MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo, amewataka Watanzania wasiwe na hofu juu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa ni mwanamke. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Kiongozi huyo wa kiroho amesema, Mungu atamtumia Rais Samia kuleta matumaini mapya Tanzania, kama alivyowatumia wanawake katika kufikisha habari njema za kufufuka kwa Bwana Yesu, katika siku ya Pasaka.
Askofu huyo ametoa wito huo tarehe 2 Aprili 2021, mkoani Kilimanjaro wakati akitoa salamu za Ijumaa Kuu ya Pasaka.
“Kipekee nitoe wito wangu kwa wale wote ambao wanafikra ambazo zimejengwa katika mfumo dume kwamba wanawake hawawezi, wakumbushwe habari hii ambayo Mungu kwa makusudi aliwatumia wanawake wale ndio wakaleta taarifa hii njema ya kufufuka kwa Yesu. Ya kwamba Mungu anawathamini sana wanawake,”amesema Askofu Shoo.
“Mungu alivyowatumia kina mama siku ya kufufuka Bwana wetu Yesu, mimi nina imani kabisa kama vile kina mama walivyokuwa wa kwanza kusuhuhudia tukio la kufufuka bwana wetu na wakawa wa kwanza kupeleka habari njema za matumaini.
Ndivyo hivyo ninavyoamini Mungu atamtumia rais wetu ambaye katika historia ya nchi yetu ni mwanamke wa kwanza, kwamba ataleta habari mpya ya matumaini kwa Watanzania wote,” amesema Askofu Shoo.
Mama Samia amekuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya juu ya uongozi, ambapo aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania, tarehe 19 Machi 2021, kufuatia kifo cha Hayati Dk. John Magufuli, kilichotokea katika Hospitali Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam.

Dk. Magufuli aliyeongoza Tanzania katika kipindi cha miaka mitano mfululizo na miezi kadhaa (Novemba 2015 hadi Machi 2021), alifariki dunia akiwa madarakani kwa ugonjwa wa mfumo wa umeme wa moyo, tarehe 17 Machi mwaka huu.
Akizungumzia utawala wa Rais Samia, Askofu Shoo amesema ana imani nao, kwani anaamini Mungu ameweka kitu ndani yake, hadi akamuinua kuwa Rais wa Tanzania.
“Mungu ameweka kitu ndani ya wanawake na nina imani ya kwamba ndani ya rais wetu Mungu amekwisha kuweka jambo ndani yake, sio leo lakini tangu utoto wake kwamba ipo siku atamuinua na kumfanya rais wa nchi hii,” amesema Askofu Shoo.
Askofu Shoo amesema KKKT ina matumaini makubwa na Rais Samia, na kutoa wito kwa Watanzania wote wamuombee ili atekeleze majukumu yake vyema.
“Sisi tuna matumaini makubwa na tunazidi kumuombea rais wetu, Mungu amjaalie ili awe mjumbe wa kuleta habari njema na za matumaini mapya kwa taifa letu la Tanzania,” amesema Askofu Shoo.
Sasa Rais Samia ni chaguo la Mungu au chaguo la Wananchi? Kama kila kiongozi anateuliwa na Mungu je Hitler je? Sultan wa Zanzibar je?