Monday , 27 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Atakayewarudisha kwenye mapigano wakulima, wafugaji kukiona
Habari Mchanganyiko

Atakayewarudisha kwenye mapigano wakulima, wafugaji kukiona

Alhaji Mwalimu Mohamed Italy, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero
Spread the love

SERIKALI wilayani Mvomero mkoani Morogoro imesema, itashughulikia mtu yeyote ambaye atathubutu kuwarejesha nyuma kwenye mapigano ya wakulima na wafugaji ambayo wameshayasahau. Anaripoti Christina Haule, Mvomero … (endelea).

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mwalimu Mohamed Utaly wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake walipokuja kutaka kujua mipango ya Serikali ya uendelezaji wa Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), maarufu kama mkaa endelevu ambao unatarajia kuisha mwisho wa mwezi.

Mwalimu Utaly amesema, yeyote atakayebainika awe mfugaji au mkulima au askari baada ya kupindisha kesi kwa ajili ya kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji atachukuliwa hatua ikiwemo kufukuzwa kazi na kutopata ajira tena sehemu nyingine.

“Kwa sasa tunahakikisha askari anatekeleza majukumu yake vyema, hakuna kubeba mzigo wa mwingine, ukikamatwa papo hapo huna kazi na si vinginevyo sababu wafugaji wana pesa wanaweza kutoa rushwa,” amesema.

Amesema, wakati alipoteuliwa kuongoza wilaya hiyo mwaka 2016 mapigano kati ya wakulima na wafugaji yalikuwa mengi ila kupitia ushirikiano baina ya pande zote wilaya, vijiji na wadau wa mazingira hali sasa ni shwari.

Mwalimu Mtaly amesema wilaya ilichukua juhudi kubwa za mazungumzo ya pande mbili za wafugaji na wakulima na kuweza kuvunja makundi mawili hasimu ya morani na mwano yaliyokuwepo awali yakiendeleza mapigano wilayani humo.

Amefafanua kuwa kikundi cha wakulima kilichojulikana kwa jina la mwano kilikuwa na utaratibu wa kukamata mifugo inayoingia shambani mwa mkulima na kulipisha faini iliyojua huku ikibaki na sehemu ya mifugo ya wafugaji jambo ambalo baadae wafugaji waliliona kama uonevu na kuendeleza mapigano.

Aidha amesema, pia kikundi cha morani kilikuwa ni kikundi rika cha kabila la wamasai ambapo kukivunja ikawa shida bali walifanikiwa kuzivunja tabia zao za kutumia silaha za jadi kuwapiga wakulima na kufikia hatua hata ya kuwajeruhi na kuwaua.

“Ilifikia wakati wafugaji hawawezi kufika kwenye kijiji cha wakulima na hata hawawezi kupata huduma za kijamii pamoja na wakulima ikiwemo maji ya kunywa na hivyo kufanya wilaya kuweka mikakati ya utatuzi na kufanikiwa kwa asilimia nyingi,” amesema Mwalimu Utaly.

Hata hivyo Mwalimu Utaly amelishukuru Shirika la MJUMITA, TFCG na TaTEDO kupitia mradi wa mkaa endelevu kutoa elimu kwa jamii tangu mwaka 2017 na hivyo kuifanya jamii kuelimika na kujua thamani ya msitu na kuendelea kuitunza bila kuwepo migogoro yoyote.

Alisema, mashirika hayo kupitia mradi wa kuleta mageuzi katika sekta ya mkaa Tanzania maarufu kama mkaa endelevu yameweza kutoa elimu ya uhifadhi misitu inayozunguka vijiji, namna ya kulinda misitu hiyo kwa kutoa mafunzo ya mgambo na ukakamavu kwa baadhi ya vijana na kufanya uvunaji kwa njia endelevu inayofanya uhifadhi bora wa misitu na kuleta manufaa kwenye vijiji vya mradi.

Hivyo amesema, mradi wa mkaa endelevu umeweza kuwasaidia vijana kupata ajira, wanasiasa kujua namna ya kupambana na migogoro hiyo, Halmashauri na vijiji kupata makusanyo ya tozo za mauzo ya mkaa na kuyatumia kwa ajili ya maendeleo vijijini na pia viongozi wa vijiji kutambua kuwa wanao uwezo wa kumchukulia mtu hatua tofauti na zamani walikuwa wakiogopa.

Awali mmoja wa walinzi wa kamati ya msitu wa asili wa kijiji cha Kihondo kata ya Doma, Deusdedit Kalori amesema mapigano baina ya wakulima na wafugaji na masuala ya uvamizi misitu yameendelea kupungua kufuatia usimamizi unaofanywa chini ya mradi wa mkaa endelevu na kwamba hadi sasa tangu mradi uanze ni watu nane pekee wamejeruhiwa na wafugaji.

Hivyo hivyo waliiomba Serikali na wadau wengine wa uhifadhi misitu kuwasaidia kupata bunduki kama silaha za kuwawezesha kukabiliana na majangili wanaoingia msituni.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kasekenya aipa Tanroads wiki kukarabati barabara Morogoro

Spread the loveNaibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ametoa wiki moja...

ElimuHabari Mchanganyiko

Rubani mtarajiwa Tusiime awashangaza wazazi

Spread the loveWAZAZI walioshiriki siku ya taaluma na maonyesho ya shule ya...

Habari Mchanganyiko

Wanne wadakwa kwa kusafirisha punda 46 nje ya nchi

Spread the loveJeshi la Polisi kikosi cha kupambana na kuzuia wizi wa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Tutaendelea kupigania malengo ya afrika

Spread the loveRais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema dhamira ya Tanzania...

error: Content is protected !!