August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askofu Malasusa kuibua gogoro KKKT

Spread the love

DK. Alex Malasusa, Askofu mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), ameanza mchakato wa kubadilisha katiba ya kanisa lake ili kuzuia kung’olewa madarakani. Anaandika Mwandishi Wetu.

Askofu Dk. Malasusa amelenga kubadilisha katiba ya kanisa hilo ili kuzuia mkuu mpya wa KKKT, Frederick Shoo, kuingilia kati mgogoro unaofukuta ndani ya Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Taarifa kutoka ndani ya kanisa hilo zinasema, Kamati Maalum ya mabadiliko ya katiba, tayari imeelekezwa kuondoa ndani ya katiba ya DMP, kifungu kinachoipa nguvu KKKT na mkuu wake kuingilia mgogoro wowote wa kanisa hilo na kumchunguza askofu wa dayosisi hiyo.

Mabadiliko ndani ya DMP yanafanyika takribani miezi mitano baada ya Askofu Dk. Malasusa kuondolewa katika wadhifa wa mkuu wa KKKT.

Aidha, mabadiliko ya katiba ya kanisa la Askofu Dk. Malasusa yanakuja miezi mitatu tangu kiongozi huyo kutuhumiwa kujihusisha kimapenzi na mchungaji wa kanisa lake na ambaye ni mke wa mtu.

Anayetajwa kuwa na uhusiano wa kingono na Dk. Malasusa, ni Leita Ngowi, mchungaji na mkurugenzi wa idara ya wanawake usharika wa Azania Front, jijini Dar es Salaam.

Leita ni mke wa Venance Mwakilima, mkazi wa eneo Vikawe, Bagamoyo, ambaye ni mfanyakazi wa Shule ya Msingi Dunda, wilayani Bagamoyo.

Dk. Malasusa anadaiwa kuwa na uhusiano na aliyepandishwa cheo siku za karibuni na askofu huyo.

“…huyu bwana (Askofu Malasusa) anahofia kuwa uchunguzi ukifanyika kama ambavyo baadhi ya wachungaji wameomba kwa mkuu wa kanisa, uchafu wake utajulikana,” ameeleza kiongozi mmoja ndani ya DMP.

Anasema, “hakuna haja ya kuwa na mabadiliko ya aina hiyo. Wala hakuna haraka ya marekebisho ya katiba, wakati marekebisho ya mwisho yalifanyika miaka miwili iliyopita.”

Akiongea kwa uchungu mtoa taarifa huyo anasema, “…anataka kufanyia mabadiliko katiba yetu ili kuzuia asiweze kuchunguzwa. Sisi wengine tunamshangaa sana, kwa nini dhambi ya watu wawili tunabebeshwa kanisa zima?”

Taarifa zinasema, ni kawaida kwa katiba ya DMP kubadilishwa kwa manufaa ya mtu binafsi.

Mara ya mwisho mabadiliko kwenye katiba ya DMP yalifanyika ili kumuondoa mchungaji mmoja ambaye alipendekezwa kuwa msaidizi wa askofu.

Anasema, “katika mabadiliko yake, Askofu wa DMP amepewa mamlaka makubwa ya kuteua msaidizi wake; kwa sasa msaidizi wa Askofu, ni kama anapendekezwa na Askofu kisha kuthibitishwa na mkutano mkuu.”

Kabla ya mabadiliko hayo, msaidizi wa Askofu alikuwa anapendekezwa na kamati mahususi ya uteuzi inayotokana na Halmashauri Kuu ya Dayosisi.

Akiongea katika mkutano wa watumishi ulioitiswa kwa dharura ili kushawishi “watumishi kuwa na kauli moja” juu kile kinachoitwa, “yanayoendelea kwenye magazeti kuhusu Askofu Malasusa,” msaidizi wa Askofu huyo alidai, yote yanayoandikwa kuhusu bosi wake, “hayana ukweli.”

Alisema, “haya mambo yanayoandikwa kwenye magazeti kuhusu mkuu wa kanisa ni uzushi na uongo mtupu.”

Hata hivyo, msaidizi wa Askofu alizuia wauamini kuhoji kwa nini magazeti yameamua kumuandama Askofu Malasusa wakati huu na siyo wakati alipokuwa kiongozi mkuu wa KKKT.

Aliishia kuwataka wajumbe kufanya maombi kwa kanisa na kiongozi wao.

Wakati msaidizi wa Askofu Malasusa akieleza wajumbe anachoita, “uongo wa magazeti,” Mchungaji Leita alikuwa ameketi mbele na viongozi wengine wa dayosisi hiyo.

Alikuwa kimya, mwenye majonzi na aliyeonekana kuwa na kitu kinamsumbua moyoni mwake.

Mwandishi wa habari hii aliyefanikiwa kujipenyeza ndani ya mkutano huo alimnukuu mmoja wa wutumishi akilalamikia namna ya viongozi wa dayosisi hiyo wanavyolishughulikia suala hilo.

“Wamefanikiwa kuwatiisha baadhi ya viongozi wa DMP, lakini hawatafanikiwa kutuziba mdomo wengine. Hatuwezi kukubali kuwa makasuku kwamba eti kashfa ya askofu ni ya kitaasisi na siyo binafsi,” ameeleza Mchungaji mmoja ambaye hakupenda kutajwa jina.

Akiongea kwa hisia kali, mchungaji huyo alisema, “… uzinzi unawezaje kuwa wa taasisi? Hawa watu wanazungumza kama wasiofahamu Biblia?

“Ndani ya Bibilia, kumeandikwa kuwa Mfalme Daudi alimuua Uria, ambaye alikuwa Jemedari wake wa vita. Mungu hakuifanya dhambi ile kuwa ya Israel. Alimwadhibu Daudi na sio taifa zima. Hatuwezi kuifanya dhambi ya Askofu Malasusa kuwa dhambi ya kanisa zima. Haiwezekani.”

Akizungumza katika mkutano huo, mchungaji Ernest Kadiva, naibu katibu mkuu utawala, alitangaza kuanza kwa mchakato wa mabadiliko ya katiba ya DMP, kwa kusema “hautafanyika kupitia vikao mahususi kama ilivyozoeleka.”

Mchungaji Kadiva ambaye likuwa pia mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba alisema, mabadiliko ya ya Katiba ya DMP yanayofanyika sasa, “yanataka kila mwenye maoni kuwasilisha mapendekezo yake kwa maandishi” kwake.

Mabadiliko haya ya katiba ya DMP yakifanyika, utakuwa “ushindi mkubwa” kwa Askofu Malasusa. Atakuwa amefanikiwa kufanya mambo mawili:

Kumzuia kisheria Askosu Shoo kushungulikia mgogoro mkubwa unaofukuta katika kanisa lake na kuzuia kuumbuliwa katika kashfa ya ngono inayomkabili.

error: Content is protected !!