December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askofu: Msiogope kubadilisha katiba

Joseph Bundala, Askofu Mkuu wa Kanisa la Methodist Tanzania

Spread the love

JOSEPH Bundala, Askofu Mkuu wa Kanisa la Methodist nchini Tanzania amezitaka taasisi za dini kufanya mabadiliko ya katiba zao, ili ziendane na wakati .Anaripoti Danson Kaijage…(endelea).

Akizungumza hivi karibuni jijini Dodoma, Askofu Bundala amewataka watu kutoogopa kuzifanyia marekebisho katiba, kwa kuwa nyakati zimebadilika hivyo katiba zao haziwezi kidhi matakwa ya mabadiliko hayo.

“Niwaombe watu wasiogope kubadilisha katiba zao, maana nyakati zinabadilika, mambo yanabadilika inakuwa ni mapya. Kwa hiyo ni vizuri tukakaa kwa pamoja na kwa umoja, tukafanya mabadiliko mazuri katika katiba zetu,” amesema Askofu Bundala na kuongeza;

“Ni ombi hata kwa makanisa mengine ambayo hayajafanya hivyo, katiba zao zimekuwa za miaka mingi. Tunamshukuru Mungu tulikuwa na kazi kubwa ya kufanya marekebisho ya katiba yetu ambayo miaka mingi ilitengenezwa, lakini Mungu ni mwema ametujaalia tumemaliza salama.”

Aidha, Askofu Bundala amewataka Watanzania kushiriki vyema katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu, kwa kuchagua viongozi sahihi

“Nawaasa Watanzania wenzangu tuchague viongozi wanaotufaa na kutupeleka mahali sahihi. Tuweze kuangalia kwa umakini tupate viongozi wazuri wenye nia nzuri na mawazo sambamba yanayoendana na Rais John Magufuli,” amehimiza Askofu Bundala.

Askofu Bundala ameeleza kuwa, kanisa lake limefanya maombi ili uchaguzi huo ufanyike kwa amani pasina fujo na vurugu.

“Tumeomba sana kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika hivi karibuni, tumemuomba Mungu aweze kutuepusha na fujo na vurugu,” amesema Askofu Bundala.

error: Content is protected !!