uwanja wa ndege wa Dodoma, kwa lengo la kutafuta njia bora na salama ya kutua.

“Wakati wote rubani alipokuwa anazunguuka uwanja, roho zetu zilikuwa zikitweta kwa hofu. Tunashukuru Mungu kuwa aliongozwa na maombi na hivyo kuamua kurejea Dar es Salaam,” ameeleza.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa huyo ambaye ni mbunge wa Bunge la Muungano, ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria kadhaa wakiwamo viongozi na mizigo lukuki, jambo ambalo lilimfanya rubani “kutua kwa riski.”

Shirika la ndege la ATC ambalo lilikuwa moja ya mashirika makubwa ya ndege katika ukanda huu wa Afrika Mashariki kabla ya kuteteleka, sasa limeanza kuimarika baada ya serikali kununua ndege zake yenyewe.

Kwa muda mrefu, ATC lilikuwa linaendeshwa kwa ndege za kukodi, jambo ambalo limeingiza shirika na serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.

error: Content is protected !!