August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askofu: Viongozi wa dini ndio tatizo nchini

Spread the love

JOSEPH Bundala, Askofu wa Kanisa la Methodist Tanzania, Jimbo la Kati amesema, viongozi wa dini nchini ndio walezi wa vitendo viovu serikalini, anaandika Dany Tibason.

Amesema, matukio ya wizi, ulevi, ufisadi na ukiukwaji maadili kwa watumishi wa umma yanatokana na udhaifu wa viongozi wa madhehebu ya dini nchini katika kulea imani zao.

Bundala ametoa kauli hiyo jana muda mfupi baada ya kumalika kongamano la akina mama wa Kanisa Jimbo la Kati lililofanyika katika Kanisa la Methodist Ipagala, Dodoma.

Amesema, kutokana na viongozi wa madhehebu ya dini kushindwa kutoa mafundisho ya kweli kwa waumini wao, kumesababisha kuwepo kwa viongozi wengi ndani ya serikali na taasisi mbalimbali kutokuwa na hofu ya Mungu.

Amesema, viongozi wa dini zote wamekuwa wakihubiri mahubiri ambayo yanachanganywa na siasa ndani yake jambo ambalo haliwafanyi waumini kuwa na hofu ya Mungu.

“Haya matukio ya viongozi wa umma au taasisi mbalimbali kuhusika katika ufisadi, wizi, ulevi na kutokuwa na maadili ya kazi watu ambao wanastahili kulaumiwa ni sisi viongozi wa madhehebu ya dini ambao tumeshindwa kuwahubiria habari za ukweli na uwazi.

“Sisi viongozi wa dini tumekuwa tukitoa mahubiri mepesi sana na tatizo kubwa ni viongozi wa dini kuwatii zaidi viongozi wa serikali badala ya kumtii Mungu.

“Mahubili ya kweli yenye upako kwa viongozi wengi wa dini yameyeyuka kwa sababu ya kuwaogopa watumishi wa serikali na wakati mwingine wamekuwa wakiwatumia watu hao kwa faida binafsi” amesema Askofu Bundala.

Katika hatua nyingine amesema, sasa umefika wakati wa viongozi wa dini kufanya toba ya kweli ili Mungu aweze kuwasamehe kwani wamesababisha nchi kutokuwa na watendaji waadilifu.

“Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, ukiona watumishi wa serikali wanafanya mambo ya ajabu ujue ni matunda ya viongozi wa dini wamesababisha.

“Kila mtumishi wa umma au katika sekta mbalimbali anatoka katika dini fulani na huko kuna wahubiri wa neno la Mungu.

“Kwa maana nyingine wahubiri hao wameshindwa kuwafundisha na kuwafanya watu hao kuwa na hofu ya Kimungu,sasa unadhani kama hawana hofu ya Ki-Mungu unadhani watakuwaje waadilifu katika utumishi wao” amesema Askofu Bundala.

error: Content is protected !!