May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askofu Nkwande amtahadharisha Rais Samia

Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mwanza, Renatus Nkwande

Spread the love

 

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mwanza, Renatus Nkwande ametahadharisha Taifa kuingia kwenye mapenzi ya jinsia moja – ushoga na usagaji. Anaripoti Mwandishi Wetu, Chato … (endelea).

Amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa imara dhidi ya sheria zinazoweza kuhalalisha ‘ushetani’ huo, pia utoaji mimba katika utawala wake.

Kiongozi huyo wa kiroho ametoa ombi hilo leo Ijumaa tarehe 26 Machi 2021, katika Misa Takatifu ya kumwombea Hayati Rais John Magufuli (61), iliyofanyika katika Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Magufuli, uliopo Rumbabangwe, Chato mkoani Geita.

Misa hiyo imeongozwa na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Mkuu, Gervas Nyaisonga.

Akitoa mahubiri katika misa hiyo, Askofu Nkwande amesema, vitendo vya ushoga na utoaji mimba ni kinyume na mapenzi ya Mungu.

“Amerika juzi wamefanya kitu kinaitwa equality act (sheria ya usawa) ni upuuzi, tunaomba viongozi wetu tusije tukafika hapa, mnapokuwa bungeni, bungeni ni mahali patakatifu sio kuanza kuzungumza mambo ya kipuuzi, watu wabadili jinsia, watoe mimba,” amesema Askofu Nkwande.

“Naomba tusije kufikia hapo, nafikiri mama yetu (Rais Samia) unaelewa mambo haya. Tusaidie ili Tanzania ikiwezekana tusijesikia mambo hayo. Ushoga, kubadili jinsia ni upuuzi wa kujidanganya,” amesema.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Askofu Nkwande amemuomba Rais Samia kufuata nyayo za mtangulizi wake, Dk. Magufuli za kumtanguliza Mungu katika kila jambo, hususan katika kuiongoza nchi.

Wito huo wa Askofu Nkwenda ameutoa wakati anazungumzia uamuzi wa Dk. Magufuli kuliongoza Taifa katika mapambano dhidi ya virusi vya corona, kwa kumtegemea Mungu zaidi badala ya sayansi.

“Hata wakati wa hofu kubwa ya corona ilipotanda ulimwenguni, yeye alikuwa tayari kutofautiana na wengi kwa maslahi ya watu wake. Magufuli ametuachia kitu muhimu kwetu kumuogopa Mungu, badala ya kutegemea sayansi na utafiti,” amesema Askofu Nkwenda.


Tangu mlipuko wa virusi vya corona uingie nchini Tanzania Machi 2020, Dk. Magufuli aliwahimiza Watanzania kumuomba Mungu ili alitokomeze janga hilo.
Akimzungumzia Dk. Magufuli, Askofu Nkwenda amesema, alitoa maisha yake kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania.

Amesema, licha ya Dk. Magufuli kusumbuliwa na maradhi ya moyo kwa zaidi ya miaka 10, alifanya kazi usiku na mchana bila kupumzika, akiwatumikia Watanzania, hadi umauti ulipomkuta akiwa madarakani.

“Rais Magufuli pamoja na kuhangaika kwa miaka mingi na maradhi ya moyo, hakuchoka kutupigania sisi Watanmzania.

“Amekufa akihangakia Watanzania watoke kwenye aibu ya umasikini, tulikuwa tunachekwa kila mahali Tanzania,” amesema Askofu Nkwenda.

Dk. Magufuli amefariki dunia tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu ya ugonjwa wa mfumo wa umeme wa moyo.

Mwili wake unatarajiwa kuzikwa leo katika makaburi ya familia kijijini kwao Chato.

Kiongozi huyo alifariki akiwa madarakani, miezi minne tangu alipoapishwa kuongoza muhula wake wa mwisho wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Dk. Magufuli aliapishwa tarehe 5 Novemba 2020, baada ya kushinda kiti cha Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Kwa mara ya kwanza Dk. Magufuli aliingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015, baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu.

error: Content is protected !!