August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askofu Ruwa’ichi ampinga Gwajima

Spread the love

 

ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Yuda Thadeus Ruwa’ichi, amewataka Watanzania wapuuze maneno yanayotolewa na baadhi ya watu wanaopinga chanjo ya Ugonjwa wa Korona (UVIKO-19). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Askofu Ruwa’ichi ametoa wito huo leo Jumanne, tarehe 24 Agosti 2021, katika Kituo cha Hija cha Pugu, jijini Dar es Salaam, wakati akihubiri kwenye adhimisho la misa takatifu ya mazishi ya Padri Paul Peter Haule.

Padri Haule aliyefariki dunia tarehe 18 Agosti 2021, kwenye Hospitali ya Kardinali Rugambwa, Ukonga, akipatiwa matibabu. Alikuwa Paroko Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Petro, Oysterbay mkoani Dar es Salaam.

Akizungumza katika ibada hiyo ya mazishi, Askofu Ruwa’ichi, amewataka Watanzania waachane na maneno hayo aliyosema yanatoka kwa kina ‘Gwajima.’

“Naomba niwakumbushe, ni utashi wa Mungu tuwe hai na tuwe na uhai tele. Kwa hiyo tuujali huo uhai, hao wanaopiga piga za kina Gwajima huko, achaneni nao.”

“Achaneni nao kabisa, hayo mazungumzo ya wanaotia shaka wanaopinga chanjo, hayo ndugu zangu muyaweke pembeni,” amesema Askofu Ruwa’ichi.

Miongoni mwa watu walioibuka hadharani kupinga chanjo hiyo ni, Mbunge wa Kawe (CCM) na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, aliyedai hakuna utafiti mahsusi uliofanywa kubaini usalama wa chanjo hiyo.

Hata hivyo, Serikali ya Tanzania, imekanusha madai hayo ikisema chanjo hizo ni salama kwa afya ya binadamu.

Akizungumzia umuhimu wa chanjo hiyo, Askofu Ruwa’ichi amesema ni vyema watu wakaipata ili kujihami na gonjwa hilo linaloitesa dunia tangu mwishoni mwa 2019.

“Sasa tujihami na tuendelee kumuomba Mungu atuhurumie, atunusuru na utuondelee hili janga. Linatuondolea uhai,” amesema Askofu Ruwa’ichi.

error: Content is protected !!