January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askofu Mshana akemea biashara kanisani

Keki yenye umbo la Kanisa la iliyokusudiwa iuzwe kanisani KKKT Usharika wa Kanisa Kuu Dodoma, ambapo Msaidi wa Askofu ambaye ndiye Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo Samwel Mshana alikataa kanisa lake kufanywa mahali pa biashara.

Spread the love

MSAIDIZI wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma, Samwel Mshana, amekemea vikali na kuwaonya waandaaji wa Tamasha la kutangaza amani, imba na badilisha kipato kuwa ajira, akisema kanisa ni nyumba ya ibada si mahali pa biashara. Anaandika Bryceson Mathias … (endelea).

Askofu Mshana alitoa rai hiyo Jumatatu ya Pasaka, ambapo kwenye tamasha la uimbaji wa kwaya mbalimbali lililoandaliwa na RASI FM Radio, waliweke tukio la kukata keki ya biashara yenye umbo la kanisa. 

Akifungua tamasha hilo kwenye Kanisa Kuu la KKKT Dodoma, Askofu Mshana ambaye ndiye Mchungaji kiongozi wa usharika huo, aliwajia juu waandaaji hao akisema, kuna mambo matatu hayakumfurahisha wanayotakiwa kuyakomesha mara moja.

“Kwenye ratiba yenu kipengele cha tisa, mmeonesha kuna kukata keki ya biashara, napenda niwaonye kanisani si mahali pa biashara; Hivyo sitaki kuona kwenye Kanisa lolote la KKKT Dodoma ninaloliongoza, kunafanywa biashara. Kama kuna biashara hiyo, ikafanyiwe nje ya Kanisa,”alikemea Mshana.

Ameonya kuwa kanisa ni mahali pa kusifu na kuabudu; Ni nyumba ya ibada, ambapo watu wanaomba, wanaimba na kuponywa magonjwa, huzuni na taabu zao ili wapate furaha na  kuhuishwa uhai wa kiroho na miili yao. 

“Tunasoma katika Luka 19:45, Yesu akaingia hekaluni akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara , akiwaambia imeandikwa, nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi, msifanye hivyo hapa,”amesema.

Baada ya kiongozi wa uandaaji wa tamasha hilo, kukiri kuwepo na makosa ya uchapaji na kwamba, tukio hilo halitafanyika, Askofu Mshana alifungua uimbaji huo akiwataka waimbaji wawe kama Mariam Magadalene, ambaye alijua umuhimu wa Kanisa na Yesu. 

error: Content is protected !!