Thursday , 2 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Askofu Niwemugizi ampa mitihani sita Rais Samia, alia na mauaji
Habari za SiasaTangulizi

Askofu Niwemugizi ampa mitihani sita Rais Samia, alia na mauaji

Spread the love

 

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara mkoani Kagera, Severine Niwemugizi amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kushughulikia changamoto sita zinazoikabili wilaya hiyo hususani tatizo la mauaji linalowatikisa kwa muda mrefu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kagera … (endelea).

Askofu Niwemugizi ametoa kauli hiyo leo tarehe 22 Februari, 2022 mjini Ngara mkoani Kagera wakati akitoa salamu za shukrani kwa wageni waliohudhuria sherehe za Jubilee ya miaka yake 25 ya uaskofu wake.

Katika sherehe hizo Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi huku maaskofu mbalimbali wa majimbo yote Tanzania wakihudhuria.

Askofu huyo akitumia msemo wa ‘Mgeni njoo mwenyeji apone’ alimuomba Rais Samia kutatua changamoto hizo.

“Ukipata bahati ya kukutana na mfalme mweleze hapohapo shida zako zote. Wapo wapiga kura wako wengi sana wenye changamoto zinazoumiza mioyo yao lakini hawana namna ya kuzifikisha kwako, pengine zikitolewa huku chini zina zimwazimwa,” amesema.

Niwemugizi ameanza kutaja changamoto hizo kuwa ni mgogoro wa ardhi wa eneo la kanisa kuu la mji huo ambapo alidai eneo hilo lilikodishwa kwa muda kwa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) mwaka 1994 hadi 1996 lakini liliporejeshwa Halmashauri ya mji huo ilichukua eneo hilo kibabe.

Amesema licha ya kuwa na vielelezo vya kutosha kuandika barua kwa mkuu wa wilaya wakati huo anasimikwa kuwa Askofu wa jimbo hilo la Rulenge, bado hakuna hatua zilizochukuwa.

Hata hivyo, Rais Samia amemuahidi kumsimamia Waziri wa Tamisemi, Inocent Bashungwa ambaye aliahidi kushughulikia suala hilo.

Rais Samia amesema atalisimamia kuhakikisha haki inapatikana.

Pili, Askofu Niwemugizi amemuomba Rais Samia kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kusamehe madeni yanayowaelemea katika hospitali zinazomilikiwa na jimbo hilo ambazo ni Biharamulo hospitali inayodaiwa Sh milioni 113 na Rulenge inadaiwa Sh milioni 213.

Amesema madeni hayo ni ya kutoka mwaka 2015 hadi 2020 ambapo licha ya hospitali hizo kuhudumia wananchi masikini ambao muda mwingine hawawezi kulipia huduma bado wanadaiwa mapato hayo na TRA.

Hata hivyo, akijibu hoja hiyo Rais Samia amesema tayari amekaa mara tatu na viongozi wa dini ambao wamefikisha kilio hicho.

Rais Samia amesema katika utafiti walioufanya walibaini hospitali hizo zinazomilikiwa na madhehebu ya dini, zinatoza gharama za matibabu sawa na hospitali binafsi.

Aidha, amesema wanaendelea kufanya tathmini ili kubaini hospitali zinazomilikiwa na taasisi za kidini ili kuona kama zinafaa kusamehewa madeni au kupunguziwa mzigo huo.

Changamoto ya tatu, Askofu Niwemugizi ameitaja kuwa ni shida ya maji ambayo alisema anajua wasaidizi wa Rais hawawezi kumuambia.

Niwemugizi amemkumbusha Rais Samia kuwa Hayati Rais John Magufuli alifanya mkutano wa hadharani jimbo hapo akiwa ameambatana na Rais wa Burundi wakati huo, Hayati Piere Nkurunzia na kuahidi kutoa pesa za kutatua tatizo hilo.

Aidha, akijibu hoja Rais Samia amesema hadi sasa katika wilaya hiyo huduma ya maji imefikia asilimia 63.7 wakati lengo likiwa ni asilimia 85 hivyo kuna Sh milioni 793 zimetengwa kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu, kujenga mtandao wa mabomba na kukarasbati miundombinu ya maji katika mji wa Ngara.

Rais Samia ameongeza hadi sasa Sh milioni 100 imetolewa kwa Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira kwa ajili ya uchimbaji wa kisima hicho na shughuli ya uchimbaji inaendelea.

Aidha, amemuagiza Waziri wa Maji, Juma Aweso kufuatilia shughuli hiyo na matumizi ya fedha hizo kabla ya kutoa nyingine.

“Lakini wizara ya maji kupitia Mamlaka ya Maji Bukoba (Buwasa) iliingia mkataba na mtaalam mshauri kwa ajili ya kusanifu mradi wa maji utakaondoa tatizo la upatikanaji wa maji Ngara na vijiji jirani saba.

“Usanifu umekamilika na hatua ya kumpata mkandarasi wa kujenga mradi huo upo hatua za wizara.,” amesema

Akitaja changamoto ya nne, Askofu Niwemugizi kumekuwapo na walanguzi wa mazao ya wananchi wa Ngara hususani zao kahawa ambapo hufika kununua mazao hayo kwa wakulima kwa bei rahisi hata kabla hayajakomaa.

Akizungumzia suala hilo, Rais Samia amemuagiza waziri husika kusimamia suala hilo iuli kukomesha tabia hiyo.

Pia amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wanaofika katika miji ya kuwekeza kwani sio wote ni walanguzi.

Tano, Askofu Niwemugizi amesema katika mradi wa uchimbaji wa madini ya Nikeli ambao unatarajiwa kufanyiwa katika mji huo, wapo wavamizi wanaowahamisha wenyeji.

Amesema wavamizi hao kutoka mikoa ya Shinyanga na Mwanza, wananunua maeneo ya wenyewe na kwenda kuotesha migomba huko kwenye pori.

Akizungumzia suala hilo, Rais Samia ametoa wito kwa wananchi kutokubali kutumika na kuachia maeneo yao kwa kuwa watakwamisha maendeleo katika eneo lao.

Ametole mfano mkoani Mara ambako kuna eneo wananchi zaidi ya 6500 wanatakiwa kufidiwa lakini imebainika zaidi ya wananchi 5000 ni wavamizi.

Akizungumzia mnyororoyo wa thamani Rais Samia amesema wameamua kujenga kiwanda kuongezea thamani katika mji wa Buzwagi badala ya Ngara kwa kuwa kuna huduma muhimu hivyo kumepunguza gharama za uwekezaji.

Askofu Niwemugizi pia ameitaja changamoto kubwa ya sita kuwa ni matukio ya mauaji na watu kujiua ambayo yametia doa Taifa.

“Shida kubwa nionavyo mimi mara nyingi tunajishughulisha na matokeo badala ya kutatua chanzo cha matokeo. Jambo hili linahitaji mjadala wa kitaifa, katika makundi yetu mbalimbali kama taifa tutafakari na kutafuta sababu chanzo cha mauaji haya nini na nini tufanye kuzuia haya matukio haya kuitokea.

“Imefika mahali dhamiri za watu wengi zimeonekana kama zimekufa kabisa, watu hawaoni maisha na utu wa watu wengine kama ni tunu takatifu za kuheshimiwa na kulindwa kwa gharama yoyote,” alisema Askofu Sverine Niwemugizi ambaye aliongeza kuwa ameitisha mkutano na viongozi wa dini wa wilaya hiyo kutafakari suluhu ya tatizo hilo.

Akikazia suala hilo Rais Samia alisema takwimu zinaonesha katika wilaya ya Ngara peke yake mwaka 2020 kulikuwa na matukio 22 ya mauaji na mwaka 2021 kulikuwa na matukio 21.

Pia mwaka 2020 kulikuwa na matukio matatu ya watu kujiua na mwaka 2021 kulikuwa na matukio mawili ya watu kujiua.

Kutokana na hali hiyo Rais Samia alitoa wito kwa viongozi dini zote kuzungumza na waumini wao kwenye suala hilo la kujali utu na kuthamini uhai wa mweziwe.

Pia amesema kwa kuwa suala hilo pia linagusa maadili, sasa litaingiza kwenye somo la uraia ambalo ili kuwafunda watoto wakiwa wadogo katika shule za msingi.

“Tuna kazi kubwa ya kufanya kuwaambiwa kinachotokea sicho tulichoamrishwa katika dini zetu, hakuna mila na desturi zinazomrisha watu wakauae, kwa hiyo kiongozi wenzangu tuna jukumu kubwa la kufanya.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Kamati ya Bunge yaitaka Serikali ichukue hatua kudhibiti mfumuko wa bei

Spread the love  SERIKALI ya Tanzania imetakiwa kufanya tathimini dhidi ya changamoto...

Habari za Siasa

Bunge lataja kinachokwamisha Mradi wa Mchuchuma na Liganga

Spread the love  MRADI wa uchimbaji chuma cha Liganga na Makaa ya...

Habari za Siasa

Chongolo aagiza watendaji wanaoonyesha mianya ya rushwa wakamatwe

Spread the love   KATIBU mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa...

Habari za Siasa

TRA iweke mfumo wa msamaha wa kodi kutekeleza miradi

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kimeitaka Mamlaka ya Mapato...

error: Content is protected !!