May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askofu Shoo azungumzia corona “tusimjaribu Mungu”

Askofu Frederick Shoo, Mkuu wa Kanisa la KKKT

Spread the love

 

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Frederick Shoo, amewataka viongozi wa kanisa hilo, kuwaelimisha waamini wake, kuchukua tahadhari ya maambukizi ya virusi hatari vya corona. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Askofu Dk. Shoo, ametoa ushauri huo kupitia barua yake ya kichungaji, aliyoandika kwa Maaskofu wa Dayosisi zote za KKKT na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya taifa ya kanisa hilo.

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, ni moja ya makanisa yenye wafuasi wengi nchini. Linatajwa kushika nafasi ya pili, nyuma ya Kanisa Katoliki.

Katika barua yake hiyo ya tarehe 26 Januari 2021, Askofu Dk. Shoo anasema, “kuchukua tahadhari ni wajibu, wala si kinyume na imani na wala siyo dhambi; na wala siyo kosa la jinai.”

Anaongeza, “kutochukua tahadhari, ni sawa na kumjaribu Mungu.” Amesema, neno la Mungu linatukumbusha likisema, “watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa.”

Amesema, “tukumbuke jibu la Bwana wetu Yestu Kristo kwa Ibilisi alipomjaribu nyikani. Ibilisi alimwambia Yesu ‘…ukiwa ndiwe mwana wa Mungu, jitupe chini; kwa maana imeandikwa, atukuagizia malaika zake wakulinde.’ Yesu akajibu, ‘imeandikwa, usimjaribu bwana Mungu wako.

Amesema, “ni wajibu wa wachungaji na viongozi wa kanisa la Mungu, kushiriki kikamilifu kuwapa watu wa Mungu maarifa sahihi, ili wasije kuangamizwa na COVID-19 au magonjwa mengine kwa kukosa maarifa. Maarifa ni pamoja na ufahamu sahihi wa hali halisi ili kujua namna ya kujikinga.”

Barua ya mkuu huyo wa KKKT, inaungana na wito wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), kuhusu tahadhari ya maambukizi ya corona.

Katika barua yake kwa Mwadhama, Mpelekwa wa Baba Mtakatifu, Maaskofu Wakuu, Maaskofu na Maaskofu Wastaafu, Rais wa TEC, Askofu Gervas Nyaisonga, ametaka kuchukulia tahadhari ya maambukizi mapya ya corona.

Barua ya rais wa TEC kwenda kwa viongozi hao, iliandikwa siku moja – tarehe 26 Januari 2021 – na barua ya Dk. Shoo. Haijaweza kufahamika kama viongozi hawa wawili, waliwasiliana kabla ya kutoa maandishi yao.

Ilipewa kichwa cha habari kisemacho: “Tahadhari juu ya maambukizi mapya ya virusi vya corona na ugonjwa wa Uviko 19 (COVID 19.”

error: Content is protected !!