January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askofu Shoo: Umewakosea wenye ulemavu, omba toba

Spread the love

 

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kithuleri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo ametoa wito kwa wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini kuhakikisha wanapinga kwa nguvu zote ukatili wa kijinsia hususan kwa watu wenye ulemavu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Pi, amewataka watu wote ambao kwa namna moja au nyingine amewahi kuwafanyia ukatili wa kijinsia watu wenye ulemavu “kuomba toba na wabadilike.”

Askofu Shoo amesema hayo leo Jumanne, tarehe 30 Novemba 2021, jijini Dar es Salaam, katika uzinduzi wa “Mpango wa Haki Yangu, Changuo Langu” unaoratibiwa na shirika la wanawake katika sheria maendeleo barani Africa (WiLDAF), yenye lengo la kupinga vita ukatili wa kijinsia.

“Mungu aliyetuumba anatupenda sote na kuheshimu watu wote. Tumeshukudia watu wakionewa, kubaguliwa hasa watu wenye ulemavu na kuwasahau. Hili halikubaliki na tunapaswa kukemea vikali,” amesema

Kiongozi huyo wa kiroho amesema watu wenye ulemavu wamekuwa wakibaguliwa na kupitia mpango huo “tumekutana hapa na kusema Mungu hapendi unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kwa watu wote.”

Akisisitiza hilo, Askofu Shoo amesema “Mungu hapendi ukatili wa aina yoyote na tunawaomba wote ambao wameshiriki katika kuwatendea ukatili, waache, wabadilike na watabu.”

“Kuna haja ya kufanya toba kwa hawa kama umewaonea. Dini zetu zinapinga tabia hii na tunasimama na watu wenye ulemavu. Tunatoa wito kwa viongozi wa dini, kusimama pamoja kwa ajili ya kutetea hali za hawa ndugu zetu wenye ulemavu,” amesema

Amesema “ni imani yangu, tukiwa na nia njema, tunaweza kutokemeza vitendo vya ukatili kwa wanawake, vijana na watoto wenye ulemavu.”

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga aliyekuwa mgeni rasmi amesema, Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali ikiwemo kutenga Sh.8 bilioni za kujenga vyuo viwili.

Amesema, vyuo hivyo vitatenjwa mikoa ya Kigoma na Songwa “na sisi tunafanya mazungumzo na wadau wengine, watatujengea chou kingine mkoani Shinyanga. Tukifanya vizuri kwenye vyuo vya watu wenye ulemavu tutafanya vizuri zaidi.”

Ummy amesema, “watu wenye ulemavu wanapata sana ukatili kuliko watu wasio na wenye ulemavu. Tukishikamana kwa pamoja tunaweza kuushinda ukatili huu.”

Aidha, ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wanawake wenye ulemavu kufanya kazi kwa bidi kwenye maeneo mbalimbali “na kikubwa tujiamini, tusitumie kigezo cha ulemavu wetu kama sababu. Ukijiamini utafanikiwa na mimi naamini sisi wenye ulemavu tukiamua kufanya jambo, tunalifanya kwa ufanisi zaidi.”

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa WILDAF, Anna Kulaya amesema kampeni hiyo ya itasaidia kutokomeza ukatili kwa wenye ulemavu kwani “wanawake na watoto wenye ulemavu wamekuwa wakikutana na changamoto za ukatili wa kijinsia, zaidi ya wasio na ulemavu.”

Anna ameiomba serikali kuangalia namna ya kuanzisha madawati ya kijinsia mahususi kwa watu wenye ulemavu, ifahamike “linapokuja suala la madawati yenye watu wenye ulemavu, wanahitaji huduma maalum, kuwachanganya na watu wengine si sawa tunawanyima fursa fulani kutokana na mahitaji yao.”

error: Content is protected !!